Monday, December 5, 2016

MH:RAIS MAGUFULI AKABIDIDHI MSAADA WA SHILINGI MILIONI TANO KWA KIJANA HAIDARI BONGE ANAYESUMBULIWA NA TATIZO LA KUOTA NYAMA MWILINI.

tip1
Kaimu Mnikulu Ngusa Samike akimkabidhi Bi Sauda Kasimu fedha tasilumu kiasi cha shilingi milioni tano kama mchango wa  Mh Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli toka kwenye mshahara wake,kwa ajili ya mahitaji ya mototo wake Haidari Bonge anayesumbuliwa na tatizo la kuota nyama mwili. Kulia kwa Bi.  Sauda Kassim ni Dr Andrew Foyi  Daktari bingwa wa magonjwa ya ngozi toka Hosipitali ya Taifa Muhimbili (Picha zote na IKULU)
tip2
Bi Sauda Kasimu akiongea na waandishi wa habari mara baada ya kupokea fedha tasilumu kiasi cha shilingi milioni tano kutoka kwenye mshahara wa Mhe. Rais Magufuli na kwa ajili ya mahitaji ya mototo Haidari Bonge anayesumbuliwa na tatizo la kuota nyama mwilini. Bi. Sauda Kassim amemshukuru Mhe Rais kwa msaada huo na kuomba Watanzania wengine kuendelea kumsaidia kijana wake.
tip3
Afisa mawasilioano na Huduma kwa wateja toka benki ya CRDB Bw Godwin Semunyu akimkabidhi kiasi cha Shilingi laki tano Bi Sauda  Kasimu ili kuunga mkono hatua ya Mh Rais Magufuli ya kutoa sehemu ya mshahara wake kiasi cha shilingi milioni tano za kuweza kumsaidia mtoto Haidari Bonge anayesumbuliwa na tatizo la kuota nyama mwilini.
tip4
Bi Sauda Kassim akiweka saini kwenye kadi ya mashine za kutolea fedha (ATM)  mara baada ya kukamilisha zoezi la kufungua akaunti ya benki katika tawi la CRDB Azikiwe jijini Dar es salaam itakayokuwa ikitumiwa na wasamaria wema kuweza kupokelea michango mbalimbali kwa ajili ya kumhudumia mtoto wake Haidari Bonge anayesumbuliwa na tatizo la kuota nyama mwilini. Akaunti hiyo ni namba 01522336450100 SAUDA KASSIMU tawi la Azikiwe

…………………………………………………………………..
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli leo tarehe 5 Desemba, 2016 wamekabidhi msaada wa Shilingi Milioni 5 kwa ajili ya kusaidia matibabu ya mtoto Haidari Bonge mwenye umri wa miaka 9 anayesumbuliwa na tatizo la kuota nyama kichwani, kinywani na machoni.
Fedha hizo zimekabidhiwa kwa Mama wa mtoto huyo Sauda Kassim  na Kaimu Mnikulu Ndugu Ngusa Samike kwa  niaba ya Rais Dokta Magufuli katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo mtoto huyo anapatiwa matibabu.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi fedha hizo, Kaimu Mnikulu Ndugu Ngusa  Samike amesema Rais Dkt. Magufuli ameguswa baada ya kutazama kipengele cha Hadubini “Habari kwa Kina” kilichorushwa hewani katika taarifa ya habari saa 2 usiku na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) tarehe 03 Desemba, 2016.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa magonjwa ya ngozi Dkt. Andrew Foi amesema mtoto Haidari anayeishi Mbagala Kuu Jijini Dar es Salaam alianza kuota nyama miezi mitatu baada ya kuzaliwa na amekuwa akifanyiwa upasuaji wa kuondoa nyama hizo mara kwa mara.
Dkt. Foi amesema Hospitali ya Taifa Muhimbili inatoa matibabu ya mtoto huyo bure tangu awasili hospitalini hapo isipokuwa kwa matibabu ambayo hayapatikani hospitalini hapo ndio analazimika kuyalipia katika sehemu husika.
Amesema mtoto Haidari anahitaji eneo maalum la kuishi muda wote ambalo lina giza na kuvaa nguo nyeusi zinazomfunika mwili wote ili kujikinga na miale ya jua ambayo imekuwa ikimuathiri kwa kiasi kikubwa.  
Mama wa mtoto Haidari, Ndugu  Sauda Kassim amemshukuru Rais Dkt. Magufuli na mke wake Mama Janeth Magufuli kwa moyo wa upendo waliouonesha baada ya kuguswa na shida zinazomkabili mtoto wake na kutoa msaada huo na hivyo kuomba wananchi wengine waige mfano wa Rais na Mkewe katika kumsaidia mwanawe.
Tayari mtoto Haidari  Bonge, ameshafunguliwa akaunti katika Benki ya CRDB tawi la Azikiwe yenye namba 0152236450100, ambapo benki hiyo kupitia kwa meneja Uhusiano wake Godwin Semunyu amekabidhi shilingi laki Tano ikiwa ni msaada kutoka Benki hiyo.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
05 Desemba, 2016

No comments :

Post a Comment