Muonekano wa moja ya mabasi
yaliyoundwa na Kampuni ya BM Motors iliyopo Kibaha mkoani Pwani kama
linavyoonekana likiwa tayari kuanza kutumika .
………………………………………………………………………………………………………….
Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya BM Motors iliyopo
Kibaha mkoani Pwani, imeingia kwenye orodha ya
kampuni zinazounda na
kutengeneza mabasi ya abiria hapa nchini.
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Bw.
Jonas Nyagawa amesema, karakana hiyo iliyojengwa eneo la Zegereni katika
Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani inatengeneza mabasi yenye
uwezo wa kubeba abiria kati ya 45 hadi 57.
Akiongea na Maafisa Habari kutoka
Idara ya Habari – MAELEZO, amesema, kutoka na na msukumo wa mazingira
wezeshi ya Serikali katika kuunga mkono Sera ya viwanda nchini, ameweza
kufanikisha ndoto yake ya kuanzisha karakana hiyo miezi sita iliyopita.
Amesema, ni fursa pekee katika
kipindi hiki ambacho Serikali ya Awamu ya Tano inahamasisha Wananchi
kuanzisha viwanda nchini ili kujenga uchumi wa nchi na kuongeza ajira
kwa vijana.
“Serikali imekuwa ikisisitiza
uanzishaji wa viwanda ili nchi yetu ifikie uchumi wa kati na Wananchi
waweze kuwa na kipato cha kati. Ili kufikia azma hiyo lazima kujengwe
viwanda vingi na wananchi nao wapate ajira.”
Bwana Nyagawa amesema, vifaa vinavyotumika kuunda mabasi hayo vinatoka sehemu mbalimbali, huku asilimia 55 vikitoka nje ya nchi.
Tangu karakana hiyo ianze kufanya
kazi tayari mabasi mawili yameshaundwa na yako katika hatua za mwisho za
usajili ili kuanza kufanya kazi.
“Kila kitu kinawezekana,
Watanzania wanapaswa kuwa na uthubutu. Karakana hii inaunda mabasi na
sio kwamba vifaa vyote vinatoka nje ya nchi, vingine vinapatikana hapa
hapa nchini.” Amesema.
Kufuatia uanzishwaji wa kampuni
hiyo, hadi sasa imetoa ajira kwa Watanzania 15 huku baadhi yao
wakiongeza ujuzi kutoka kwa Wataalamu wa nje ya nchi wanaofanya kazi na
kampuni hiyo.
Frank Ngewe ambaye ni fundi mkuu
wa karakana hiyo amesema, ujenzi wa karakana hiyo umekuwa mkombozi
mkubwa kwa vijana hususani wale waliopata mafunzo ya uchomeleaji vyuma,
umeme, rangi n.k.
“Kwanza tunamshukuru Rais wetu na
Serikali kwa ujumla kwa kukazania Sera ya Tanzania ya Viwanda.
Watanzania wengi hususan vijana hivi sasa wanapata ajira na kujikwamua
kimaisha kutokana na kuanzishwa kwa viwanda nchini. ”Amefafanua zaidi
Bw. Ngewe.
Kwa upande wake Elibariki Maleshe
ambaye ni fundi bodi wa mabasi katika karakana hiyo ameeleza kwamba,
vijana wanapaswa kuchangamkia fursa za viwanda ili kupata uzoefu na
kujifunza zaidi vitu vipya.
”Vijana hasa wanaomaliza masomo ya
ufundi wanapaswa kujikita kwenye masuala ya viwanda ili watakapomaliza
masomo yao waweze kupata ajira kwenye viwanda vipya vinavyoanzishwa
nchini.”
Wakati karakana hiyo ikiwa na
miezi sita tu tangu ianze kufanya kazi ya kuunda mabasi, eneo hilo la
Zegereni limetengewa zaidi ya ekari elfu moja kwa ajili ya viwanda
vinavyojihusisha na shughuli mbalimbali ikiwa ni kuiishi Sera ya
Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania ya viwanda.
No comments :
Post a Comment