MWENYEKITI
wa Kikundi cha Hamasa Afisi Kuu ya CCM Zanzibar Ndugu Shaaban Ali
Othman (wa pili kushoto) akizungumza mara baada ya kuwasili katika
Hospitali ya Wilaya ya Kaskazini ‘A’ Unguja, Daktari dhamana Tamim Hamad
Said (wa kwanza kushoto) pamoja na Katibu wa CCM Wilaya ya Kaskazini
‘A’ Haji Machano Juma(wa kwanza kulia) wakiwa katika hafla ya
makabidhiano ya vifaa tiba vilivyotolewa na kikundi cha hamasa.
MWENYEKITI
wa Kikundi cha Hamasa Afisi Kuu ya CCM Zanzibar Ndugu Shaaban Ali
Othman (kushoto) akimkabidhi Daktari dhamana Tamim Hamad Said(kulia) Friji mbili za kuhifadhi dawa za hospitali zilizotolewa na kikundi cha hamasa cha vijana wa Afisi Kuu CCM Zanzibar.
BAADHI
ya vijana wa kikundi cha hamasa cha Afisi Kuu ya CCM Zanzibar
wakisikiliza kwa makini nasaha za viongozi mbali mbali wa CCM, UVCCM na
Hospitali ya Wilaya Kivunge katika hafla ya makabidhiano ya Vifaa Tiba
iliyofanyika leo Tarehe 30/01/2019.(PICHA NA IS-HAKA OMAR
………………………….
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
VIJANA
mbali mbali nchini wameshauriwa kuendeleza utamaduni wa kujitolea
katika kuisaidia jamii katika masuala mbali mbali ya kiuchumi, kijamii,
kisiasa na kimaendeleo.
Rai
hiyo imetolewa leo na Mwenyekiti wa Kikundi cha Hamasa cha Afisi Kuu ya
CCM Zanzibar Ndugu Shaaban Ali Othman wakati akikabidhi Friji(Jokofu)
mbili zilizotolewa na
kikundi hicho na kukabidhi Uongozi wa Hospitali ya
Kivunge ya Wilaya Kaskazini ‘A’ Unguja.
Amesema
vifaa hivyo vimetolewa kwa ajili ya kusaidia uhifadhi wa vifaa tiba vya
hospitali hiyo hasa dawa za matumizi ya binadamu zinazohitaji hali ya
baridi muda wote.
Ameutaka
uongozi wa Hospitali hiyo kuvitunza na kuvitumia katika matumizi
yaliyokusudiwa ili vitoe huduma endelevu kwa wananchi mbali mbali
wanaofika hopitalini hapo kwa ajili ya matibabu.
Pamoja
na hayo amebainisha kuwa vifaa hivyo ni sehemu ya kuunga mkono juhudi
zinazofanywa na viongozi wa CCM ambao ni Mwenyekiti wa CCM Taifa
Dkt.John Pombe Magufuli pamoja na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar
Dk.Ali Mohamed Shein wanaotekeleza kwa kasi mipango ya maendeleo kwa maslahi ya wananchi wote.
Ameeleza
kwamba vijana nchini wana wajibu wa kutekeleza kwa vitendo masuala
mbali mbali ya kijamii kwa lengo la kuwasaidia wananchi wanaokabiliwa na
changamoto katika mazingira wanayoishi.
Katika
maelezo yake Mwenyekiti huyo Shaaban,amesema endapo vijana wa Zanzibar
wataweka mbele dhana ya uzalendo,umoja, mshikamano na kuelekezana mambo
mema ya kuisaidia jamii, itasaidia Zanzibar kuwa nchi bora zaidi duniani
iliyopiga hatua kubwa za kimaendeleo.
Awali
Katibu wa Kikundi hicho cha Hamasa, Suleiman Mohamed Rashid amefafanua
kuwa kikundi hicho kitaendelea kusaidia masuala mbali mbali ya kijamii
katika maeneo mbali mbali yaliyopo katika Wilaya zote za Unguja na
Pemba.
Amesema Chama Cha Mapinduzi kipo mstari wa mbele kushughulikia changamoto zinazoikabili jamii katika maeneo ya mijini na vijijini.
Akizungumza
mara baada ya kupokea vifaa hivyo Daktari Dhamana wa Hospitali hiyo
Tamim Hamad Said, amesema uongoizi wa hospitali hiyo umefurahi kupokea
vifaa hivyo kwani vilikuwa ni miongoni mwa mahitaji muhimu ya taasisi
hiyo.
Dr.Tamim
ameahidi kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa hasa kuhifadhi dawa na
vifaa mbalimbali vinavyotumika katika matibabu ili wananchi wapate
huduma bora za Afya.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ndugu Pandu
Salum Sungura amesema vijana wa mkoa huo wapo imara katika kuunga mkono
juhudi za vijana wenzao wa kikundi cha hamasa kutoka Afisi Kuu ya CCM
Zanzibar, kilichoonyesha mfano bora wa kutoa vifaa hivyo kwa hospitali
ili viwasaidie wananchi wa Mkoa huo.
Akizungumza
katika hafla hiyo kwa niaba ya Afisi Kuu ya CCM Zanzibar, Katibu
Msaidizi wa Taasisi hiyo Ndugu Khamis Salum Abdi amesema Chama Cha
Mapinduzi kinaendelea kusimamia na kutekeleza Ilani yake ya Mwaka
2015/2020 kwa ufanisi mkubwa kwa lengo la kumaliza kero zinazoikabili
jamii.
Amesema
suala la kuwapelekea wananchi maendeleo halina itikadi za kisiasa hivyo
kila mwananchi, kikundi pamoja na taasisi yoyote wana wajibu wa kutatua
changamoto za wananchi.
No comments :
Post a Comment