Thursday, November 2, 2017

Ijue hali halisi ya Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii


Mwenyekiti wa bodi  ya wadhamini ya mfuko wa NSSF Profesa Samweli Wangwe katika mkutano wa wadau wa NSSF AICC jijini Arusha

Na CHRISTIAN GAYA

Shirika la taifa la hifadhi ya jamii (NSSF) ilianza 1964 kama idara ya serikali, mpaka kufikia mwaka 1975 mfuko wa taifa wa akiba ya wafanyakazi (NPF) ulipitishwa kuwa Shirika la Umma. Mwaka 1997 ulibadilishwa kutoka Mfuko wa Akiba (NPF) na kuwa mfuko kamili wa hifadhi ya jamii (NSSF). NSSF huendeshwa kwa kuzingatia kanuni za...
bima ya jamii na huratibiwa chini ya wizara ya kazi na ajira.
Dira ya NSSF ni kuongoza katika utoaji huduma bora za mafao ya hifadhi ya jamii katika bara la Afrika ifikapo mwaka 2020. Majukumu makuu ya NSSF ni uandikishaji, ukusanyaji wa michango, uwekezaji na ulipaji mafao
Mwenyekiti wa bodi  ya wadhamini ya mfuko wa NSSF Profesa Samweli Wangwe wakati wa mkutano wa saba wa wadau wa NSSF kuanzia 18-20 Oktoba 2017 AICC Arusha anasema mpaka kufikia Juni 2016 mfuko uliweza kuandikisha waajiri wapya wapatao 2, 788, wakati kwa upande wa idadi ya waajiri mpaka kufikia juni 2016 ilifikia kuwa na waajiri  25,328. Mpaka juni 2016 jumla ya wanachama wapya wapatao 107, 764 waliandikishwa na mpaka kufikia mwezi Juni  2016 mfuko ulikuwa jumla ya wanachama wapatao 1,087,227.
"Mpaka kufikia Juni 2016 mfuko uliweza kukusanya michango ya wanachama ipatayo jumla ya milioni 724,079.00. Idadi ya wastaafu wanaopata pensheni mpaka kufikia Juni 2016/17 walikuwa 12,704. Kima cha chini cha pensheni kinachotolewa na NSSF ni Shs  100,000/- kwa mwezi wakati kima cha juu cha pensheni Shs 17,242,789/-. NSSF ni shirika pekee Tanzania linalopandisha viwango vya pensheni kulingana na mabadiliko ya kiuchumi na kwa mara ya mwisho pensheni iliongezwa  Agosti 2016" anafafanua mwenyekiti.
Anasema kwa upande wa mabadiliko ya viwango vya pensheni ya NSSF, kufikia Julai 1998 mpaka Juni 2000 kima cha chini cha pensheni kwa mwezi kilikuwa shilingi 14,000/ mpaka sasa kima cha chini cha pensheni kimefikia shilingi 100,000/- kwa mwezi.
"Tathmini ya kitaalam  ya mwaka 2009 ya ILO, na zile zilizofanywa mwaka 2010 na 2013 chini ya SSRA zinathibitisha ya kuwa NSSF ni shirika imara na lina uwezo wa kujiendesha na kulipa mafao ya wanachama wake  kwa miaka 6 bila kukusanya michango" profesa  anasema .
Profesa Wangwe anawahakikishia wanachama na wadau ya kwamba huduma ya matibabu hutolewa bure, kufaidika na mafao ya matibabu hakuathiri michango ya mwanachama kwa namna yoyote ile hata wakati wa kujitoa. Mafao mengine yote ya muda mfupi kama kuumia kazini na uzazi hauathiri pensheni ya mwanachama.
Anasema NSSF ni shirika lililo imara na lina thamani ya Shs 3.0 trillion kwa hesabu za kuishia Juni, 2016. Makadirio ya thamani ya shirika kwa mwaka 2017 ni  Shs trillioni 4, NSSF ina mtandao mpana wa ofisi 65 nchi nzima, Ofisi za Mikoa 27, Ofisi za Wilaya zipatazo 12, na vituo vipatazo ofisi 26. NSSF ni shirika imara linaweza kuendelea kulipa wanachama wake kwa muda wa miaka 6 bila makusanyo kwa mujibu wa ripoti ya tathmini ya mfuko uliofanyika mwaka 2013.
Anataja baaadhi ya changamoto zikiwemo juu ya baadhi ya wanachama kukimbilia kuchukua michango yao kabla ya kustaafu na mwisho wake huwa ni mateso  na msongo wa mawazo, waajiri kutolipa michango ya wafanyakazi wao kwa wakati, uelewa mdogo wa hifadhi ya jamii kwa watanzania na changamoto za uandikishaji wa sekta isiyo rasmi wakiwemo wakulima na wavuvi.
Mwandishi wa makala hii ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni, mshauri na mtaalamu wa masuala ya pensheni. Kwa maelezo zaidi gayagmc@yahoo.com unaweza kutembelea tovuti hakipensheni monitor online na hakipensheni blog   +255 655 13 13 41

No comments :

Post a Comment