Mishahara mipya hailipiki - waajiri
22nd April 2010
Wasema wafanyakazi wengi watapunguzwa
Wadai Waziri Juma Kapuya amekurupuka
Wadai Waziri Juma Kapuya amekurupuka
Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya.
Waajiri katika sekta binafsi na
wanasiasa wameilalamikia serikali kupandisha kima cha chini cha
mishahara ya sekta binafsi kwa asilimia 100 na wameonyesha wasiwasi wao
kwamba kiasi hicho kitakua vigumu kulipa.
Walitoa malalamiko hayo kufuatia tangazo la juzi la Waziri wa Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, Profesa Juma Kapuya (pichani).
Mjini Arusha, baadhi ya waajiri,
wameeleza kushtushwa na hatua ya serikali kupandisha mishahara ya
wafanyakazi wa sekta binafsi kwa asilimia 100 wakidai kuwa hatua hiyo
itawafanya wapunguze wafanyakazi kwa kuwa hawatakubali kupata hasara.
Wamesema hatua hiyo itawafanya washindwe
kumudu kulipa mishahara kwa idadi kubwa ya wafanyakazi walionao kwani
hakuna ambaye anapenda kupata hasara.
“Ongezeko hili la mishahara litaenda
sambamba na ongezeko la mchango wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF),
hali ambayo itawafanya waajiri walio wengi waingie gharama mara mbili,”
alisema Wilson Leguna kutoka kampuni ya Insignia Ltd iliyopo mtaa wa
viwanda mjini hapa.
Alisema mwajiri yeyote anataka kupata faida zaidi kwa kupunguza matumizi, hivyo, nyongeza ya mishahara itawapa wakati mgumu.
“Kuongeza mishahara ni kuongeza matumizi,
hivyo hali hiyo itawafanya waajiri wengi katika sekta ya biashara
kupandisha bei ya bidhaa zao ili kufidia matumizi katika malipo ya
mishahara,” alisema.
Hata hivyo, alisema waajiri kama hao
hawawezi kupandisha ghafla bei ya bidhaa zao hasa ikizingatiwa kwamba
wakati huu ni wa ushindani wa kibiashara. Meneja Mkuu wa kiwanda cha
magodoro, TanFoam, Riaz Somji, alisema ameshtushwa na habari ya
kupandishwa kwa mishahara ya wafanyakazi kwa asilimia 100. Hata hivyo,
Somji anayemiliki kiwanda hicho chenye wafanyakazi wapatao 120 alikataa
kutoa maoni kuhusu nyongeza, kwa maelezo kuwa anayepaswa kufanya hiyo ni
Mkurugenzi Mkuu wake, Bala Subiramania, ambaye yupo safarini.
Alisema menejimenti ya kiwanda hicho
itakaa hivi karibuni kutafakari suala hilo. Mwajiri mwingine, mwenye
asili ya Kiasia, alisema hakuwa na taarifa yoyote ya nia ya serikali
kupandisha mishahara kwa wafanyakazi wa sekta binafsi.
Jijini Tanga, baadhi ya waajiri walisema
serikali ilipaswa kutafuta mbinu mbadala ili kupata suluhu ya kutatua
matatizo ya wafanyakazi badala ya kuwakomoa waajiri wa sekta binafsi.
Baadhi ya waajiri kutoka makampuni ya
ulinzi, viwandani, hospitali binafsi na waajiri wa majumbani, wakiongea
kwa sharti la kutotaka kutajwa majina yao kwa madai yataleta
uchonganishi na watumishi wao, walisema kuwa Serikali ilipaswa
kupandisha kwanza kima cha mishahara kwa watumishi wake.
Walisema serikali ilipaswa kutafuta maoni
kwanza kutoka kwa waajiri wa sekta binafsi kabla ya kuamua kutoa
tangazo hilo kwani litaleta uchochezi na chuki baina ya watumishi wa
sekta binafsi na waajiri wao.
