Wananchi wa kijiji cha Muhuru
wilayani Ruangwa wakifanya kila linalowezekana ili wamwone Mbunge wao,
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kijijini hapo
Desemba 28, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
……………………….
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka wakazi wa Ruangwa na mkoa mzima wa Lindi wachangamkie fursa ya
kulima mihogo na alizeti kwa sababu mazao hayo yana uhakika wa soko.
Alitoa wito huo wakati akizungumza
na wananchi wa vijiji mbalimbali vya wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi
ambako anapita kuwasalimia wananchi wa jimbo lake na kuhimiza kazi za
maendeleo. Waziri Mkuu yuko Ruangwa kwa siku nne kwa mapumziko ya mwisho
wa mwaka.
“Nimekuja na fedha, wangapi
wanataka kupata fedha?” alihoji Waziri Mkuu katika mikutano yake na
kuitikiwa “Sisi” na umati wa watu walionyoosha mikono juu kuonesha kuwa
wako tayari kupokea fedha hizo. Mikutano hiyo ilifanyika kwenye vijiji
vya Namilema, Mbuyuni, Nandandara, Namkonjera, Muhuru, Chikundi, Chibula
na Matumbu.
“Mnataka fedha siyo? Fedha iko
shambani! Nimewaletea fursa ya mwekezaji anayetaka kununua mihogo yote
katika mkoa huu,” alisema Waziri Mkuu na kusababisha kicheko kwa watu
waliokuwa wakinyoosha mikono yao.
“Limeni mtu mmoja mmoja au
jiungeni kwenye vikundi ili mpate ekari tatu hadi nne kwa sababu mna
uhakika wa soko. Mwekezaji huyu anataka kununua mihogo yote na ya wilaya
hii peke yake haitoshi kiasi ambacho anataka. Kwa hiyo tumekubaliana na
wabunge wenzangu kwamba kiwanda hiki kitajengwa Nanjilinji ambako ni
katikati ya mkoa ili iwe rahisi kusomba na kupeleka mazao hayo,”
alisema.
Waziri Mkuu alisema eneo la
Nanjilinji lililoko wilayani Kilwa, linafikiwa kwa urahisi na wakazi
wote kutoka Kilwa, Nachingwea, Ruangwa, Lindi Vijijini na Liwale.
Akifafanua zaidi, alisema
mwekezaji aliyepatikana (bado ni mapema kumtaja) yuko tayari kufuata
mazao waliko wakulima na atakuwa akiwalipa hukohuko. “Yeye anachotaka ni
mihogo ya kutosha, ndiyo maana nawasisitizia muanze kulima zao hili kwa
wingi cha msingi mfuate kanuni bora za kilimo,” aliongeza.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu
amewataka wakazi hao walime zao la alizeti kwa wingi kwa sababu
amekwishapatikana mwekezaji wa kununua zao hilo na kwa bei nzuri.
“Nilipokwenda Singida nilikutana
na mmiliki mmoja wa kiwanda cha kusindika mafuta ya alizeti akasema
anahitaji kununua zao hilo kwa wingi kwa sababu inayozalishwa kule
haitoshi. Ameshakuja hapa na kuangalia ardhi ya hapa amesema inafaa kwa
zao hilo,” alisema.
“Yeye atawaletea mbegu na kila
ekari moja inahitaji kilo tano. Ukivuna kila ekari unapata magunia 20 na
kila gunia lina uwezo wa kutoa lita 20. Bei ya dumu mojala lita 20 ni
sh. 60,000 kwa hiyo katika ekari yako moja una uhakika wa kupata sh.
milioni 1.2. Hata ukitoa gharama ya kulima na palizi, bado huwezi kukosa
walau sh. milioni moja kwa kila ekari.”
Alimwagiza Mkuu wa Idara ya Kilimo
(Umwagiliaji na Ushirika) wa wilaya hiyo, Bi. Violeth Byanjweli afanye
kazi ya kuratibu ni wakazi wangapi wana mashamba ya alizeti na wangapi
wako tayari kuanzisha kilimo hicho ili mbegu zitakapoletwa iwe ni rahisi
kuwasambazia huko waliko.
“Hiki kilimo ni cha miezi mitatu
tu na palizi yake ni mara moja tu. Kwa hiyo mvua za Januari zikianza,
changamkieni hiyo fursa na baada ya miezi mitatu kila mtu atakuwa na
hela yake badala ya kusubiria korosho ambazo mnavuna mara moja kwa
mwaka,” alisisitiza.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, DESEMBA 29, 2016.
No comments :
Post a Comment