Pages

Tuesday, May 29, 2012

Upinzani wahoji mabilioni ya NSSF yaliyokopeshwa Kiwira

17th July 2009
  Yasema inawekeza pasipo na tija

Kambi ya Upinzani bungeni, imehoji mkopo uliotolewa na Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) wa Sh. Bilioni 8.4 kwa Kampuni ya Makaa ya Mawe na Nguvu ya Umeme – Kiwira utarudishwa lini, huku wanachama wanaostahili kulipwa mafao yao wakisaga soli za viatu kufuatilia.
Hoja hiyo ilitolewa na Msemaji wa Kambi hiyo, Salim Abdallah Khalfani, kwa Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana, wakati akichangia maoni ya Makadirio ya Matumizi katika wizara hiyo.
Alisema kambi hiyo ina wasiwasi wa kutokuwepo ushahidi wowote wa dhamana iliyowekwa iwapo mkopaji atashindwa kurejesha.
Ameir alisema mkopo huo ulitarajiwa kulipwa baada ya miezi sita lakini hadi Machi 26, mwaka huu, ulikuwa haujalipwa.
“Isitoshe, Mkataba huo katika kifungu 10.5 unasema kuwa mkopo huo umedhaminiwa na serikali kwa asilimia 100 pamoja na Benki ya CRDB. Hii inashangaza kwani fedha zenyewe ni za wafanyakazi wa Tanzania, na serirkali yao inadhamini kwa asilimia 100,” alisema.
Ameir alisema Kambi hiyo inaitaka serikali kuhakikisha inachukua hatua za haraka za kiutawala ili kuhakikisha shirika hilo linaendeshwa kama sheria inavyotaka.
Alisema mbali na matatizo hayo ya udhibiti wa fedha za wanachama pia NSSF imetamkwa kuwa ni miongoni mwa taasisi zenye utunzaji mbovu wa kumbukumbu za wafanyakazi ambapo mikataba ya ajira, nakala za vyeti, barua za ajira, taarifa za kupandishwa vyeo, uhamisho na ongezeko la mishahara wakati wa ukaguzi havikuwepo.
Aidha, alisema shirika hilo halizingatii sheria ya ajira ambapo wakati wa ukaguzi iligundulika kuwepo kwa uvunjwaji wa sheria za ajira kwa kutoa ajira bila kufuata taratibu zilizowekwa.
Katika hatua nnyingine, Kambi hiyo ilisema taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali katika ukaguzi wake kwenye Shirika hilo iligundua matumizi ya hovyo hovyo ya fedha za wanachama.
Alisema NSSF ilikopesha jumla ya Sh. 1,525,368,525 kwa kampuni ya M/S Medtech toka Aprili 2003 na mkopo ulitakiwa kurejeshwe Desemba 2004, hadi sasa pesa za wanachama hazijarudishwa.
“Kwa ujumla ripoti imebaini kuwa NSSF imekuwa inawekeza sehemu zisizo na tija kwa wanachama,” alisema.
Aliongeza kuwa taarifa hiyo inasema kuwa NSSF ni miongoni mwa taasisi zenye masurufu yanayofikia jumla ya Sh. 22,231,219 ambayo hayajarejeshwa na kwamba imenunua hisa au kuwekeza katika mashirika kadhaa lakini hakuna gawio inayopata.
Alisema fedha zilizowekezwa na NSSF kwenye mabano ni Tanzania Oxygen Ltd (sh. 13,200,000), Tanzania Housing Bank (sh. 495,280,000) na kwamba 1st Adili Bank Corp Litd ilipewa mkopo wenye utata wa sh 3,152,024,742.
Kampuni zingine ambazo NSSF imewekeza bila kupata gawio kwa kipindi chote ni CDC Mbeya Cement (sh. 1,152,024,742), Ubungo Plaza (sh. 9,817,038,702), TANR Share (sh.1,000,000,000), HEPZ Quality Group Share (sh. 47,156,025,113) na PPL pension Properties (sh. 3,500,00). Jumla ya uwekezaji usio na tija ni sh. 62,789,093,299.
Alisema mifano hiyo ni michache inayoashiria udhaifu mkubwa katika upangaji wa miradi na uwekezaji wa NSSF na kwamba inapaswa suala hilo kuchukuliwa kwa uzito maalumu ili kunusuru fedha za wanachama.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment