Tuesday, June 20, 2023

‘Shilingi ya Tanzania fedha pekee inayoruhusiwa kutumika nchini’-Benki Kuu.

 


Christian Gaya-HakiPensheni Centre

Benki Kuu ya Tanzania inasema ya kuwa shilingi ya Tanzania ndiyo fedha ya pekee inayoruhusiwa kutumika nchini. Hivyo hakuna mtu au kampuni yoyote inayoruhusiwa kuikataa kwa...

malipo yoyote halali.

Kufuatana na maelezo hayo yaliyotolewa na Benki Kuu inasema ya kwamba Serikali ilishatoa tamko kuhusu katazo la matumizi ya fedha za kigeni kwa wakaazi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kulipia bidhaa na huduma nchini.

“Hata hivyo, katika siku za karibuni imebainika kuwepo kwa ukiukwaji wa Tamko hilo. Hivyo, Benki Kuu inapenda kuukumbusha umma kwamba maagizo yaliyotolewa hapo awali kuhusu matumizi ya fedha za kigeni,”maelezo yanaeleza.

Maelezo haya yanasisitiza ya kuwa bei zote hapa nchini zitangazwe kwa shilingi ya Tanzania. “Bei hizi zinajumuisha kodi za kupangisha ardhi, nyumba na ofisi; gharama za elimu; huduma za afya, vifaa tiba na vitendanishi; gharama za usafiri, lojistiki na bandari; vifaa vya kielektroniki na huduma za mitandao ya mawasiliano.

Maelezo ya Benki Kuu hayo yanasisitiza ya kuwa bei ambazo walengwa wake wakuu ni watalii au wateja wasio wakaazi zinaweza kutangazwa kwa fedha za kigeni na malipo yake yanaweza kufanyika kwa fedha za kigeni. Bei hizi zinajumuisha gharama za hoteli, usafiri, gharama za viwanja vya ndege na viza kwa wageni, usafirishaji kwenda nchi za nje kupitia Tanzania na gharama za mizigo bandarini.

“Walipaji wanaotumia fedha za kigeni watambuliwe kwa vitambulisho vyao kama pasi za kusafiria na nyaraka za usajili kwa makampuni” Gavana anasema.

Anasema, viwango vya kubadilisha fedha vitakavyotumika katika kuweka bei hizo viwekwe wazi na visizidi vile vya soko. Ifahamike wazi kuwa ni benki na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni pekee yanayoruhusiwa kupanga viwango vya kubadilisha fedha kutokana na ushindani katika soko la fedha za kigeni.

“Mkaazi yeyote wa Tanzania anapaswa kufanya malipo kwa kutumia shilingi ya Tanzania pekee na hivyo asilazimishwe kulipia bidhaa au huduma yoyote hapa nchini kwa kutumia fedha za kigeni,” anasisitiza.

No comments :

Post a Comment