Pages

Tuesday, May 29, 2012

Majambazi yavamia nyumba ya Mkurugenzi Mkuu NSSF

18th April 2010
  Kiasi kikubwa cha fedha chaibwa
Dk. Ramadhan Dau

Watu wanaosadikiwa kuwa majambazi, jana walivamia nyumba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk. Ramadhan Dau na kuiba kiasi kikubwa cha fedha.
Tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia jana maeneo ya Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo watu hao walibomoa ukuta unaozunguka nyumba hiyo na kuingia ndani.
Akizungumza na Nipashe Jumapili, Kamanda wa Polisi wa Kinondoni, Elias Kalinga alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema hata hivyo, watu hao hawakumjeruhi mtu na hawakuchukua kitu chochote zaidi ya fedha ambazo zilikuwa zimehifadhiwa kwenye masanduku maalum ya kuhifadhia fedha.
"Ni kweli tukio hilo limetokea majira ya saa 9 (juzi) usiku ambapo majambazi hao ambao bado hatujajua idadi yao, waliingia ndani baada ya kubomoa ukuta wa nyumba hiyo," alisema Kalinga.
Aidha, Kamanda huyo wa Polisi alisema baada ya kuingia ndani waliwakamata walinzi wawili wa nyumba hiyo waliokuwa na silaha aina ya shotgun na kuwafunga kamba kabla ya kuingia chumbani na kuiba fedha hizo ambazo kiasi bado hakijajulikana.
Alisema baada ya kuwafunga kamba walinzi hao waliingia chumbani kwa mwenye nyumba (Dk. Dau) na kubomoa sanduku la kuifadhia fedha na kuondoka na fedha hizo.
Alisema wakati tukio hilo linatokea, Dk. Dau hakuwepo nyumbani hapo pamoja na familia yake na walibaki walinzi hao.
Aidha, Kamanda Kalinga alisema kutokana na mazingira ya tukio hilo kuwa ya kutatanisha, Jeshi la Polisi linawashikilia walinzi wa nyumba hiyo, Deus Mtatilo (52) pamoja na Yusuph Bakari (59) waliokuwepo siku ya tukio hilo.
Alisema mazingira ya tukio hilo yanonyesha kuwa na ulakini kutokana na ukweli kuwa walinzi hao walikuwa na silaha za moto ambazo hawakuzitumia wakati wa tukio na pia hakukuwepo kwa milio yoyote ya risasi. Alisema Polisi wanaendelea na uchunguzi.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment