Lina Ndemfoo akichapa kazi katika kiwanda cha TBL Arusha.
*********************************
Wakati bado kuna dhana kwenye
jamii kuwa baadhi ya kazi ni maalumu kwa ajili ya Wanaume na kusababisha
Wanawake wengi kuzikimbia, wapo baadhi ya Wanawake makini wanaamini
kuwa kazi au taaluma zote zinahusu jinsia zote na wameweza kuthibitisha
suala
hilo kwa vitendo.
Miongoni mwao ni Lina Ndemfoo,
Mhandisi wa mitambo katika kiwanda cha kutengeneza Bia cha TBL kilichopo
mjini Arusha, ambaye pia anatoa wito kwa Wasichana waliopo mashuleni
kuacha dhana ya kuogopa baadhi ya masomo hususani ya Sayansi na hesabu
na kudhani kuwa hawayawezi
Katika mahojiano hivi karibuni
Mhandisi, Lina Ndemfoo, alisema kuwa pamoja na majukumu mengi ya kazi
aliyonayo huwa anahakikisha anasoma mambo mbalimbali kuhusiana ufundi wa
mitambo na teknolojia mpya zinazoibuka kila kukicha duniani ili
kuhakikisha anakwenda sambamba na mabadiliko hayo
“Naipenda taaluma yangu ya
uhandisi wa mitambo, muda wangu mwingi huwa nautumia kusoma mambo mengi
yanayohusiana na fani hii kwa kuwa teknolojia inakuwa kwa kasi kubwa
kiasi kwamba, ukitaka kuwa mtaalamu na kufanya kazi kwa ufanisi kwenye
kampuni kubwa kama TBL, unahitaji kuhakikisha muda wote unakwenda na
wakati”, alisema Lina.
Alisema mara nyingi huwa anawaza
ni jinsi gani wasomi wa fani ya sayansi nchini wanaweza kutumia taaluma
zao kuleta mabadiliko kwenye jamii kupitia ubunifu wa kiteknojia badala
ya kutegemea ubunifu wa wataalamu wa nje ya nchi.
Mhandisi Lina Ndemfoo, alisema
kuwa amepata elimu ya Shahada ya kwanza ya Uhandisi wa Mitambo, katika
chuo cha Dar es Salaam Institute of Technology (DIT) na alikuwa
miongoni mwa wahitimu waliofanya vizuri katika mwaka wao wa 2017.
Baada ya kumaliza masomo
aliajiriwa na Kampuni ya TBL, katika kiwanda cha Arusha, akiwa kama
mwendeshaji mashine za uzalishaji. Kutokana na ufanisi wake katika
kazi katika kipindi cha muda mfupi amepandishwa kufikia nafasi aliyonayo
ya ufundi wa Mitambo.
Mbali na kupata elimu za
vyuoni akiwa mwajiriwa wa TBL, tayari amehudhuria kozi mbalimbali za
ndani ya kampuni ambazo zimezidi kumpatia maarifa katika fani yake na
kumfanya awe na uwezo sambamba na kujiamini katika kuendesha na
kuifanyia matengenezo mitambo iliyotengenezwa kwa teknolojia za kisasa.
“TBL kuna mafunzo ya aina
nyingi na kuna mitambo ya kisasa na tumekuwa tukipata mafunzo ya aina
mbalimbali ikiwemo ya mifumo ya uendeshaji viwanda kwa ufanisi mfano
‘ABInBEV Voyager Plant Optimisation (VPO), ambayo tunaitumia, imeonyesha
mafanikio makubwa na kufanya viwanda vyetu kuwa kioo katika kufanikisha
ajenda ya Serikali ya kuwa na Tanzania ya viwanda”. Alisema.
Pia alisema kuwa anaweza kufanya
kazi zake vizuri kutokana na ushirikiano mzuri anaopata kutoka kwa
wafanyakazi wenzake “TBL ni tanuru la kupika wataalamu na imeajiri watu
wenye uwezo mkubwa katika fani zao hivyo nafanya kazi na wataalamu ambao
wana upeo mkubwa na wanaoelewa nini wanachokifanya bila kuhitaji
usimamizi mkubwa pia inatoa fursa kwa wafanyakazi wa jinsia zote
kusimamia vitengo na mawazo yao kuheshimiwa.
Kuhusu changamoto anazokumbana
nazo katika kazi yake alisema ni za kawaida na kutokana na elimu yake na
uzoefu wa kazi alionao anaweza kuzitatua kwa urahisi na maisha kuendela
kama kawaida.
Lina Ndemfoo,alisema kuwa
anajivunia kufanya kazi na kampuni kubwa kama TBL ambayo imemuwezesha
kujifunza mambo mengi ikiwemo kupata mafanikio mbalimbali katika maisha
yake mojawapo ikiwa ni maendeleo yake binafsi.
Malengo yake ya baadaye ni
kujiendeleza zaidi kielimu ili kwendana na mabadiliko ya kiteknolojia
yanayotokea kila siku hususani katika kipindi hiki ambacho sekta ya
viwanda inazidi kukua kwa kasi na kuhitaji wataalamu tofauti na
ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Anatoa wito kwa vijana wa
kitanzania hasa Wasichana, kutokimbia masomo ya sayansi wanapokuwa
mashuleni bali wajitahidi kukomaa nayo kwa kuwa katika dunia hii ya
sayansi na teknolojia bila wataalamu katika nyanja hii itakuwa vigumu
kwa taifa kupiga hatua ya maendeleo.
Alimalizia kwa kuwaasa
vijana kuacha tamaa ya maisha na kuwa wavumilivu, kutulia na kuwa tayari
kujifunza. “Vijana wengi wa siku hizi wanakuwa sio wavumilivu na
wanapanga malengo makubwa ambayo inakuwa vigumu kuyafikia kwa muda
mafupi matokeo yake wanajikuta wamejiingiza kwenye vitendo ambavyo
vinasababisha wasiaminike kwa waajiri wao na kukosa fursa
mbalimbali.Alitoa wito pia kwa kampuni kuwaamini wanawake na kuwapa
fursa katika nyadhifa mbali mbali katika uongozi.
No comments :
Post a Comment