Jijini Dar es Salaam, Chama Cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema mshahara huo ni ‘kiini
macho’ na kwamba serikali haina dhamira ya dhati kuhusu ilichosema.
Chadema imesema kama serikali ingekuwa na
dhamira ya kweli ingeanza yenyewe kutangaza nyongeza ya mishahara kwa
watumishi wake kabla ya ile ya sekta binafsi.
Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa chama
hicho, John Mnyika, alisema jana kuwa tamko hilo la serikali ni la
kisiasa tu kujaribu kuzima mgomo kwa kuwa bado haijatangaza viwango vya
mishahara kwa watumishi wake.
Alisema Waziri Kapuya amekurupuka kutoa tamko kuzima shinikizo la kumtaka ajiuzulu, kama alivyoshauriwa na wadau mbalimbali.
Alisema serikali bado pia haijatoa notisi
kwenye gazeti la serikali kwa kuwa notisi namba 223 ya mwaka 2007
ilivurugwa, kwa hiyo hata watumishi wa sekta binafsi wasichekelee kwa
kuwa kuna dalili zote kuwa tamko hilo ni mchanga wa macho.
Naye Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi
na Mahusiano wa Chama cha Wananchi (CUF), Ashura Mustafa, alisema
serikali bado haijatatua matatizo ya wafanyakazi na badala yake
imeingiza siasa katika mgogoro huo mkubwa.
Alisema kumekuwa na utendaji mbovu katika
idara nyingi za serikali na chanzo kikubwa ni kwa serikali kutowajali
wafanyakazi wake ipasavyo.
Alisema watumishi wengi wa umma wanashindwa kuhudumia wananchi hadi watoe rushwa kutokana na uduni wa mishahara.
Alishauri kima cha chini kiwe sawa kwa sekta zote na kwamba hali hiyo inaweza kusaidia ufanisi kuonekana sehemu za kazi.
Mwenyekiti wa PPT Maendeleo, Peter
Mziray, alisema kama ni suala la kuongeza mshahara serikali ndiyo
inayopaswa kuanza na sekta binafsi inafuata.
Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Samweli
Ruhuza, alionyesha wasiwasi kwamba watumishi wa umma watabaki kwenye
hali ngumu na hivyo wanaweza kupungua kwa asilimia kubwa kwa kutimkia
sekta binafsi.
Ruhuzu alisema sekta binafsi inajiendesha
kulingana na uwekezaji, hivyo mwajiri wake atakapofanya vizuri katika
kuzalisha kipato ndipo hupatiwa mshahara mzuri.
Alisema kuwa serikali inatakiwa kuangalia
suala hilo kwa kina zaidi kwani mtumishi wa umma hulipwa kulingana na
cheo chake tofauti na sekta binafsi.
Alisema kuwa suala hilo litasababisha
wataalamu wa utumishi wa umma kuondoka serikalini na kuelekea sekta
binafsi kwa ajili ya kufuata maslahi.
Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party
(TLP), Augustine Mrema, alisema suala la serikali kutangaza ongezeko la
mshahara katika sekta binafsi bado limekuwa ni kitendawili kutokana na
kwamba jambo hilo halijatolewa ufafanuzi wa kutosha.
Mrema alisema alipokuwa akitizama taarifa
ya habari kuhusiana na tangazo la serikali, alishangaa kumuona Profesa
Kapuya akisita kutaja kiasi cha fedha kilichoongezeka.
Alisema Kapuya alitakiwa kutoa ufafanuzi wa kina kwa mfano, kueleza mtumishi wa ndani atalipwa kiasi gani na kadhalika.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha
Waajiri Tanzania (ATE), Dk. Agrey Mlinuka, alisema chama chake kitatoa
tamko kuhusu ongezeko hilo ambalo limetangazwa na serikali kitakapopata
taarifa rasmi ya serikali.
Imeandikwa na John Ngunge, Arusha, Lulu George, Tanga, Joseph Mwendapole na Beatrice Shayo, Dar.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment