Benki kupiga mnada Mgodi wa Kiwira
12th March 2011
Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja
Mgodi wa Makaa ya Mawe Kiwira ambao
uligeuzwa kuwa kitega uchumi cha kujipatia fedha za kukopa kutoka
taasisi mbalimbali za fedha nchini hivi sasa madeni hayo yameanza
kuutokea puani ambapo Benki ya CRDB imeandika barua kwa serikali
ikielezea kusudio lake la kutaka kuupiga mnada mgodi huo.
Mgodi huo ambao hadi sasa upo chini ya
mwekezaji wa kampuni ya Kiwira Coal and Power Limited (KCPL) licha ya
serikali kupitia Waziri wa Nishati na Madini, William Ngereja, kutoa
taarifa kuwa umerejeshwa serikalini, hadi sasa unadaiwa madeni na
taasisi mbalimbali za fedha zaidi ya Sh.28,869,938,996.
Taasisi za fedha ambazo zinaudai mgodi
huo ambazo zilikopwa na mwekezaji ni pamoja na CRDB deni lote pamoja na
riba ni Sh.bilioni 4.077, Mfuko wa Pesheni kwa Watumishi wa Umma (PSPF),
Sh.bilioni 9.497 na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Sh.
bilioni 15.294.
Madeni hayo kwa mgodi huo yalibainika
wakati Mkurugenzi wa Mipango, Uwekezaji na Miradi wa NSSF, Yakubu
Kidula, alipokuwa akitoa taarifa juu ya pendekezo la NSSF la kuchukua
kampuni ya Kiwira Coal and POWER Limited kwa wabunge wa Kamati ya
Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAOC).
Alisema kutokana na hali hiyo, Benki ya
CRDB imechukua hatua ya kuiandikia barua serikali ikielezea kusudio la
kutaka kuupiga mnada mgodi huo kwa kushindwa kulipa deni hilo ambalo
mwekezaji huyo alikopa Dola milioni saba kwa lengo zitumike kuzalisha
umeme megawati 50.
Kidula alisema hata hivyo, NSSF wameiomba
Benki ya CRDB isitishe uamuzi wake wa kutaka kuupiga mnada mgodi huo
kwasababu NSSF inakusudia kuwa mwekezaji mpya wa mgodi ambapo
itachukua jukumu la kulipa madeni yote yanayodaiwa na taasisi zote
zinazoudai mgodi huo.
Kwamujibu wa barua ya CRDB yenye kumbu
Na. 3390/654316/4113 ya 28 Julai 2009 ambayo NIPASHE imepata nakala,
aliandikiwa Ngeleja, ikitaka serikali kulipa deni hilo lililokopwa na
mwekezaji wa kampuni ya Kiwira Coal and Power Project (KCPL) kwa ndiye
mdhamini mkuu wa mkopo huo.
Hata hivyo Septemba 5 , 2009 Waziri wa
Nishati na Madini, William Ngeleja, katika barua yake yenye kumbu Na.CDA
48/171/01 aliijibu Benki ya CRDB kwa kueleza kuwa wizara yake ingefanya
kazi kwa kushirikiana na wakopeshaji ili kuhakikisha kuwa suala hilo
linatatuliwa mapema iwezekanavyo.
Februa mwaka jana, CRDB ilimkumbusha
Waziri wa Nishati na Madini kuhusiana na kushindwa kwa kampuni ya KCPL
kulipa deni lake na kueleza kuwa hatua iliyobaki ni kwa wakopeshaji
kuuza mgodi wa KCPL kwa mnunuzi yeyote ili kurudisha fedha
walizoikopesha KPCL.
Pamoja na mfululizo wa barua
zilizoandikwa na CRDB, wizara iliendelea kukaa kimya ambapo Disemba
mwaka jana (2010) Benki ya CRDB iliandika barua ngingine kwa Waziri
yenye kumbu Na. 3390/654316/4113 ikimtaarifu kwamba wakopeshaji hawana
njia nyingine zaidi ya kuuza Mgodi wa Kiwira.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment