Kaimu Mnikulu Ngusa Samike
akimkabidhi Bi Sauda Kasimu fedha tasilumu kiasi cha shilingi milioni
tano kama mchango wa Mh Rais Dkt John Pombe Joseph Magufuli toka kwenye
mshahara wake,kwa ajili ya mahitaji ya mototo wake Haidari Bonge
anayesumbuliwa na tatizo la kuota nyama mwili. Kulia kwa Bi. Sauda
Kassim ni Dr Andrew Foyi Daktari bingwa wa magonjwa ya ngozi toka
Hosipitali ya Taifa Muhimbili (Picha zote na IKULU)
Bi Sauda Kasimu akiongea na
waandishi wa habari mara baada ya kupokea fedha tasilumu kiasi cha
shilingi milioni tano kutoka kwenye mshahara wa Mhe. Rais Magufuli na
kwa ajili ya mahitaji ya mototo Haidari Bonge anayesumbuliwa na tatizo
la kuota nyama mwilini. Bi. Sauda Kassim amemshukuru Mhe Rais kwa msaada
huo na kuomba Watanzania wengine kuendelea kumsaidia kijana wake.
Afisa mawasilioano na Huduma kwa
wateja toka benki ya CRDB Bw Godwin Semunyu akimkabidhi kiasi cha
Shilingi laki tano Bi Sauda Kasimu ili kuunga mkono hatua ya Mh Rais
Magufuli ya kutoa sehemu ya mshahara wake kiasi cha shilingi milioni
tano za kuweza kumsaidia mtoto Haidari Bonge anayesumbuliwa na tatizo la
kuota nyama mwilini.
Bi Sauda Kassim akiweka saini
kwenye kadi ya mashine za kutolea fedha (ATM) mara baada ya kukamilisha
zoezi la kufungua akaunti ya benki katika tawi la CRDB Azikiwe jijini
Dar es salaam itakayokuwa ikitumiwa na wasamaria wema kuweza kupokelea
michango mbalimbali kwa ajili ya kumhudumia mtoto wake Haidari Bonge
anayesumbuliwa na tatizo la kuota nyama mwilini. Akaunti hiyo ni namba
01522336450100 SAUDA KASSIMU tawi la Azikiwe
…………………………………………………………………..
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Mkewe Mama Janeth Magufuli leo
tarehe 5 Desemba, 2016 wamekabidhi msaada wa Shilingi Milioni 5 kwa
ajili ya kusaidia matibabu ya mtoto Haidari Bonge mwenye umri wa miaka 9
anayesumbuliwa na tatizo la kuota nyama kichwani, kinywani na machoni.
Fedha hizo zimekabidhiwa kwa Mama
wa mtoto huyo Sauda Kassim na Kaimu Mnikulu Ndugu Ngusa Samike kwa
niaba ya Rais Dokta Magufuli katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ambapo
mtoto huyo anapatiwa matibabu.
Akizungumza mara baada ya
kukabidhi fedha hizo, Kaimu Mnikulu Ndugu Ngusa Samike amesema Rais
Dkt. Magufuli ameguswa baada ya kutazama kipengele cha Hadubini “Habari kwa Kina” kilichorushwa hewani katika taarifa ya habari saa 2 usiku na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) tarehe 03 Desemba, 2016.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa
magonjwa ya ngozi Dkt. Andrew Foi amesema mtoto Haidari anayeishi
Mbagala Kuu Jijini Dar es Salaam alianza kuota nyama miezi mitatu baada
ya kuzaliwa na amekuwa akifanyiwa upasuaji wa kuondoa nyama hizo mara
kwa mara.
Dkt. Foi amesema Hospitali ya
Taifa Muhimbili inatoa matibabu ya mtoto huyo bure tangu awasili
hospitalini hapo isipokuwa kwa matibabu ambayo hayapatikani hospitalini
hapo ndio analazimika kuyalipia katika sehemu husika.
Amesema mtoto Haidari anahitaji
eneo maalum la kuishi muda wote ambalo lina giza na kuvaa nguo nyeusi
zinazomfunika mwili wote ili kujikinga na miale ya jua ambayo imekuwa
ikimuathiri kwa kiasi kikubwa.
Mama wa mtoto Haidari, Ndugu
Sauda Kassim amemshukuru Rais Dkt. Magufuli na mke wake Mama Janeth
Magufuli kwa moyo wa upendo waliouonesha baada ya kuguswa na shida
zinazomkabili mtoto wake na kutoa msaada huo na hivyo kuomba wananchi
wengine waige mfano wa Rais na Mkewe katika kumsaidia mwanawe.
Tayari mtoto Haidari Bonge,
ameshafunguliwa akaunti katika Benki ya CRDB tawi la Azikiwe yenye namba
0152236450100, ambapo benki hiyo kupitia kwa meneja Uhusiano wake
Godwin Semunyu amekabidhi shilingi laki Tano ikiwa ni msaada kutoka
Benki hiyo.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
05 Desemba, 2016
No comments:
Post a Comment