NA
ELEUTERI MANGI- SAUT
RAIS
Mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin
Mkapa anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi katika uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 20 kuelekea
miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania (SAUT). Kwa
mujibu wa Makamu wa Mkuu wa Chuo hicho Balozi Prof. Costa Ricky Mahalu amesema
kuwa chuo kimemualika Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa kwa kutambua
na kuthamini mchango wake katika elimu ya juu ambapo uzinduzi wa maadhimisho
hayo unatarajiwa kufanyika chuoni hapo Julai, 2 mwaka huu jijini Mwanza. Akiongea
na waandishi wa habari leo chuoni hapo makamu wa Mkuu wa Chuo hicho Balozi
Prof. Mahalu amesema kuwa yapo mafanikio mengi ambayo chuo kinajivunia tangu
kuanzishwa kwake mwaka 1998. Miongoni mwa mafanikio hayo ni pamoja na kuongezeka
udahili wa wanafunzi kutoka wanafunzi 204 hadi wanafunzi 11400 kwa mwaka wa
masomo 2018/2019 licha ya kwamba katika mwaka wa masomo 2012/2013 udahili uliwahi
kufikia wanafunzi 13121 kabla ya kuongezeka kwa matawi 13 ya chuo hicho.
“Katika
mtaala wa chuo, wanafunzi wanapata fursa ya kusoma masomo ya ujasiriamali na
kujiajiri baada ya kuhitimu masomo yao na hivyo kuondokana na dhana ya kungoja
kuajiriwa. Chuo kimeboresha kiwango cha elimu inayotolewa kuhakikisha wahitimu wanahimili soko la ushindani Afrika
Mashariki na duniani kote pia kutokana
na elimu ya dini na maadili kwa wanafunzi wote.” Amesema Balozi Prof.
Mahalu
Katika
kuunga mkono juhudi za Serikali, Balozi Prof. Mahalu amesema kuwa chuo
kimefanikiwa kuanzisha kituo cha kuzalisha na kuwawezesha wajasiriamali ambapo
wanafunzi wanaohitimu masomo yao wanapata fursa ya kuandika mawazo ya biashara
na baada ya mawazo yao kukubalika hupatiwa mafunzo maalumu juu ya mawazo hayo
na kisha wanapatiwa mtaji kati ya shilingi milioni 25 hadi 30 kwa ajili ya
kuendeleza shughuli zao za ujasiriamali.Aidha, chuo hicho kimefanikiwa kuongeza vitivo vingine vinne (4) kutoka kitivo kimoja ambacho kilikuwa cha Sayansi ya Jamii na Mawasiliano kilichokuwa na shahada moja ya Mawasiliano ya Umma na kuongezeka kwa Kitivo cha Biashara na Utawala, Kitivo cha Ualimu, Kitivo cha Sheria na Kitivo cha Uhandisi.
Zaidi ya hayo Balozi Prof. Mahalu amesema chuo cha SAUT kina mchango mkubwa katika kutoa wanataaluma na wataalam katika fani mbalimbali ikiwa ni pamoja na Wahadhiri, Wanahabari, Wanasheria, Wasimamizi katika taasisi za Fedha na Wakaguzi wa Fedha, Walimu, Wahandisi, Wafanyabiashara, Watunza amani katika majeshi ya Ulinzi na Usalama pamoja na Wanasiasa. Miongoni mwa wahitimu hao ni Mhe. Dotto Biteko Waziri wa Madini, Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt. Hassan Abbasi, Zawadi Machibya na Sammy Awami ambao ni watangazaji wa BBC, pamoja na wataalamu mbalimbali wanaofanya kazi ndani na nje ya nchi.
Chuo
cha SAUT nje ya taaluma pia kinatoa huduma kwa jamii ambapo kimefanikiwa kuanzisha
mradi mkuwa wa umeme wa kutumia nishati ya jua kwa kushirikiana na nchi ya Ujerumani
ambapo mradi huo unatekelezwa katika vijiji mbalimbali katika mikoa ya Mwanza,
Shinyanga, Kagera na Geita.
Naye
Mratibu wa Kamati ya Habari-Maandalizi ya kuelekea miaka 20/25 ya chuo cha SAUT
Padre Titus Ngapemba amesema kuwa Rais Mtaafu Benjamin Mkapa amekuwa mdau
muhimu katika sekta ya Elimu nchini katika ngazi mbalimbali za uongozi.
Padre
Ngapemba amesema kuwa Rais mstaafu Benjamin Mkapa amekuwa mdau muhimu katika
sekta ya elimu nchini na kwa namna ya pekee katika chuo cha SAUT, akiwa
madarakani alifanikisha ujenzi wa barabara ya kutoka jijini Mwanza kuingia chuoni
hapo ambapo ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami ulianza mwaka 2002 na
kuzinduliwa mwaka 2004.”“Mzee
Mkapa anakumbukwa sana kwa kuwa mwasisi wa utoaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa
wanafunzi wa vyuo vyote vya umma na binafsi. Uamuzi huu wa Mzee Mkapa wa
kuwapatia mikopo wanafunzi wa vyuo vikuu binafsi umesaidia Watanzania wengi
kusoma elimu ya juu. Kwa hili utakumbukwa Mzee Mkapa” alisisitiza Padre Ngapemba.
Padre
Ngapemba aliendelea kusema “Kwa mara ya kwanza mwaka 2005 Serikali ya Awamu ya
Tatu ilibadilisha Sera ya mikopo ya elimu ya juu na kuanza kutoa mikopo kwa
vyuo vikuu binafsi ikiwemo SAUT baada Makamu
wa Mkuu wa chuo wa wakati huo Padre Deogratius Rweyengeza kutoa ombi hilo
wakati wa mahafali ya kwanza mwaka 2001 tangu kipandishwe hadhi.”Chuo
Kikuu cha SAUT kinamilikiwa na kusimamiwa na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) kimeanzishwa
kwa mujibu wa sheria za nchi na kinafanya kazi chini ya Tume ya vyuo vikuu
Tanzania (TCU) kwa mujibu wa masharti ya vyuo vikuu sheria namba 7 ya mwaka
2005 ambapo awali kilikuwa kinajulikana kama Chuo cha Maendeleo ya Jamii
Nyegezi (NSTI) kilichoanzishwa tangu mwaka 1960 na wamisionari wa kanisa
katoliki ambao kwa sasa wanajulikana kama Wamisionari wa Afrika wakiwa chini ya
Askofu Mkuu Joseph Blomjous wa Jimbo Kuu
la Mwanza.
No comments :
Post a Comment