Saturday, May 4, 2019

TANZANIA YASHIKA NAFASI YA NNE KWA WATU WANAOAMINI UMILIKI WA ARDHI NA MAKAZI UKO SALAMA



 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akionesha Ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Msingi kuhusu Haki na Usalama wa Umiliki wa Rasilimali Ardhi na Makazi Tanzania baada ya kuizindua jijini Dodoma leo tarehe 3 Mei 2019. Kushoto ni Mwakilishi wa kutoka Taasisi ya Prindex David Ameyaw na wa pili kulia ni Mtakwimu Mkuu Serikali Dkt Albina Chuwa.
 Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizindua Ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Msingi kuhusu Haki na Usalama wa Umiliki wa Rasilimali Ardhi na Makazi Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 3 Mei 2019. Kushoto ni Mwakilishi wa kutoka Taasisi ya Prindex David Ameyaw na wa pili kulia ni Mtakwimu Mkuu Serikali Dkt Albina Chuwa.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wawakilishi wa taasisi wakati wa uzindua Ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Msingi kuhusu Haki na Usalama wa Umiliki wa Rasilimali Ardhi na Makazi Tanzania jijini Dodoma leo tarehe 3 Mei 2019. Wa pili kushoto waliokaa ni Mwakilishi wa kutoka Taasisi ya Prindex David Ameyaw na wa pili kulia waliokaa ni Mtakwimu Mkuu Serikali Dkt Albina Chuwa.(PICHA NA WIZARA YA ARDHI)
Na Munir Shemweta, DODOMA
Tanzania imeshika nafasi ya nne kati ya nchi tisa za Kusini na... Mashariki mwa Afrika zilizofanyiwa utafiti kwa kuwa na asilimia 64 ya watu wanaoamini kuwa hali ya umiliki wa ardhi na makazi ni salama.
Hayo yalibainika leo tarehe 3 Mei 2019 wakati wa uzinduzi wa Ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Msingi kuhusu Haki na Usalama wa Umiliki wa Rasilimali Ardhi na Makazi Tanzania uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, uzinduzi ulifanyika jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa kuzindua Ripoti hiyo, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisema kiwango hicho ni kikubwa zaidi ya wastani wa asilimia 61 kwa nchi tisa zilizofanyiwa utafiti katika Afrika ya Magharibi.
Aidha, Utafiti wa Ripoti hiyo unaonesha Tanzania imeshika nafasi ya kumi kati ya nchi 33 zilizoshiriki katika Utafiti huo kwa kuwa na asilimia zaidi ya hamsini ya watu wanaomiliki makazi yao wenyewe.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alisema, matokeo ya utafiti huo yametokana na hatua mbalimbali ambazo serikali imeendelea kuzichukua ili kuhakikisha wananchi wake wanakuwa na usalama wa umiliki wa ardhi na makazi.
Kawa mujibu wa Dkt Mabula, kama ungefanyika utafiti  mwingine leo basi huenda matokeo yake  yangekuwa tofauti kutokana na Serikali kudhamiria kupanga , kupima na kumilikisha kila kipande cha ardhi na kutolea mfano  katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali ilipanga kupima na kumilikisha vipande vya ardhi.
Dkt Mabula alibainisha kuwa, takwimu zinaonesha kati ya mwezi Agosti 2018 na Machi 2019 Hatimiliki 36,428 zimeandaliwa kwa wamiliki wa viwanja na mashamba na Hatimili za kimila 286472 ziliandaliwa kwa ajili ya wamiliki wa ardhi walioko vijijini.
Dkt Mabula alisema, hatua nyingine ambazo serikali imechukua ni pamoja na kuanza kutumia  mifumo ya kielektroniki katika utoaji huduma za ardhi  ambapo Mfumo Unganishi wa Kumbukumbu za Sekta ya Ardhi (ILMIS) umeendelea kufanyiwa majaribio katika wilaya za Ubungo na Kinondoni na kusisistizia kuwa mfumo huo utasaidia kuongeza kasi ya umilikishaji ardhi na kupunguza gharama kwa kiasi kikubwa..
Kwa upande wake Mtakwimu Mkuu wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt Albina Chuwa alisema utafiti uliofanyika ulishirikisha sekta zote muhimu na kuzitaja baadhi yake kuwa ni pamoja na Wizara ya Ardhi, Global Land Allience, DFID sambamba na wananchi wote wakiwemo wakuu wa kaya za Tanzania Bara na Zanzibar.
Alisema, Tanzania ni nchi ya kwanza kutoa ripoti yake mwenyewe kati ya nchi 33 na ripoti hiyo itatumiwa na Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi katika kupanga mipango yake na kuzitaka taasisi za vyuo kutumia ripoti hiyo kufanyia utafiti ili kuisaidia sekta ya Ardhi.

No comments :

Post a Comment