Thursday, December 31, 2020

MAAFISA USTAWI WA JAMII NA MAAFISA MAENDELEO YA JAMII WAHIMIZWA KUENDELEA KUTOA HUDUMA BORA KWA WATU WENYE ULEMAVU


Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe.
Ummy Nderiananga akizungumza na Maafisa Ustawi wa Jamii pamoja na
Maafisa Maendeleo ya Jamii wakati wa kikao kazi kilichofanyika Jijini
Dar es Salaam Disemba 30, 2020 katika ukumbi wa Mkutano wa Anatouglou
uliopo kwenye ofisi ya halmashauri ya Ilala lengo ikiwa ni kujadiliana
na kushauriana namna bora ya kuhudumia watu wenye ulemavu pamoja na
kutatua changamoto zinazo wakabili. (Kushoto) ni Katibu Tawala wa
Wilaya ya Ilala, Bi. Charangwa Makwiro.
Baadhi ya Maafisa Ustawi wa Jamii pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii
walioshiriki kikao kazi hicho wakifuatilia kwa makini hotuba ya Naibu
Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy
Nderiananga (hayupo pichani.)
Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Bi. Charangwa Makwiro akieleza jambo
wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga alipokutana na
Maafisa Ustawi wa Jamii pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii
kujadiliana pamoja na kushauriana namna bora ya kuhudumia watu wenye
ulemavu pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe.
Ummy Nderiananga akiteta jambo na Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala,
Bi. Charangwa Makwiro (kushoto) wakati wa kikao kazi hicho.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe.
Ummy Nderiananga (katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Maafisa
Ustawi wa Jamii pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii wakati wa kikao
kazi kilichofanyika Jijini Dar es Salaam Disemba 30, 2020 katika
ukumbi wa Mkutano wa Anatouglou uliopo kwenye ofisi ya halmashauri ya
Ilala kwa ajili ya kujadiliana na kushauriana namna bora ya kuhudumia
watu wenye ulemavu pamoja na kutatua changamoto zinazo wakabili.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Wenye Ulemavu Mhe.
Ummy Nderiananga akisalimiana na Afisa Mipango na Uratibu ambaye pia
ni Mwakilishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Gerald
Sando mara baada ya kuwasili Jijini Dar es Salaam kwa ziara ya kikazi.
(Katikati) ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Bi. Charangwa Makwiro.




MAAFISA Ustawi wa Jamii pamoja na Maafisa Maendeleo ya Jamii
wamehimizwa kutoa huduma bora kwa watu wenye ulemavu ili kuimarisha
ustawi na kuchochea maendeleo ya kundi hilo maalum.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia
Wenye Ulemavu Mhe. Ummy Nderiananga alipokutana na Maafisa hao katika
kikao kazi kilichofanyika Jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa
Mkutano wa Anatouglou uliopo kwenye ofisi ya halmashauri ya Ilala
lengo ikiwa ni kujadiliana pamoja na kushauriana namna bora ya
kuhudumia watu wenye ulemavu pamoja na kutatua changamoto zinazo
wakabili.

Mheshimiwa Ummy alieleza kuwa Serikali kwa kutambua na kuthamini haki
za wenye ulemavu imekuwa ikishirikiana na asasi za Watu wenye ulemavu
kwa nia njema na dhamira ya dhati ili kuhudumia kundi hilo kwa
kuwapatia huduma bora kulingana na jamii inayowazunguka.

“Katika kipindi kifupi serikali imetimiza wajibu wake huo kwa kutoa
Elimu, huduma za Afya, mafunzo ya stadi za kazi, ajira, nyenzo za
kujimudu, huduma za kijamii, kuwezeshwa kiuchumi na vilevile kuboresha
miondombinu ili iwe Rafiki kwa matumizi ya watu wenye ulemavu katika
kupata huduma stahiki,” alieleza Mheshimiwa Ummy.

Aliongeza kuwa kundi hilo hapo nyuma liliachwa lakini tangu Serikali
ya Awamu ya Tano iingie madarakani kundi hilo linapigiwa chapuo na
limekuwa likijumuishwa katika kila nyanja muhimu, lakini serikali
iliyopo imeendelea kujenga mazingira kwa wenye ulemavu ili waweze
kujiletea maendeleo kwa kutumia rasilimali zilizopo katika kuboresha
huduma zao.

