Tuesday, March 31, 2020

VIONGOZI WA DINI RUKWA WAAZIMIA KUPUNGUZA MUDA WA IBADA KUJIHADHARI NA CORONA





Mganga Mkuu wa mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu akitoa Elimu ya Ugonjwa wa Corona (Covid -19) Kwa viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini (Hawapo pichani).
Mchungaji Byanosisi Mwikole wa kanisa la Monravian akichangia mada katika kikao cha viongozi wa dini kilichoitishwa na mkuu wa mkoa wa Rukwa ili kupewa elimu juu ya namna ya kuepukana na Ugonjwa wa Corona (Covid -19)
Baadhi ya Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini wakisikiliza kwa makini elimu wanayopatiwa juu ya namna ya kuepukana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona (Corona-19) kutoka kwa mganga mkuu wa mkoa wa Rukwa (hayupo pichani) 
Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Julieth Binyura akitoa neno la kufunga kikao hicho kifupi kilichowakutanisha viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini katika mkoa wa Rukwa.
Viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini katika mkoa wa Rukwa wakiiombea nchi kuepukana na ugonjwa wa Corona (Covid-19) mara baada ya kumaliza kikao kilichoitishwa na mkuu wa mkoa wa Rukwa. 
…………………………………………………………………………………………………..
Viongozi wa madhehebu ya dini mkoani Rukwa wamekubaliana kuwa kila dhehebu kulingana na
imani zao kuona namna ya kupunguza muda wa kufanya ibada katika misikiti na makanisa mbalimbali ili kukabiliana na ugonjwa wa homa kali ya mapafu unaosababishwa na virusi vya Corona (Covid-19).
Wamekubaliana hayo wakati wa kikao kifupi kilichoitishwa na Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Julieth Binyura katika kikao hicho kilicholenga kuwaelimisha viongozi hao juu ya Chanzo, usambaaji na namna ya kujikinga na ugonjwa huo ambao unaendelea kuisumbua dunia huku jukumu la kutoa elimu likifanywa na Mganga mkuu wa mkoa wa Rukwa.
Wakati akielezea namna ya kutekeleza azma hiyo Shekhe wa mkoa wa Rukwa Rashid Akilimali alisema kuwa atazungumza na mashekhe wa wilaya na Maimamu wa miskiti ya mkoa huo kupunguza muda wa ibada ili kukwepa kuwaweka watu wengi katika eneo moja kwa muda mrefu lakini pia kuwafanya waumini hao wasikose ibada hizo.
“Niungane na Askofu wa Monravian, tupunguze nyakati za ibada zetu, na kubwa iwe ni kuongoza dua na maombi kwaajili ya nchi yetu, sisi tumelipunguza hili baada ya kutokea hili, ibada ya nusu saa tumekwenda dakika kumi na tano, dakika kumi inakuwa ni mahubiri na dakika tano ni kuiombea nchi ili Mungu atuepushe na jambo hili,” alisema
Naye Mwakilishi wa Kanisa la Anglikan Mkoani Rukwa Mchungaji Mathias Gwakila alisema kuwa atajitahidi kufikisha ujumbe na elimu aliyoipata kutokana na namna alivyojifunza na kuwasisitiza waumini hao kuendelea kufanya maombi ili kuepukana na ugonjwa huo na kusisitiza kuwa ugonjwa huo ni pepo na hivyo hatunabudi kulikemea na kisha kushauri juu ya kufupisha ibada.
“Hicho ni kitu muhimu mno, ibada ziwe fupi zisiwe ndefu, kwahiyo kwa ushauri wangu kupitia madhehebu mengine yote, viongozi wote wa madhehebu wajitahidi kufupiza, kwa mfano kanisa la Anglican ibada zetu ni masaa mawili, sasa tufupishe, ibada ichukue saa moja katika vipengele vyovyote vile ambavyo wewe utaviona upunguze kipi na kipi ilimradi ibada iwe fupi watu watoke mapema,” Alisema.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Kanisa la Waadventista Wasabato Jimbo la Ziwa Tanganyika Mchungaji Haruni Kikiwa alisema kuwa kupitia kikao hicho wamepata elimu ya kutosha ya namna ya kuwaelekeza wananchi ambao ni waumini wao juu ya namna ya kupambana na janga la kirusi cha Corona na kusisitiza kuwa atayafikisha kwa askofu ili kusambazwa kwa makanisa.
“Tunachukua hatua za kunawa kabla ya ibada na baada ya ibada, lakini pia hatua za kupunguza muda wa ibada ili kupunguza muda wa waumini kukaa pamoja katika msongamano lakini pia hatua za kupunguza misongamano kwa makanisa makubwa kwa maana wanaweza wakafanyia hata nje ili kupunguza msongamano watu wakae mbalimbali, haya yote nitayafikisha,” alisema.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Dkt. Boniface Kasululu wakati akieleza namna ya kujikinga na ugonjwa huo alitoa msisitizo kwa viongozi hao kutumia maji tiririka pamoja na sabuni ya maji wakati wa kunawa huku akieleza madhara ya kutumia sabuni ya unga na ya kipande kuwa na tabia ya kushikwa na kila mtumiaji.
“Sabuni ya unga ambayo imechanganywa na maji ikawekwa kwenye chombo maalum kama chupa, kwahiyo mtu anaweza kuitumia hii, tunaepuka kuweka sabuni ya unga kama ilivyo kwamba mtu mmoja achukue na mwingine aje achukue na mwingine achukue, tunaepuka kuweka sabuni ya kipande kwasababu lazima mtu aje aishike akishajipaka arudishe mwengine aje aishike, kwahiyo tunasema ni sabuni ya maji na kama ni sabuni ya unga basi ichanganywe na maji,” Alisisitiza.
Wakati akifunga kikao hicho Mkuu wa Wilaya ya Kalambo Mh. Julieth Binyura aliwaomba viongozi hao kuzingatia makubaliano ya kikao hicho na kuongeza kuwa anaamini viongozi wa dini wasingependa waumini wao wateketee na kisha kusisitiza juu ya kupunguza muda wa ibada pamoja na mikusanyiko hasa kwa madhehebu ambayo yana waumini wengi.
“Kuna makanisa ambayo ni madogo sana au misikiti midogo watu wanajua lakini kama mikiti naona wameshajipanga wao wanasali muda mfupi lakini kuna makanisa mengine tunatumia masaa mengi, mkishaingia saa 4 mpaka saa 9 kwahiyo huo ni muda mrefu sana mnaweza mkajichanganya sana, hivyo ninaona kwamba hii kumbunguza mud ani muhimu zaidi, vile vipindi vyetu tuvipunguze zaidi tutoe elimu hasa ya kuwa na imani,” Alisistiza
Aidha, alibainisha kuwa kama serikali hawataweza kuwapangia muda wa kufanya inbada hizo huku akiweka msisitizo kuwa imani zinatofautiana na kufafanua kuwa waumini hao wanaweza hata kulala ndani ya makanisa yao kwa kuomba lakini msisitizo ni kuwa wachache ili kuepusha msongamano.

No comments :

Post a Comment