Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa
Rais Prof. Faustin Kamuzora (kulia) akimsikiliza Diwani wa Kata ya
Buguruni Mhe. Adam Fugame (Kushoto) wakati wa ziara ya kikazi ya
kukagua ujenzi wa mfereji wa maji taka katika eneo la Ilala Bungoni,
Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi
wa Manispaa ya Ilala Bw. Palela Msongela (kushoto) akiongea na Katibu
Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Prof. Faustin Kamuzora mara baada ya
kukagua ujenzi unaoendelea katika mfereji wa kupitisha maji taka eneo la
Ilala Bungoni
Gervas wa Kampuni ya Dezo Civil
Contractors Co. Ltd akifanunua jambo kwa Prof Kamuzora, Katibu Mkuu
Ofisi ya Makamu wa Rais, katika eneo la Temeke ambapo Kampuni hiyo
imepewa kazi ya kusafisha na kujenga mfumo wa maji taka. Katikati ni Bw.
Motongori Chacha, Afisa Mazingira Manispaa ya Temeke.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa
Rais Prof. Faustin Kamuzora (kushoto) akimsikiliza Bi. Ukende Mkumbo
kutoka Taasisi ya Mwalimu Nyerere Kigamboni akifafanua hatua za ujenzi
wa ukuta katika eneo lao. Katikati ni mwakilishi kutoka Kampuni ya Dezo
Civil Contractors Co. Lt
Sehemu ya Ukuta wa Obama/Ocean Road ukarabati ukiendelea
…………
Na Lulu Mussa
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa
Rais Prof. Faustin Kamuzora ameuagiza ungozi wa Dezo Civil Constractors
Co. Ltd kuhakikisha ujenzi wa Miundombinu ya maji taka katika Manispaa
za Ilala na Temeke unakamilika kwa muda uliopangwa na kwa ubora wa hali
ya juu kwa kuzingatia makubaliano yaliyopo katika mkataba.
Akikagua ujenzi unaoendelea wa
miundombinu hiyo, katika Wilaya ya Ilala eneo la Bungoni, Prof. Kamuzora
amemtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala Bw. Palela Msongera
kuhakikisha changamoto zinazojitokeza katika ujenzi huo zinatatuliwa
mara moja ikiwa ni pamoja na utupaji wa taka maji na taka ngumu katika
mfereji huo unaojengwa.
Awali Mkurugenzi wa Manispaa ya
Ilala Bw. Palela Msongela alimueleza Katibu Mkuu kuhusu changamoto
zinazohusu mazingira hususan uhaba wa miundombinu ya mifumo ya maji taka
na ujenzi wa makazi holela unaosababisha udhibiti hafifu wa taka.
Aidha, Prof. Kamuzora amewataka
watendaji wa Manispaa ya Ilala kuwaelimisha wananchi juu ya athari
zinazoweza kujitokeza kwa kutiririsha maji machafu kuwa ni pamoja na
milipuko ya magonjwa hususan kipindupindu na kuhatarisha afya za wakazi
hao.
Kwa upande wake Diwani wa Kata ya
Buguruni Bw. Adam Fugame amemhakikishia Prof Kamuzora kuwa ataongea na
wananchi katika Kata yake na kusisitiza matumizi sahihi ya sheria
ndogondogo za mitaa walizojiwekea ikiwa ni pamoja na kuwatoza faini
wananchi wanaokiuka taratibu hizo.
“Nikuhakikishie, kwa kupitia
mikutano na vikao na wananchi katika Kata yangu, tutazidi kusisitiza juu
ya jambo hili na kuweka sheria kali zaidi kwa watakao kaidi”.
Alisisitiza Mhe. Diwani Fugame
Ujenzi huo wa Ukuta wa
(Obama/Ocean Road na Kigamboni) na Miundombinu ya maji taka katika
Manispaa za Ilala na Temeke unatekelezwa chini ya Ofisi ya Makamu wa
Rais chini ya Mradi wa Kuhimili Mabadiliko ya Tabianchi. Mradi huu
unafadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira (UNEP).
Kampuni ya Dezo Civil Contractors ndio inafanya ujenzi huu na
unatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni na kazi zinatarajiwa kukamilika
mwezi Julai 2017.
(Picha na Habari na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini – Ofisi ya Makamu wa Rais.)
No comments :
Post a Comment