Wastaafu Elimu Kibaha wagomea mafao ya PPF
3rd June 2010
Rais Jakaya Kikwete
Wafanyakazi waliostaafu wa Shirika la
Elimu Kibaha, mkoani Pwani, wamegoma kupokea mafao yao kutoka Mfuko wa
Pensheni ya Mashirika ya Umma (PPF), kwa madai kwamba fedha zilizotolewa
na mfuko huo ni kidogo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana,
Mwenyekiti wa wastaafu hao, Ally Gombati, alisema wafanyakazi walioamua
kugomea mafao hayo ni wale waliostaafu kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka
huu.
Alisema wameyakataa mafao hayo kupinga
mfumo unaotumiwa na PPF ya kuwalipa wafanyakazi waliostaafu malipo
kidogo tofauti na mifuko mingine ambayo inalipa wanachama wake kiwango
ambacho kinamfanya mstaafu kuishi kwa muda mrefu.
"Tumeamua kueleza bayana kuwa hatuwezi
kuchukua pesa za mafao hadi hapo PPF watakapofanya marekebisho na kulipa
kama ilivyo mifuko mingine," alisema Gombati.
Alisema katika shirika hilo, kuna
wafanyakazi wengi waliostaafu lakini baadhi ya wengine waliokuwa
wanachama wa mifuko mingine ya jamii ukiwemo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi
ya (NSSF) ambao walilipwa kiasi kikubwa cha fedha hadi kufikia Sh.
milioni 25 lakini wao waliambulia Shilingi milioni tano tu.
"Kitu hiki hakiwezekani kwani hawa
wafanyakazi wenzetu tulikuwa na cheo kimoja lakini wamepewa mafao
yanayowawezesha kuanza maisha mapya bila kutetereka, iweje sisi
tuliojiunga na mfuko huo tuondoke masikini wa kutupwa," alihoji
Mwenyekiti huyo.
Pamoja na hayo, Gombati alisema baada ya
kuchukua hatua hiyo, walikwenda makao makuu ya mfuko huo kueleza msimamo
huo lakini hawakupata ufumbuzi.
Aidha, wastaafu hao, wamemuomba Rais
Jakaya Kikwete kuingilia kati mgogoro kati yao na mfuko huo ili hata
watu wanaotarajia kustaafu kwa kipindi hiki waweze kulipwa mafao
kulingana na muda waliolitumikia taifa.
Hata hivyo, juhudi za kumpata msemaji wa mfuko huo hazikuzaa matunda jana.
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment