Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa
Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba akiwasilisha taarifa ya
Bajeti ya Ofisi yake kwa mwaka fedha 2017/2018 na mapendekezo ya Mapato
na Matumizi kwa mwaka 2018/19. Taarifa iliyowasilishwa mbele ya Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, hii leo Mjini Dodoma.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa
Rais Mhe. Kangi Lugola alifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Katiba
na Sheria mara baada ya kuwasilisha taarifa yao kwa Kamati hiyo hii leo
Mjini Dodoma.
Baadhi ya Watendaji wa Ofisi ya
Makamu wa Rais wakifuatilia majadiliano ya wajumbe wa kamati mara baada
ya kuwasilisha taarifa yao. Kutoka kushoto ni Bw. Richard Muyungi
Mkurugenzi wa Mazingira, Bi. Oigenia Mpanduji Mkurugenzi wa Sera na
Mipango na Bi. Butamo Phillip Naibu Katibu.
Pichani, Wajumbe wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Saed Ahmed Kubenea (kulia) na
Mhe. Joseph Kizito Mhagama wakifuatilia majadiliano katika Kamati yao
hii leo Mjini Dodoma.
………………
Imebainika kuwa nyongeza ya mambo
11 ya Muungano yamefanyika kwa kufuata taratibu za kisheria na kwa
mariadhano baina ya pande zote mbili za Muungano.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa
Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba
wakati akijibu hoja za Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya
Katiba na
Sheria hii leo mjini Dodoma.
Awali Mjumbe wa Kamati ya Bunge ya
Katiba na Sheria Mhe. Saed Ahmed Kubenea akichangia taarifa ya
iliyowasilishwa na Waziri Makamba juu ya Miradi inayotekelezwa Tanzania
Zanzibar na ile ya Utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi hiyo kwa mwaka wa
fedha 2017/18 na makadirio kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwa fungu 26 na
31, alihoji namna mambo ya Muungano yameongezeka kutoka 11 hadi kufika
22.
Akijibu hoja hiyo Waziri Makamba
alitumia fursa hiyo kufafanua kwa kina jinsi nyongeza ya mambo hayo
ilivyofanyika kwa kusema jambo la 12 liliongezwa mara baada ya kuvunjika
kwa Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki (East African Currency Body)
mwaka 1964. Hivyo Serikali zote mbili zilikubaliana masuala hayo
yashughulikiwe na Serikali ya Muungano.
Aidha, tarehe 11 Agosti 1967
yaliongezwa mambo ya Leseni za Viwanda na Takwimu (Jambo la 13) na Elimu
ya Juu (Jambo la 14) kupitia Sheria ya mabadiliko ya Muda ya mwaka
1965. Hata hivyo tarehe 22 Julai 1968 “Rasilimali ya mafuta, petroli na
gesi asilia” liliongezwa kwenye orodha ya Mambo ya Muungano na kuwa
jambo la 15.
Waziri Makamba amesema kuwa, Jambo
la 16 ambalo ni Baraza la Mitihani la Taifa liliongezwa tarehe 22
Novemba 1973, mara baada ya kuvunjika kwa Baraza la Mitihani la Afrika
Mashariki mwaka 1971. Pia, Usafiri wa Anga, Utafiti, Utabiri wa hali ya
hewa na Takwimu pia yaliongezwa kama mambo ya Muungano.
“Kwa mara ya kwanza Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ilifanyiwa marekebisho
mwaka 1979 ili kuanzisha Mahakama ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania mara baada ya kuvunjika kwa Mahakama ya Rufani ya iliyokuwa
Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1978. Marekebisho haya yalisababisha
orodha ya mambo ya Muungano kubadilika kwa kuongezeka suala la Mahakama
ya Rufani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania” Makamba alisisitiza.
Vilevile, mabadiliko ya nane
ya Katiba yaliyofanyika mwaka 1992 yalifuta mfumo wa chama kimoja cha
siasa na kurejesha mfumo wa vyama vingi vya siasa hali iliyosababisha
kuongezeka kwa jambo jingine la Muungano ambalo ni “Uandikishaji wa
Vyama vya Siasa”.
Waziri Makamba amesema kuwa
utaratibu uliotumika katika kuongeza idadi ya mambo ya Muungano ni
kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa kuzingatia
matakwa ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kama ilivyoelekezwa
katika Ibara ya 98(1) (b) ikisomwa pamoja na Orodha ya Pili kwenye
Nyongeza ya Pili ya Katiba ambayo imeweka masharti kuwa Mswada wa Sheria
kwa ajili ya kubadilisha orodha ya mambo ya Muungano lazima kuungwa
mkono na theluthi mbili ya Wabunge wote kutoka Tanzania Bara na theluthi
mbili ya Wabunge wote kutoka Tanzania Zanzibar.
Kamati ya Katiba na Sheria imepitia na kukubali Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2018/2019 kwa fungu 26 na 31.
No comments :
Post a Comment