JK atoa changamoto kwa Mamlaka ya Hifadhi ya Jamii
24th March 2011
B-pepe
Chapa
Maoni
Rais Jakaya Kikwete
Rais
Jakaya Kikwete, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Hifadhi ya
Jamii nchini (SSRA), kuyaangalia kwa makini malalamiko ya wafanyakazi
kuhusu tofauti kubwa ya utoaji wa mafao ya mkupuo na pensheni ya uzeeni,
iliyopo kati ya mfuko mmoja wa hifadhi ya jamii na mwingine.
Mifuko
hiyo, ni pamoja na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko
wa Pensheni kwa Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF), Mfuko wa Pensheni
ya Wafanyakazi wa Serikali Kuu (GEPF), Mfuko wa Pensheni kwa
Wafanyakazi wa Umma (PSPF), Mfuko wa Pensheni nchini (PPF) na Mfuko wa
Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Rais
Kikwete alitoa kauli hiyo jana jijini Dar es Salaam, wakati akizindua
Bodi ya Wakurugenzi ya SSRA pamoja na nembo ya mamlaka hiyo,
inayosimamia mifuko hiyo.
Alisema
kutokana na tofauti hizo, wafanyakazi wenye viwango sawa vya mishahara
na muda sawa wa utumishi wanapostaafu, mmoja anapata mafao hadi mara
tatu zaidi ya mwenzake aliye mfuko mwingine, na kusema: “Hili ni jambo
la kuliangalia kwa makini sana.”
Hata
hivyo, aliipongeza SSRA kwa uamuzi wake wa kuajiri Mshauri Mwelekezi
anayeshughulikia suala hilo ili kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuwapo
kwa uwiano mzuri wa mafao kati ya mfuko na mfuko, na kushauri uamuzi
utakaofikiwa, uzingatie afya ya mifuko na pia tathmini ihakikishe
serikali inapunguziwa mzigo.
Pia
aliitaka SSRA kuangalia malalamiko ya wastaafu kwamba, mafao ya
pensheni hayazingatii mfumuko wa bei, viwango vya riba katika masoko na
ukuaji wa uchumi, hali ambayo alisema inasababisha wengi wao kupata
pensheni isiyokidhi maisha yao ya kawaida.
Alisema
uanzishwaji wa mfuko wa pensheni ya wazee, ni jambo lisiloepukika hivi
sasa nchini kwani inasikitisha kusikia kuwa ni asilimia nne tu ya wazee
ndiyo wanaopata pensheni.
Aliitaka
SSRA kwa kushirikiana na wadau, kuandaa mkakati wa kutekeleza jambo
hilo akisema kuanzisha pensheni ya wazee, serikali itafanikiwa kupunguza
kiwango cha umaskini kwa zaidi ya asilimia 10.
Naye
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa SSRA, Siraju Kaboyonga, alisema
wafanyakazi wengi nchini, bado hawajatambua ipasavyo umuhimu wa hifadhi
ya jamii, hali ambayo alisema inachangia kuwakatisha tamaa baadhi ya
wanachama watarajiwa kuhiari kujiunga katika mifuko hiyo.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment