Saturday, May 2, 2020

MUHIMBILI,RRH-DODOMA WAPOKEA MSAADA WA MAGARI YA WAGONJWA



Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Dharura katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. Juma Mfinanga akipokea msaada wa moja ya magari ya kubeba wagonjwa kutoka kwa Mkurugenzi wa Australia Tanzania Society Bw. James Chialo. Gari moja ni kwa ajili ya Muhimbili na jingine ni la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma. Kulia ni Balozi wa shirika hilo, Bw. Banana Zoro.
Pichani ni moja ya gari la kubeba wagonjwa.
Mwakilishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Bw. Maxmillian Tryphone akipokea moja magari kutoka kwa Mkurugenzi wa Australia Tanzania Society Bw. James Chialo.
Wawakilishi wa Muhimbili na Hopistali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kupokea msaada huo.
…………………………………………………………………………………
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma (RRH) leo wamepokea msaada wa magari mawili ya kubeba wagonjwa kutoka asasi ya Australia Tanzania Society  (ATS) kupitia Rafiki Surgical Mission.
Akipokea msaada huo, kwa niaba ya MNH na Dodoma, Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya
Dharura wa MNH, Dkt. Juma Mfinanga amesema msaada huu umekuja wakati mzuri kwani matumizi ya magari haya hospitalini ni makubwa.
Dkt. Mfinanga ameishukuru Rafiki Surgical Mission imekua msaada mkubwa kwa Muhimbili kwani wamekua wakisaidia sana hasa upande wa upasuaji (plastic surgery).
“Rafiki Surgical Mission wamekuwa msaada mkubwa kwa Muhimbili kwani wamekuwa wakisaidia kwa muda mrefu hasa katika eneo la upasuaji. Lakini pia wamesaidia kupeleka madaktari bingwa na wauguzi nje ya nchi ili kuwajengea uwezo. Tunawashukuru kwa msaada huu,” amesema Dkt. Mfinanga.
Kwa upande wa mwakilishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Bw. Maxmillian Tryphone ameshukuru kupatiwa msaada huo kwani itasaidia kwa kiwango kikubwa katika kuendesha shughuli za matibabu hospitalini hapo.
Naye Mkurugenzi wa ATS Bw. James Chialo amesema leo amekabidhi magari hayo na kufikisha idadi ya magari sita ambayo wameshatoa msaada nchini na kuna magari kama hayo 10 wataleta na kuyasambaza nchini ili kusaidia sekta ya afya.
Amesema ATS kupitia Rafiki Surgical Missions kila mwaka wamekua wakileta watalaamu wa upasuaji ili kushirikiana na watalaamu wa hapa nchini kufanya aina mbalimbali za upasuaji.
Balozi wa ATS, Bw. Banana Zoro amesema amekuwa akifanya kazi na asasi hiyo katika kusaidia sekta ya Afya nchini na kwamba ni jambo zuri kushiriki katika shughuli ya utoaji wa msaada huo.

No comments :

Post a Comment