Katika gazeti la Mwananchi toleo la
Desemba 16 mwaka huu, ukurasa wa 11, kulichapishwa barua ya Afisa Mifugo
mstaafu wilayani Mpwapwa, Dododma, Bw. Edward Chedego Uledi. Katika
barua yake iliyosomeka “Rais Magufuli nisaidie nilipwe stahiki zangu,”
mstaafu huyo alilalamikia kupunjwa mafao yake.
Mtumishi huyo aliyestaafu tangu 2008,
alilalamikia kitendo cha maafisa utumishi kuchelewa kurekebisha
taarifa zake kwa kuzingatia cheo chake cha mwisho na hivyo kusababisha
apunjwe mafao na akalipwa kwa mujibu wa cheo cha zamani.
Serikali imefuatilia kwa kina na kuona
kuna ukweli katika sehemu ya madai ya mstaafu huyo. Tunapenda kuutaarifu
umma kuwa malalamiko ya mwananchi huyo sasa yameshughulikiwa haraka na
Bw. Uledi amejulishwa na kuridhika na hatua zilizochukuliwa. Akiishukuru
Serikali kwa hatua hizo alisema:
“Nimeeleweshwa vizuri, nimeelewa na
naishukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kasi hii. Namshukuru sana
Rais na nawapongeza watendaji wote waliojitoa kufuatilia na kutatua
malalamiko ya mimi mwananchi wa kawaida.”
Serikali inatumia nafasi hii kuvipongeza
vyombo vya habari nchini vinavyojitoa na kujikita katika kusaidia
kutatua changamoto za kweli za wananchi. Aidha tunawakumbusha watendaji
wa Serikali kuendelea kufanyakazi kwa bidii, ubunifu, kasi na kujituma
katika kufuatilia na kutatua kero mbalimbali za wananchi.
Imetolewa na:
Dkt. Hassan Abbasi,
Mkurugenzi Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali.
No comments :
Post a Comment