“Malengo ya serikali ni kuhakikisha inaendeleza watu wenye ulemavu
pasipo kuachwa nyuma na hivyo katika kutambua hilo imeendelea
kuwahamasisha wenye ulemavu kushiriki katika kila nyanja,” alisema.

Sambamba na hayo, amewata Maafisa hao kuongeza juhudi na kasi katika
kuhamasisha Watu wenye Ulemavu, Vijana na Wanawake kuanzisha vikundi
ambavyo vitachangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na halmashauri kwa
kuanzisha miradi au kuendeleza miradi waliyonayo ili waweze kujikwamua
kiuchumi.

“Upo umuhimu wa kutambua uwezo na vipaji maalum vya watu wenye
ulemavu, vijana na wanawake na kuweka mikakati madhubuti ya
kuviendeleza vikundi wanavyoanzisha ili waweze kujikomboa kiuchumi na
waweze kuajiri watu wengine,” alisema Ummy.

Alifafanua kuwa katika suala la uwezeshaji wa watu wenye ulemavu
inaonyesha kuwa wametambua umuhimu wa mikopo hiyo inayotolewa na
halmshauri na ndio maana wamekuwa wakijitokeza kuchukua mikopo
inayotolewa na halmashauri.

“Jambo hili limenifurahisha kuona sasa mikopo inatolewa kwa wingi kwa
watu wenye ulemavu ambao wamekuwa wakikumbana na changamoto nyingi,
tunashuhudia kupitia uwezeshaji huo kumekuwa na ongezeko la miradi
mbalimbali inayoendeshwa na wenye ulemavu,” alisema Ummy.

“mafanikio haya yanayoonekana yanatokana na juhudi zenu kama maafisa
wa serikali katika kupanga utekelezaji wa shughuli zenu vizuri,
muongeze juhudi katika kutoa huduma bora ili kwa pamoja kutimiza
malengo ya kukuza uchumi wa taifa letu,” alieleza.

Aidha, Naibu Waziri Ummy alitoa rai kwa vikundi ambavyo vimekuwa na
tabia ya kukopa katika halmashauri moja na baadae kuhamia kwenye
halmashauri nyingine kutaka kukopa tena kwenye halmashauri nyingine
kuacha mara moja tabia hiyo huku akiwataka warejeshe mikopo yao kwanza
ndio wakope tena.

Pia, Mheshimiwa Ummy alitumia fursa hiyo kuvitanga vikundi vya watu
wenye ulemavu kuachana na kasumba kuwa mikopo wanayopatiwa na
halmashauri ya 2% kuwa ni misaada au inatolewa bure badala yake wakope
na kurejesha kwa wakati ili waweze kukopeshwa tena zaidi.

Akizungumza kabla, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ilala, Bi. Charangwa
Makwiro alieleza kuwa bado yanafanyika maboresho makubwa katika
kuwezesha watu wenye ulemavu, vijana na wanawake ili kuboresha miradi
yao iweze kunufaika kiuchumi zaidi.

Kwa upande wake, Afisa Mipango na Uratibu ambaye pia ni Mwakilishi wa
Sekretarieti ya Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Gerald Sando alieleza kuwa
Halmashauri zote sita za mkoa zimekuwa zikitoa mikopo hiyo katika kila
mwaka wa fedha sambamba na kujiwekea mikakati ya kuwezesha vikundi
vingi zaidi.

Naye, Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Halmashauri ya Kigamboni Bi.
Christina alisema kuwa tangu kuanzishwa kwa halmashauri hiyo
wamefanikiwa kuwezesha vikundi vingi ikiwemo watu wenye ulemavu kwa
kuwapatia mikopo ya bajaji, usindikaji na mikopo mingine inayoendana
na ulemavu alionao mtu husika.

Katika kikao kazi hicho walishiriki Maafisa Ustawi wa Jamii, Maafisa
Maendeleo ya Jamii pamoja na Maafisa Vijana ambao walipata fursa ya
kutoa taarifa ya uwezeshaji wa mikopo ya 10% inayotolewa na
halmashauri zao kwa Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu.

 

No comments :

Post a Comment