***************************
*Asema wenye maambukizi wamefikia 480 ikiwa ni ongezeko la wagonjwa 196
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amesema wagonjwa 167 wamepona ugonjwa wa homa kali ya
mapafu inayosababishwa virusi vya corona (COVID-19) na ameendelea
kuwasisitiza Watanzania wachukue tahadhari ya kutosha na wafuate ushauri
wa Wataalamu wa Afya na
maelekezo ya Serikali.
Hata hivyo,
Waziri Mkuu amesema kuanzia tarehe 23 hadi 28 Aprili, 2020 wamepatikana
watu wengine wapya wenye maambukizi ya Corona 196 (Bara 174 na Zanzibar
22 ambao walitangazwa na Waziri wa Afya wa SMZ) na kufanya jumla ya
wenye maambukizi nchini kuwa 480.
Waziri Mkuu
ametoa taarifa hiyo ya mwenendo wa ugonjwa wa COVID-19 nchini leo
(Jumatano, Aprili 29, 2020) kwenye viwanya vya Ofisi ya Waziri Mkuu,
Mlimwa jijini Dodoma wakati akikabidhi magari ya kubebea wagonjwa kwa
wabunge. Pia amesema mbali na magari hayo kutolewa kwa ajili ya
kuboresha huduma za mama na mtoto yatatumika kuwahudumia wagonjwa wa
COVID-19.
“Tarehe 24
Aprili Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
aliwatangaza jumla ya waliopona kuwa ni 37 na hivyo kufanya jumla ya
waliopona kuwa 48. Leo tunafurahi kusema kuwa idadi ya waliopona
imeongezeka kutoka 48 na kufikia 167 (Zanzibar 36 waliotanganzwa jana na
Waziri wa Afya – SMZ na Bara 83).”
“Tunasikitika
kueleza kuwa tuna ongezeko la vifo sita na kufanya jumla ya vifo sasa
kuwa 16. Hata hivyo kati ya wenye maambukizi 297 waliobaki, watu 283
wanaendelea vizuri sana na watu 14 wako chini ya uangalizi maalum na
tunaendelea kuwaondoa walio karibu na wagonjwa (contacts) walio
karantini baada ya kumaliza siku 14.”
Waziri Mkuu
ameongeza kuwa hadi tarehe 28 Aprili, 2020 watu 644 wameruhusiwa, ambao
wanatoka katika mikoa ya Zanzibar, Dar-es-Salaam, Tanga, Kilimanjaro,
Arusha, Mwanza, Kagera, Dodoma, Kigoma na Songwe.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu amewataka wananchi wachukue tahadhari kuhusu
taarifa za upotoshaji kwani kwa sasa kumeibuka tabia ya watu kutoa
takwimu zisizo sahihi kuhusu vifo vitokanavyo na ugonjwa wa COVID-19
ambazo zinasababisha mtafaruku usio wa lazima katika jamii.
“…Sio kila
kifo ni cha Corona, tunasahau kuwa magonjwa mengine yanaua pia sio kila
anayeugua na anayekufa ni corona tuna malaria, BP, kisukari, ukimwi ni
magonjwa yanayoua. Tuache tabia ya kupotosha umma. Tuwaache wataalam
wetu wafanye kazi zao.”
“Kwa wale
ambao hawana maambukizi waendelee kufanya kazi zao, mkulima aende
akalime tupate chakula cha kutosha, waliko maofini wawajibike kufanya
kazi, waliopo viwandani wafanye kazi na kila mmoja na sekta yake kama
unafanyabiashara sokoni toa huduma ili wananchi wasikose kupata huduma
wanazozihitaji.”
Hata hivyo,
Waziri Mkuu ameendelea kuwasisiza Watanzania wazingatie maelekezo
yanayotolewa na Serikali katika kujikinga na COVID-19 ikiwa ni pamoja na
kujiepusha na misongamano. “Tukizingatia makatazo na maeneo yenye
tahadhari tutaishinda vita hii dhidi ya ugonjwa huu.”
No comments :
Post a Comment