Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akimkabidhi
kadi ya Bima ya Afya Bw. Said Akili kutoka AMCOS ya Nyundo B iliyopo
Halmashauri ya Nanyamba kijiji cha Nyundo, wakati alipofanya ziara ya
kukagua utendaji kazi wa Mfuko wa Bima ya Afya Mkoa wa Mtwara na Lindi.
Picha ya pamoja ikiongozwa na
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt.
Faustine Ndugulile baada ya ziara ya kukagua utendaji kazi wa Mfuko wa
Bima ya Afya Mkoa wa Mtwara na Lindi, na muitikio wa Wakulima kujiunga
na Bima ya Afya Mkoa wa Mtwara na Lindi.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akikagua idadi
ya watu walioingizwa kwenye mfumo ili kupata kadi za Bima ya Afya,
wakati wa ziara ya kukagua utendaji kazi wa Mfuko wa Bima ya Afya Mkoa
wa Mtwara na Lindi, na muitikio wa Wakulima kujiunga na Bima ya Afya
Mkoa wa Mtwara na Lindi.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile akipitia
majarada ya wateja wanalioomba kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya, wakati
wa ziara ya kukagua utendaji kazi wa Mfuko wa Bima ya Afya Mkoa wa
Mtwara na Lindi, na muitikio wa Wakulima kujiunga na Bima ya Afya Mkoa
wa Mtwara na Lindi.
…………………………………………………………………
Na WAMJW – MTWARA
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile ameuagiza
uongozi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutatua changamoto ya
uchelewaji wa vitambulisho vya bima ya afya kwa wananchi.
Ameyasema hayo mapema leo wakati
alipofanya ziara ya kukagua hali ya utendaji kazi wa mfuko huo Mkoa wa
Mtwara, ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kukagua hali ya utoaji
huduma za Afya Mkoani hapo.
DKt. Ndugulile amesema kuwa NHIF
ni lazima ihakikishe inawahudumia vizuri wananchi wanaokuja kujiunga
katika mfuko huo, ikiwemo kuhakikisha ndani ya wiki mbili baada ya
kujaza fomu, wateja wapate kadi zao.
“Tuendelee kuwahudumia vizuri, na
kuhakikisha kwamba, ndani ya wiki mbili baada ya kujaza fomu na
kukamilisha taratibu, waweze kupata kadi zao” alisema DKt. Ndugulile
Pia, Dkt. Ndugulile amesema
Serikali imeridhishwa kwa kiasi kikubwa na mwitikio mzuri wa wananchi
kujiunga na Bima ya Ushirika jambo litalowasaidia kupata huduma za afya
katika vituo takribani 6,000 nchi nzima.
Aidha, Dkt. Ndugulile ameagiza
NHIF kuweka utaratibu wa kuwafuata na kuwapatia kadi za bima wateja
waliojiandikisha ili kuweka hamasa kwa wananchi wengine kujiunga na bima
ya afya na kuwapunguzia usumbufu.
Mbali ya hayo DKt. Ndugulile
ametoa onyo kwa watoa huduma za afya wanaofanya udanganyifu, na kuwataka
watoe huduma kwa kufata sheria, na kwa mujibu wa miongozo ya Wizara ya
Afya,
DKt. Ndugulile aliendelea kusema
kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za maboresho ya sheria ambazo
zitatoa adhabu kali kwa yeyote atakayehusika na udanganyifu wowote
utaopelekea hasara kwa Serikali.
Kwa upande mwingine DKt.
Ndugulile amewaagiza watoa huduma za afya kuhakikisha wanawasilisha
madai yao kwa NHIF kwa wakati, huku akisisitiza kuwa NHIF nayo inapaswa
kulipa madeni kwa wakati.
“Haipendezi wananchi wanahudumiwa
katika vituo vyetu vya kutolea huduma za Afya, na madai yanakaa zaidi
ya miezi miwili au mitatu, kwahiyo niombe watoa huduma waharakishe madai
yao, ili waweze kulipwa kwa wakati” alisema DKt. Ndugulile.
Nae Mkulima wa Korosho kutoka
Halmashauri ya Nanyamba kijiji cha Nyundo, amewataka wakulima kupitia
vyama vya Ushirika wajiunge na Bima ya Afya ili kuepuka gharama kubwa za
matibabu na ugonjwa hauchagui muda wa kuja.
“Nimehamasika kujiunga na bima ya
afya baada ya kuelewa kwamba ukulima una muda wa kupata pesa na una
muda wa kukosa, alafu homa haichagui muda,” alisema Bw. Said Akili.
Aidha Bw. Said Akili ameiomba
Serikali kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za afya hasa kwa Wateja
wanaotumia kadi za Bima ya Afya, jambo litalo wahamasisha wakulima wengi
zaidi kujiunga na mfuko huo.
No comments :
Post a Comment