WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema Serikali imedhamiria kuwalinda watoto wa kike na ndiyo maana
inasisitiza waachwe wasome hadi wamalize kidato cha sita.
Alitoa kauli hiyo kwa nyakati
tofauti wakati akizungumza na wananchi wa vijiji mbalimbali vya wilaya
ya Ruangwa, mkoani Lindi ambako anapita kuwasalimia wananchi wa jimbo
lake na kuhimiza kazi za maendeleo. Waziri Mkuu yuko Ruangwa kwa siku
nne kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.
“Tumesema mtoto wa kike aachwe
asome hadi kidato cha sita, akifika chuo kikuu atakuwa na uwezo wa
kufanya maamuzi yake lakini kwa sasa waacheni watoto wa kike wasome.
Ninyi vijana, mkibainika mmewapa mimba mabinti wanaosoma, adhabu yake ni
miaka 30 jela,” alisema.
Alisema nia ya Serikali ni kupata
watumishi ambao ni wataalamu wa kada tofauti kama madaktari, wanasheria,
mafundi, walimu na hata Wakuu wa Wilaya ambao ni wanawake.
Aliwaonya wazazi ambao huwa
wanakubali kuongea pembeni (kupewa fedha) na wanaume waliowapa mimba
mabinti zao na kuwaeleza kuwa, kwa mujibu wa sheria ilivyo, nao pia
wanastahili kupewa adhabu ya kifungo jela.
“Mzazi ukigundua binti yako ana
ujauzito toa taarifa haraka ili mhusika akamatwe mara moja. Usikubali
kuongelea jambo hili pembeni, nawe pia utawekwa ndani pamoja na huyo
mhusika ambaye tayari ni mhalifu,” alisema na kuongeza:
“Mwanao akisema anataka kuoa,
mzazi inabidi upeleleze kwanza anataka kumuoa nani. Asije kuwa anamuona
binti ambaye bado anasoma. Akisema anaoa na wewe ukamkubalia tu, ikija
kubainika kuwa ni mwanafunzi, wewe na mkeo mnakwenda jela miaka mitano
mara sita,” alisema huku akionyesha ishara ya kukunja ngumi.
Akiwa kwenye baadhi ya vijiji,
Waziri Mkuu alielezwa kwamba kuna shule ambazo zina walimu wa kiume
watupu na akamtaka Afisa elimu asimamie suala hilo kwa kuwahamisha
baadhi ya walimu kutoka Ruangwa mjini na kuwapeleka shuke za vijijini.
“Kuna shule pale Ruangwa mjini
zina walimu wamerundika lakini hapa naambiwa hakuna Mwalimu wa kike hata
mmoja. Hili tatizo kwa wanafunzi wa kike. Wana masuala ambayo hawawezi
kuongea na walimu wa kiume, ni lazime awepo Mwalimu wa kike wa
kusikiliza shida zao,” alisema na kumsisitiza afisa elimu afuatilie
tatizo hilo kwenye shule zote.
Mapema, akitoa taarifa ya mkoa
mbele ya Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi alisema
mkoa huo unakabiliwa na tatizo la utoro mashuleni kwani wanaoandikishwa
darasa la kwanza si wote wanaomaliza darasa la saba na vivyo kwa
wanaoanza kidato cha kwanza na kumaliza kidato cha nne.
“Takwimu zinaonesha mkoa wa Lindi
unalo tatizo kubwa sana na ambalo tunaendelea kulipa uzito wa pekee la
kudhibiti wanafunzi wanaoandikishwa kuanza shule lakini wanashindwa
kukamilisha kipindi chao cha miaka saba shuleni. Idadi kubwa ya
wanafunzi ni watoro,” alisema.
Takwimu za kidato cha nne
zinaonyesha kuwa idadi ya watahiniwa wa shule walikuwa 4,764 (wavulana
2411 na wasichana 2,353) na watahiniwa wa kujitegemea walisajiliwa 335
na kati yao watahiniwa 290 (asilimia 86.6) walifanya mtihani na
watahiniwa 45 ambao ni sawa na asilimia 13.4 hawakufanya mtihani.
Kwa upande wa masomo ya sayansi,
shule zilizofanya mitihani ya sayansi ya vitendo (actual practical)
zilikuwa ni 78 (Kilwa 19, Liwale 11, Lindi Manispaa 9, Ruangwa 4, Lindi
vijijini 14 na Nachingwea 21) watahiniwa ambao hawakufanya mtihani baada
ya kusajiliwa ni 100 (wavulana 50 wasichana 50).
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, DESEMBA 29, 2016.
No comments :
Post a Comment