Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Hakika hakuna ubishi kuwa
Serikali ya Awamu ya Tano inawajali wanyonge na imekukusudia kuwapa
unafuu katika kufanikisha mambo mbalimbali ambayo yalikuwa magumu
kuwezekana katika kipindi cha nyuma kwa ajili ya kuharikisha maendeleo.
Hatua hii inatokana na kuwakingia
kifua wananchi wenye vipato vya chini kulikoonyeshwa na Waziri wa
Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo na kuungwa mkono na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli la kupinga
upandishwaji wa bei ya huduma za umeme.
Naamini kuwa umeme ni huduma
muhimu sana katika kuharakisha maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja na
Taifa kwa ujumla kupitia sekta mbalimbali kama vile viwanda na huduma
nyingine za kiafya na kijamii.
Kitendo kilichokuwa kimetangazwa
cha kutaka kupandisha umeme kingeweza kurudisha nyuma wananchi na sekta
nyingine kama vile ujenzi wa viwanda.
Mnamo Oktoba 4 mwaka 2016,
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lilipeleka ombi katika Mamlaka ya
Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) la kuidhinishiwa ongezeko
la bei ya huduma za umeme kwa asilimia 18.19 na kupendekeza kuwa bei
hiyo ianze rasmi Januari Mosi mwaka 2017.
Kwa mujibu wa Shirika hilo,
liliomba kuidhinishiwa ongezeko la bei ya huduma hizo kwa ajili ya
kuliwezesha shirika kupata fedha za kulipia gharama za uendeshaji,
kupata fedha za uwekezaji katika miundombinu pamoja na kuhakikisha
huduma ya umeme inawafikia asilimia 75 ya wananchi wote ifikapo mwaka
2025.
Baada ya TANESCO kuwasilisha
taarifa zinazohitajika kwa ajili ya kukamilisha maombi yao, EWURA
ilifanya mikutano ya taftishi, matangazo kwa umma pamoja na kushirikisha
wadau mbalimbali kutoa maoni juu ya ongezeko hilo ambapo baada ya
uchambuzi wa maoni hayo ililidhia kuongeza asilimia 8.5 tu ya ongezeko
la bei hizo.
Kwa kuwa Serikali yetu iko
makini, sikivu na inayojali wanyonge kwa kuangalia vipato vyao na hali
zao za kimaisha iliamua kuliangalia suala hilo kwa makini kwani wananchi
wengi katika sehemu mbalimbali nchini wameonekana kutoridhishwa na
upandaji wa bei hizo.
Pongezi nyingi sana zimfikie
Prof. Muhongo, Waziri mwenye dhamana ya Nishati na Madini kwa kutambua
umuhimu wa umeme kwa wananchi hivyo kuamua kusitisha upandaji wa bei ya
nishati hiyo ili kuhakikisha kila mwananchi anaweza kumudu gharama hizo.
Sio tu wananchi kumudu gharama
kwa ajili ya matumizi madogo madogo bali pia kwa upande mwingine,
viwanda haviwezi kuendeshwa bila umeme hivyo uongezaji wa gharama ya
nishati hiyo utasababisha kupungua kwa ukuaji wa viwanda ambapo
itapelekea nchi ya Tanzania kushindwa kufikia uchumi wa kati.
Ni vema kila Asasi inayotoa
huduma kwa wananchi kwa njia ya malipo kuhakikisha kuwa wanatoa
mapendekezo ambayo kwa kiwango kikubwa ni rafiki kulingana na hali
halisi ya maisha ya wananchi ili usiwe mzigo kwao na kusababisha
kuiingiza Serikali yao pendwa katika lawama.
No comments :
Post a Comment