Pages

Monday, January 2, 2017

HONGERA SERIKALI KWA KUWAJALI WANYONGE

index


Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Hakika hakuna ubishi kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inawajali wanyonge na imekukusudia kuwapa unafuu katika kufanikisha mambo mbalimbali ambayo yalikuwa magumu kuwezekana katika kipindi cha nyuma  kwa ajili ya kuharikisha maendeleo.

Hatua hii inatokana na kuwakingia kifua wananchi wenye vipato vya chini kulikoonyeshwa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo na kuungwa mkono na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli la kupinga upandishwaji wa bei ya huduma za umeme.
Naamini kuwa umeme ni huduma muhimu sana katika kuharakisha maendeleo ya mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla kupitia sekta mbalimbali kama vile viwanda na huduma nyingine za kiafya na kijamii.
Kitendo kilichokuwa kimetangazwa cha kutaka kupandisha umeme kingeweza kurudisha nyuma wananchi na sekta nyingine kama vile ujenzi wa viwanda.
Mnamo Oktoba 4 mwaka 2016, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) lilipeleka ombi katika Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) la kuidhinishiwa ongezeko la bei ya huduma za umeme kwa asilimia 18.19 na kupendekeza kuwa bei hiyo ianze rasmi Januari Mosi mwaka 2017.
Kwa mujibu wa Shirika hilo, liliomba kuidhinishiwa ongezeko la bei ya huduma hizo kwa ajili ya kuliwezesha shirika kupata fedha za kulipia gharama za uendeshaji, kupata fedha za uwekezaji katika miundombinu pamoja na kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia asilimia 75 ya wananchi wote ifikapo mwaka 2025.
Baada ya TANESCO kuwasilisha taarifa zinazohitajika kwa ajili ya kukamilisha maombi yao, EWURA ilifanya mikutano ya taftishi, matangazo kwa umma pamoja na kushirikisha wadau mbalimbali kutoa maoni juu ya ongezeko hilo ambapo baada ya uchambuzi wa maoni hayo ililidhia kuongeza asilimia 8.5 tu ya ongezeko la bei hizo.
Kwa kuwa Serikali yetu iko makini, sikivu na inayojali wanyonge kwa kuangalia vipato vyao na hali zao za kimaisha iliamua kuliangalia suala hilo kwa makini kwani wananchi wengi katika sehemu mbalimbali nchini wameonekana kutoridhishwa na upandaji wa bei hizo.
Pongezi nyingi sana zimfikie Prof. Muhongo, Waziri mwenye dhamana ya Nishati na Madini kwa kutambua umuhimu wa umeme kwa wananchi hivyo kuamua kusitisha upandaji wa bei ya nishati hiyo ili kuhakikisha kila mwananchi anaweza kumudu gharama hizo.
Sio tu wananchi kumudu gharama kwa ajili ya matumizi madogo madogo bali pia kwa upande mwingine, viwanda haviwezi kuendeshwa bila umeme hivyo uongezaji wa gharama ya nishati hiyo utasababisha kupungua kwa ukuaji wa viwanda ambapo itapelekea nchi ya Tanzania kushindwa kufikia uchumi wa kati.
Ni vema kila Asasi inayotoa huduma kwa wananchi kwa njia ya malipo kuhakikisha kuwa wanatoa mapendekezo ambayo kwa kiwango kikubwa ni rafiki kulingana na hali halisi ya maisha ya wananchi ili usiwe mzigo kwao na kusababisha kuiingiza Serikali yao pendwa katika lawama.

No comments:

Post a Comment