Mafao chini ya NSSF ni ukombozi wa wengi, wanachama zindukeni
13th December 2009
Maoni ya katuni
Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii
(NSSF) ni moja ya mifuko ya hifadhi ya jamii nchini ambalo limepania
kujenga maisha bora ya wanachama wake sasa na baadaye. Kudhihirisha
hilo, shirika limejikita katika kutoa kinga kwa wanachama wake zaidi ya
460,000 hivi sasa kutokana na majanga ya kiuchumi na kijamii ambayo
husababishwa na kupungua kwa kipato.
Mwishoni mwa wiki, uongozi wa juu NSSF
uliandaa mkutano mjini Zanzibar ambao uliwashirikisha wahariri toka
vyombo vikuu vya habari nchini kuwaelimisha pamoja na mambo mengine
huduma zitolewazo na mfuko na namna shirika lilivyojipanga kuboresha
maisha ya wanachama wake siku za usoni.
Akitoa mada katika mkutano huo,
Mkurugenzi Mkuu NSSF, Dk.Ramadhan Dau aliwahakikishia wanachama kwamba
mfuko uko imara kwa miaka 20 ijayo, hivyo wasiwe na wasiwasi na wale
ambao hawajajiunga kufanya hivyo hima.
Alisema kwa sasa NSSF ina vitenga uchumi
vyenye thamani ya sh. bil.848.8 kwa mapato ya bil.58.3/- ilipofika Juni
mwaka huu, ikilinganishwa na vitega uchumi vya bil.670.3/- kwa pato la
bil.43.9/- mwaka uliotangulia. Malengo mwaka 2009/2010 ni kuwekeza
vitega uchumi vya tril.1,078.2/- kwa pato la bil.89.7/-
NSSF imeongeza idadi ya mafao toka matano
ya awali na kufikia saba hivi sasa. Mafao ya muda mrefu ni pensheni ya
uzeeni, mafao ya mkupuo maalum, pensheni ya ulemavu na pensheni ya
urithi. Yale ya muda mfupi ni mafao ya matibabu, mafao ya uzazi, mafao
ya kuumia kazini na mafao ya mazishi.
Mafao yote haya, hakika, yamelenga kumpa
ahueni ya maisha mwanachama pindi atakapokuwa hajiwezi kutokana na
majanga ya kiuchumi na kijamii. Pamoja na ukweli huo, kama alivyoeleza
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, bado wapo wanaosita kuchangamkia mafao hayo
hasa fao la matibabu pamoja na kwamba ni wanachama wakihofia kukatwa
pensheni. “Huduma hiyo ni bure hakuna makato”, alisistiza Mkurugenzi wa
Matekelezo NSSF, Crescentus Magori katika mada yake.
Pamoja na ukweli kwamba fao la matibabu
ni bure lakini ni idadi ndogo sana ya wanachama waliojitokeza kupata
huduma hiyo. “Zilitengwa sh. bil.3/- mwaka 2004 lakini hadi sasa ni mil.
100 tu zilizotumika. Watu bado hawaamini…ni wachache sana wamejitokeza
kuliko ilivyotegemewa”, alisema Dk.Dau.
Hata sisi tunajiuliza, kwanini walengwa
wanasita kutibiwa bure kupitia fao hilo la matibabu? Je, ni elimu
haijawafikia vema kuhusu fao hilo au ni kitu gani. Utafiti wa kina yafaa
ufanywe kujua tatizo liko wapi.
Lakini hata hivyo, huduma hiyo ni nzuri na muhimu hasa ikizingatiwa kuwa ni ya bure kwa wanachama wa mfuko huo.
Pia NSSF imeonesha mfano wa kuigwa kwa
kuongeza kiwango cha pensheni kwa wanachama kuanzia Septemba mwaka huu
kutoka sh.33,200/- hadi 52,000. Hii ni katika jitihada zake za kuwajali
wanachama wake.
Ni mfuko uliojiwekea malengo hadi miaka
50 ijayo. Lakini ili ufike huko, yapo mambo mengi yamewekewa mkakati
ikiwa ni pamoja na kutaka yawepo maboresho ya sheria zinazolinda mifuko
ili iweze kuendelea, kuimarika na hatimaye idumu.
Kwa mfano, Dk.Dau anasema, waliojiajiri
wenyewe, sheria haiwalazimishi kujiunga na NSSF. Hawa nao mfuko unataka
wajiunge. Au mtu akiacha kazi asipewe fedha zake hadi atimize muda wa
kustaafu. Kwa sasa mtu anaruhusiwa kuchukua fedha zake kabla ya
kustaafu. Utaratibu huu unatishia maisha ya mfuko wa hifadhi.
Wengine wanataka kuchangia lakini
wanachagua fao mojawapo. Kisheria ni lazima wanaojiajiri wenyewe
wachangie mafao yote saba, jambo ambalo hawalikubali.
Tunaamini kwamba mamlaka husika
zimeshafikishiwa mapendekezo hayo kuona uwezekano wa kuyafanyia kazi ili
NSSF na mifuko mingine ya hifadhi ya jamii iweze kudumu na kuendelea
kutoa huduma kwa wanachama wake.
Siyo siri kwamba mafao ya NSSF yanagusa
makundi muhimu ndani ya jamii yetu ambayo ni wazee, walemavu, wanawake
na watoto, wafanyakazi na kadhalika, hivyo serikali inapaswa kuunga
mkono juhudi zake zilizolenga kujenga maisha ya wanachama wake sasa na
baadaye.
Ni imani yetu kwamba waajiri na
wafanyakazi wote katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta binafsi, wizara,
idara zilizoajiri wafanyakazi ambao wako chini ya mikataba maalum,
mashirika ya umma, mtu binafsi aliyejiajiri mwenyewe, watazinduka na
kuchangamkia kujiunga na NSSF kunufaika na mafao yatolewayo.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment