Na Habari – MAELEZO
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Mwenyekiti wa Chama cha Siasa
cha Alliance for Democraytic Party – ADC, Hamad Rashid Mohamed amesema,
Vyama vya Upinzani vina nafasi kubwa katika kuishauri Serikali
inayoongozwa na Rais Dkt. Ali Mohamed Shein katika masuala ya maendeleo
visiwani Zanzibar.
Waziri Hamad Rashid Mohamed
amesema hayo alipohojiwa na Idara ya Habari (MAELEZO) leo kuhusiana na
mafanikio yaliyopatikana tangu mapinduzi ya Zanzibar yalipofanyika miaka
53 iliyopita. Amesema, Dkt. Shein amekuwa akivitaka Vyama vya Upindani
Visiwani Zanzibar kushiriki katika masuala ya maendeleo kwa njia
mbalimbali. Alitolea mfano, yeye kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri, Chama
chake cha ADC kwa kushirikiana na Wananchi wamejenga uwanja wa mpira wa
Gombani, Pemba kwa msaada kutoka Serikali ya Korea.
Waziri huyo pekee kutoka Chama cha
Upinzani amewabeza Wanasiasa wanaodai kuwa Dkt. Shein hatoi nafasi kwa
Vyama vingine katika kutoa michango yake katika masuala ya maendeleo.
“Mimi mwenyewe nimepewa dhamana ya Uwaziri kupitia chama changu cha ADC
na katika vikao tunavyokaa kila mtu anatoa mawazo yake kuhusiana na
masuala ya maendeleo ya Zanzibar na kama hoja unayotoa ni ya msingi
lazima itakubalika. Inapofikia suala la maendeleo Dkt. Shein haangalii
Chama, anaangalia maslahi ya Zanzibar kwanza.”
Akizungumizia maadhimisho ya miaka
53 ya Maapinduzi ya Zanzibar Waziri Hamad amesema, Wazanzibar na
Watanzania kwa ujumla wana kila sababu ya kuenzi Mapinduzi hayo ambayo
yalikuwa chachu cha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Muungano wetu
ulizingatia uwepo wa umoja kwani Serikali ya Kikoloni ilipandikiza mbegu
ya kubaguana hata Waafrika kwa Waafrika wenyewe.
Alifafanua kuwa, mapinduzi hayo
yaliifanya nchi iwe huru zaidi na Wananchi wake waishi kwa amani, umoja
na mshikamano. Chini ya uongozi wa Rais wa Awamu ya kwanza wa Zanzibar
marehemu Sheikh Abeid Aman Karume, Zanzibar ilipata maendeleo makubwa
ambapo zilijengwa nyumba bora za makazi za Wananchi, elimu ilitolewa
bure, huduma za afya, maji na hivyo kufuta kabisa aina zote za ubaguzi
uliokuwa umeota mizizi kabla ya mapinduzi.
Akijibu swali kuhusiana na
masimamo Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe
Magufuli juu ya mageuzi ya kuekelea kwenye uchumi wa Viwanda amesema,
kukua kwa uchumi ndio kigezo cha maendeleo katika Taifa lolote duniani.
“Rais anaposema anataka Taifa liondokane na umasikini inawezekana iwapo
tutakuwa na viwanda vidogo vidogo, vya kati na vikubwa.
Ameeleza kuwa, kutokana na viwanda
Watu watapata ajira, Wakulima watapata soko la uhakika la mazao
wanayozalisha na bidhaa zitakazozalishwa zitauzwa ndani na nje ya nchi
kwa kuwa zimeongezwa thamani. Hivyo katika kufikia malengo hayo lazima
tukubali mageuzi hayo na Wananchi lazima wafanye kazi.
Mwisho alimalizia kwa kutoa wito
wa Zanzibar lazima iwe salama na ibaki salama kwa kusisitiza nchi ni
lazima iwe na Amani, Mshikamano na Utulivu. Inapotetereka ni vema
kushirikisha viongozi wa dini na Wazee wenye busara ili kutanzua
matatizokuliko amani kutoweka. kwa Wazanzibar, kila mmoja ajiiulize
ameifanyia nini Zanzibar ili kuleta maendeleo.
Kwa wanasiasa alitoa wito kwa
kusema njia za kurekebisha makosa zipo kukubali kukaa chini na
kuzungumza kutoa lawana sio suluhisho. Vyama vya siasa vishiriki
kikamilifu katika utekelezaji wa maendeleo ya Zanzibar.
No comments :
Post a Comment