Pages

Thursday, December 29, 2016

SERIKALI IMEPANIA KUMLINDA MTOTO WA KIKE – MAJALIWA


weqq
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kuwalinda watoto wa kike na ndiyo maana inasisitiza waachwe wasome hadi wamalize kidato cha sita.
Alitoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wananchi wa vijiji mbalimbali vya wilaya ya Ruangwa, mkoani Lindi ambako anapita kuwasalimia wananchi wa jimbo lake na kuhimiza kazi za maendeleo. Waziri Mkuu yuko Ruangwa kwa siku nne kwa mapumziko ya mwisho wa mwaka.

“Tumesema mtoto wa kike aachwe asome hadi kidato cha sita, akifika chuo kikuu atakuwa na uwezo wa kufanya maamuzi yake lakini kwa sasa waacheni watoto wa kike wasome. Ninyi vijana, mkibainika mmewapa mimba mabinti wanaosoma, adhabu yake ni miaka 30 jela,” alisema.
Alisema nia ya Serikali ni kupata watumishi ambao ni wataalamu wa kada tofauti kama madaktari, wanasheria, mafundi, walimu na hata Wakuu wa Wilaya ambao ni wanawake.
Aliwaonya wazazi ambao huwa wanakubali kuongea pembeni (kupewa fedha) na wanaume waliowapa mimba mabinti zao na kuwaeleza kuwa, kwa mujibu wa sheria ilivyo, nao pia wanastahili kupewa adhabu ya kifungo jela.
“Mzazi ukigundua binti yako ana ujauzito toa taarifa haraka ili mhusika akamatwe mara moja. Usikubali kuongelea jambo hili pembeni, nawe pia utawekwa ndani pamoja na huyo mhusika ambaye tayari ni mhalifu,” alisema na kuongeza:
“Mwanao akisema anataka kuoa, mzazi inabidi upeleleze kwanza anataka kumuoa nani. Asije kuwa anamuona binti ambaye bado anasoma. Akisema anaoa na wewe ukamkubalia tu, ikija kubainika kuwa ni mwanafunzi, wewe na mkeo mnakwenda jela miaka mitano mara sita,” alisema huku akionyesha ishara ya kukunja ngumi.
Akiwa kwenye baadhi ya vijiji, Waziri Mkuu alielezwa kwamba kuna shule ambazo zina walimu wa kiume watupu na akamtaka Afisa elimu asimamie suala hilo kwa kuwahamisha baadhi ya walimu kutoka Ruangwa mjini na kuwapeleka shuke za vijijini.
“Kuna shule pale Ruangwa mjini zina walimu wamerundika lakini hapa naambiwa hakuna Mwalimu wa kike hata mmoja. Hili tatizo kwa wanafunzi wa kike. Wana masuala ambayo hawawezi kuongea na walimu wa kiume, ni lazime awepo Mwalimu wa kike wa kusikiliza shida zao,” alisema na kumsisitiza afisa elimu afuatilie tatizo hilo kwenye shule zote.
Mapema, akitoa taarifa ya mkoa mbele ya Waziri Mkuu, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bw. Godfrey Zambi alisema mkoa huo unakabiliwa na tatizo la utoro mashuleni kwani wanaoandikishwa darasa la kwanza si wote wanaomaliza darasa la saba na vivyo kwa wanaoanza kidato cha kwanza na kumaliza kidato cha nne.
“Takwimu zinaonesha mkoa wa Lindi unalo tatizo kubwa sana na ambalo tunaendelea kulipa uzito wa pekee la kudhibiti wanafunzi wanaoandikishwa kuanza shule lakini wanashindwa kukamilisha kipindi chao cha miaka saba shuleni. Idadi kubwa ya wanafunzi ni watoro,” alisema.
Takwimu za kidato cha nne zinaonyesha kuwa idadi ya watahiniwa wa shule walikuwa 4,764 (wavulana 2411 na wasichana 2,353) na watahiniwa wa kujitegemea walisajiliwa 335 na kati yao watahiniwa 290 (asilimia 86.6) walifanya mtihani na watahiniwa 45 ambao ni sawa na asilimia 13.4 hawakufanya mtihani.
Kwa upande wa masomo ya sayansi, shule zilizofanya mitihani ya sayansi ya vitendo (actual practical) zilikuwa ni 78 (Kilwa 19, Liwale 11, Lindi Manispaa 9, Ruangwa 4, Lindi vijijini 14 na Nachingwea 21) watahiniwa ambao hawakufanya mtihani baada ya kusajiliwa ni 100 (wavulana 50 wasichana 50).
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, DESEMBA 29, 2016.

No comments:

Post a Comment