Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe.
Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyeketi mbele) akiwa pamoja na baadhi ya
Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Jaji Kiongozi, Mtendaji Mkuu na
Ugeni kutoka Mahakama nchini Guatemala pindi Wageni hao walipomtembelea
Mhe. Jaji Mkuu ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Jaji Mkuu wa Tanzania
(pichani) akiwa katika mazungumzo na Wageni hao (hawapo pichani), katika
mazungumzo yao Mhe. Jaji Mkuu amefurahishwa na hatua iliyofikiwa na
Mahakama nchini Guatemala.
Baadhi ya Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani wakiwa katika kikao hicho.
Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Ferdinand Wambali akiongea jambo na Wageni hao, Mhe.
Wambali aliwaelezea Wageni hao juu ya Mfumo wa Mahakama nchini.
Jaji Mkuu aliyemaliza muda wake wa Mahakama nchini Guatemala, Mhe. Osvaldo Mendez akizungumza jambo.
Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Hussein Kattanga akizungumza jambo katika kikao hicho.
Mtaalamu kutoka Benki ya Dunia, Bw. Waleed Malik akiongea jambo katika kikao hicho.
Picha ya pamoja baada ya mazungumzo.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama
………………..
Na Mary Gwera
Katika mwendelezo wa
Utekelezaji wa Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (5)
(2015/2016-2019/2020), Mahakama ya Tanzania inaendelea na jitihada za
kupata uzoefu na ujuzi kutoka katika Mahakama mbalimbali duniani
zilizopiga hatua katika maboresho ya huduma ya utoaji haki kwa wananchi.
Haya yamejidhihirisha kufuatia
ugeni wa Maafisa wa Mahakama waliowasili kutoka nchini Guatemala kwa
mualiko wa Mahakama ya Tanzania kushiriki katika Hafla ya Siku ya Sheria
nchini, iliyofanyika Februari 01, 2018 vilevile Mahakama ya Tanzania
kupata maoni na ushauri zaidi wa jinsi ya kuendelea kuiboresha Mahakama
nchini kwa manufaa ya wananchi ambao ndio walengwa Wakuu.
Akiwatambulisha wageni hao kwa
Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania, Februari 1 katika Ofisi ya Mhe. Jaji Mkuu,
Mahakama ya Rufani Dar es Salaam, Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania,
Mhe. Hussein Kattanga alisema kuwa takribani miaka mitatu sasa baadhi ya
Maafisa wa Mahakama nchini walifanya ziara nchini Guatemala kwa lengo
la kujifunza ni kwa namna gani Mahakama nchini Guatemala imefanikiwa
katika utoaji wa huduma zake.
“Mhe. Jaji Mkuu,
tulichojifunza na tukaona ni vyema kuiga kutoka Guatemala ni pamoja na
huduma ya Mahakama inayotembea ‘mobile court’, ufanyaji kazi wa Mahakama
kwa masaa 24, kuweka mbele matumizi ya teknolojia katika shughuli zake
n.k, hivyo tumeona ni vyema pia kwa Mahakama nchini kupata
utaalamu/uzoefu kutoka kwa wenzetu jinsi ya kuweza kutekeleza haya,”
alisema Bw. Kattanga.
Mahakama ya Tanzania
imeonyesha nia ya dhati katika suala zima la maboresho, hivyo basi ujio
wa Wageni hawa ambao watakuwepo nchini kwa takribani siku 5, utawezesha
Wataalamu wa Mahakama kupata uzoefu na ujuzi zaidi wa namna gani
Mahakama zinazotembea zinavyofanya kazi n.k.
Aidha; kwa upande wake, Jaji
Mkuu aliyemaliza muda wake wa Mahakama nchini Guatemala, Mhe. Osvaldo
Mendez alisema kuwa Mahakama nchini humo amepiga hatua kubwa katika
suala zima la Matumizi ya TEHAMA hali ambayo imesaidia kurahisisha
utendaji na kutoa haki kwa wakati.
“Mahakama yetu pia inafanya
kazi masaa 24, na tunatoa huduma hii katika Miji mikubwa mitano nchini
Guatemala na tunafanya kwa ushirikiano na Wadau wetu wa Mahakama kama
Waendesha Mashitaka ‘Prosecutors’ n.k ili kufanikisha kumaliza mashauri
hayo kwa muda muafaka,” alieleza Mhe. Mendez.
Mpango Mkakati unaotekelezwa
na Mahakama umegawanyika katika nguzo kuu tatu ambazo ni Utawala na
Menejimenti bora ya Rasilimali, Upatikanaji na utoaji wa Haki kwa wakati
na kuimarisha imani ya Jamii na Ushirikishaji wa wadau katika shughuli
za Mahakama; nguzo zote zikilenga katika uboreshaji wa huduma za
Mahakama.
No comments :
Post a Comment