NSSF, Dowans, Muhimbili na Tanesco, zanyooshewa kidole
29th April 2009
Shirika la Umeme (Tanesco).
Mashirika kadhaa ya umma na taasisi
nyeti za serikali yamepuuza mapendekezo ya ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti
Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) yaliyotakiwa kufanyiwa kazi, kwani
kasoro zilizogundulika na kutakiwa kurekebishwa zimeendelea kuwepo mwaka
mmoja baadaye.
Kasoro hizo ni uvunjaji wa kanuni za
matumizi ya fedha za walipa kodi ambazo katika kipindi cha ukaguzi
kilichopita zilitakiwa kufanyiwa kazi.
Kwa mujibu wa ripoti ya Ukaguzi wa
Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha 2007/08 iliyowasilishwa bungeni
juzi, baadhi ya taasisi hizo ni Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya Taifa
(NSSF), Shirika la Umeme (Tanesco), Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)
na taasisi nyingine nyeti za serikali.
Kwa hospitali ya Muhimbili, kwa mfano,
ripoti inaonyesha kwamba kuna jengo binafsi lililojengwa katika eneo la
hospitali ambalo mkataba unaonyesha kwamba lilitakiwa kuwa mali ya
hospitali kuanzia mwaka 1992, lakini limeendelea kuwa mali ya mtu huyo,
H.A Kiluvia.
Imeelezwa kuwa jengo hilo kwa sasa kuna benki ya National Microfinance Bank (NMB) na duka la dawa.
“Mkataba umeshamalizika lakini jengo bado
liko kwenye himaya ya H. A. Kiluvia kinyume na makubaliano ya mkataba
(licha ya mapendekezo yetu ya mwaka 2006/07),” imesema sehemu ya ripoti
hiyo.
Ofisi ya CAG pia ilipendekeza, katika
ripoti yake iliyopita, kusitishwa kwa mkataba wa Kampuni ya Kuhudumia
Makontena Bandarini (TICTS) kutokana na kuongezewa kipindi kingine cha
miaka 15 kinyume cha sheria, lakini mkataba bado haujavunjwa hadi ripoti
hiyo inaandikwa.
Ripoti inaonyesha kwamba ofisi ya CAG
ilipofuatilia mapendekezo hayo yaliyotolewa mwaka 22 06/07, haikupata
majibu, hali inayoonekana kwamba hakuna utekelezaji kwa upande wa
serikali.
Kadhalika, CAG anasema katika ripoti yake
kwamba Tanesco ilishauriwa kuidai kampuni ya M/s Dowans Holdings tozo
(liquidated damage) kutokana na kampuni hiyo kukiuka mkataba kwa
kushindwa kuzalisha umeme wote wa megawati 100 kama mkataba
unavyoonyesha.
Ripoti inaonyesha kwamba ofisi ya CAG haikupata majibu kuhusu utekelezaji wa mapendekezo hayo.
Ofisi ya CAG pia ilipendekeza kwa Hazina
kukusanya madeni yatokanayo na mauzo na ubinafsishaji wa mashirika ya
umma kutoka kwa wawekezaji.
Ilipendekeza pia kwamba hatua za kisheria
zichukuliwe dhidi ya wawekezaji walioshindwa kutekeleza majukumu yao ya
mikataba ya uwekezaji.
Pia ilipendekeza kwamba mashirika na
taasisi za umma ambazo bado zinajiendesha kwa hasara zichukuliwe na
serikali au kuuzwa tena.
Hata hivyo, ripoti inasema kwamba mapendekezo hayo hayajafanyiwa kazi hadi ripoti mpya ilipokuwa ikiandaliwa.
Kuhusu NSSF, ofisi ya CAG ilipendekeza
isiendelee kukopesha na kwamba kiasi cha mikopo kilichoripotiwa ni
kikubwa kuliko inavyotakiwa.
Hata hivyo ripoti inaonyesha kwamba ushauri haukuzingatiwa.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment