Tuesday, January 31, 2017

CUF YA PROFESA LIPUMBA YAJIBU MAPIGO KUHUSU RUZUKU WALIYOPEWA NA HAZINA


 
Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi (Taifa) wa Chama cha Wananchi (CUF), Thomas D.C Malima (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari Makao Makuu ya Chama hicho jijini Dar es Salaam leo kuhusu ruzuku ya chama hicho iliyopokelewa kupitia akaunti namba 2072300456 ya Benki ya NMB Tawi la Temeke. Kulia ni Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Mneke Jafar na Katibu Jumuiya ya Wanawake (JUKE), Salama Masoud.
Meza Kuu. Kutoka kulia ni Kamanda Mkuu, Athumani Hamadi,Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Mneke Jafar, Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi (Taifa) wa Chama cha Wananchi (CUF), Thomas D.C Malima, Katibu Jumuiya ya Wanawake (JUKE), Salama Masoud na Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, Masha Amour.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo.
Mkutano ukiendelea.

TAARIFA KWA UMMA 
 
The Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) chini ya Uongozi thabiti wa Mwenyekiti wake Mhe Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kinaishukuru na kuipongeza Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa kwa kukipatia Chama chetu Ruzuku yake inayopatikana kwa Mujibu wa Sheria ya vyama vya Siasa Namba 5 ya mwaka 1992.
 
Pamoja na Ruzuku ya CUF kuzuiwa kwa Muda wa miezi mine (4) kuanzia mwezi Septemba, 2016 hadi Desemba 2016 kutokana na sintofahamu ya uongozi wa Kitaifa wa CUF, Msajili hakuona haja ya kuendelea kuizuia wakati shughuli za chama zinafanyika kila siku. Kuendelea kuizuia Ruzuku halali ya chama ni kukizuia kufanya kazi zake halali za kisiasa ikiwa ni pamoja na kushiriki katika chaguzi mbali mbali za kiserikali zinazoendelea nchini. 
 
Waheshimiwa wanahabari, Baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa kupitia katiba ya CUF ya mwaka 1992, Toleo la 2014 alijiridhisha kuwa Mhe Profesa Ibrahim Haruna Lipumba ndiye Mwenyekiti halali wa CUF kwa kuwa mchakato wa kukamilisha kujiuzulu kwake haukukamilika kabla yeye kutengua barua yake ya kujiuzulu.
 
Mnamo Tarehe 23 Septemba 2016 , Msajili aliandika barua kwa Katibu Mkuu wa CUF kumjulisha msimamo na mwongozo wa wake  kuwa  “Mwenyekiti wa Taifa wa CUF ni  Mhe Profesa Ibrahim Haruna Lipumba”
 
Baada ya Katibu Mkuu kupokea barua hiyo aliamua kupinga Uamuzi huo wa Msajili wa Vyama vya Siasa uliotokana na Malalamiko ya wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa wapatao 324 kati ya 343 ambao walilalamikia uvunjifu wa Katiba ya CUF unaofanywa na Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad kwa Msajili wa Vyama vya Siasa.
 
Maaalim Seif na timu yake walienda mbali kwa “kuikimbia ofisi yake” iliyoko hapa Ofisi Kuu ya CUF Buguruni na kukimbilia Mafichoni kusikojulikana na kusababisha kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kiutendaji.  Hivyo, Mwenyekiti wa Taifa aliamua kufanya mabadiliko ya Kurugenzi za Chama kwa kumujibu wa ibara ya 91(1)(f) ya katiba ya CUF, nainukuu:
 
“Mwenyekiti wa Taifa atateua kutoka miongoni mwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa, wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa au wanachama wajasiri kuwa wakurugenzi na manaibu wakurugenzi wa Chama pamoja Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama baada ya kushauriana na Makamu Mwenyekiti na kufikisha uteuzi huo mbele ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa kuthibitishwa”. 
 
Kwa mujibu wa Ibara ya 95(3) ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992, Toleo la 2014, Nainukuu:-
  “Naibu Katibu Mkuuatakayemfuatia Katibu Mkuu kwa madaraka ni Yule anayetoka upande tofauti wa Jamhuri ya Muungano na upande anotoka Katibu Mkuu”.  Kwa kifungu hicho, Katibu Mkuu anaposhindwa kutekeleza majukumu yake kwa sababu yoyote ile, Naibu Katibu Mkuu Bara ndiye anakaimu Ukatibu Mkuu mpaka atakaporejea ofisini kuendelea na majukumu yake.
 
Hii inatokana ukweli wa kikatiba uliowekwa kwenye ibara ya 105 (1) ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992, Toleo la 2014, Nainukuu:-
  
 “Pale ambapo mwanachama yeyote wa Chama mwenye madaraka kwa mujibu wa masharti ya katiba hii, kwa sababu yeyote ile, hawezi kutekeleza kazi zake kwa muda, mwanachama anayemfuata kwa madaraka kwa mujibu wa katiba atakaimu nafasi yake”. 
 
Hivyo, kwa mujibu wa ibara hii na ile ya 95(3) Ni suala la kikatiba lisilo na shaka kwa Mheshimiwa Magdalena Sakaya (Mb) ambaye ndiye anayemfuata Katibu Mkuu kwa Madaraka kukaimu ofisi ya Katibu Mkuu mpaka atakaporejea ofisini kwake Buguruni. Kwa hiyo, Mhe Sakaya ataendelea kufanya majukumu yote ya Katibu Mkuu kwa mujibu wa Katiba ya CUF. Na Katibu Mkuu hapaswi kulalamika.
 
Kuhusu masuala ya fedha, Kwa mujibu wa kanuni ya jfedha ya mwaka 2014, ibara ya 22(2)(a) (B):-“Masuala yote ya fedha yanasimamiwa na Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi na ndiye Mshauri Mkuu wa Katibu Mkuu kuhusu Masuala ya Fedha”. 
 
Na kwa kuwa Katibu Mkuu ni Ofisi siyo mtu, anapokuwa hayupo ofisini Naibu Katibu Mkuu Bara atatekeleza majukumu yote ya ofisi ya Katibu Mkuu kama Kaimu Katibu Mkuu.  Ni aibu kwa Mwalimu Seif kulalamika wakati anaijua katiba ya CUF na anajua kuwa amekimbia ofisi mwenyewe ndiyo maana Mhe Sakaya anafanya kazi alizozikimbia kwa kushirikiana na wakurugenzi walioteuliwa na Mwenyekiti wa Taifa kwa mujibu wa Katiba.
 
Waheshimiwa wanahabari, Chama Chetu kimepokea sehemu ya malimbikizo ya ruzuku ya CUF Kiasi cha Tsh. 369,366,671/=. Tumepokea Ruzuku hiyo kupitia Akaunti namba 2072300456 ya The Civic United Front (CUF-Chama cha Wananchi)  NMB Tawi la Temeke. Hii siyo akaunti Mpya ya Chama kama inavyodaiwa Maalimu Seif na genge lake.
 
Akaunti hii ilifunguliwa zaidi ya miaka Kumi iliyopita na Katibu Mkuu kwa ajili ya kupokea na kutoa fedha za CUF kwa wilaya ya Temeke. Na kwa mujibu wa Kanuni ya Fedha ya CUF ya mwaka 2014, ibara ya 23(1)(f) Nainukuu: –
  
“Chama ngazi ya Taifa kinaweza kufungua akaunti tofauti au kubadili matumizi ya akaunti iliyopo kwa ajili ya kazi au shughuli maalum kadri itakavyoona inafaa. Akaunti hizo zilizofunguliwa utawekwa utaratibu maalum wa kuzihudumia”.
 
Kwa kuzingatia hali iliyopo, Tuliona kubadilisha matumizi ya Akaunti ya The Civic United Front (CUF-Chama cha Wananchi), Tawi la Temeke itumike kupokelea Ruzuku ya Chama toka serikalini ili iweze kufikia katika mikono salama kwa ajili ya uendeshaji wa Shughuli za Chama.
 
Waheshimiwa wandishi, Baada ya kuipokea Ruzuku hiyo, tayari tumeshaitumia katika harakati za Kiuchaguzi katika Chaguzi za marudio ya Udiwani katika kata 14 ambapo CUF imefanya vizuri sana katika kata tatu (3) ambazo ni Nkome (Geita), Malya (Kwimba) na Kijichi (Temeke). 
 
Waheshimiwa wandishi, Ikumbukwe kuwa Tangu  Mwalimu Seif na Genge lake wakimbie Ofisi Kuu Buguruni Tarehe 23 Septemba 2016, shughuli za chama zilikuwa zikiendelea kufanyika japokuwa hatukuwa tunapata ruzuku toka Serikalini. Wanachama wetu walikuwa na ari zaidi ya kukichangia chama ili kuendeleza harakati za ukobozi wa Haki sawa kwa Wote. Kwa mapenzi makubwa ya Chama chake Mheshimiwa Mwenyekiti wetu Profesa Ibrahim Haruna Lipumba alikuwa Msitari wa mbele kukisaidia chama kwa kujitolea na hata kukikopesha chama ili tutekeleze Majukumu ya ujenzi wa chama.
 
Waheshimiwa wanahabari, Hii si mara ya kwanza Mhe Profesa kukisaidia chama Chetu. Ipo mikataba kadhaa ambayo Mwenyekiti wetu amewahi kukikopesha chama fedha zake mwenyewe.
 
Waheshimiwa wandishi, Ni jambo la kusikitisha kuwa kwa takribani mwaka mmoja hasa baada ya Mhe Profesa Lipumba kuwa nje ya uenyekiti wa Taifa wa CUF, Wilaya zote za Tanzania Bara zilisitishiwa Ruzuku toka Ofisi kuu wakati wilaya zote za Zanzibar zikiwa zinaendelea kupokea ruzuku. Kwa kweli huu ni uonevu mkubwa kwa wanaCUF wa Tanzania Bara na huu ni mpango wa Makusudi wa Maalim Seif na genge lake.
 
Baada ya kupokea Ruzuku hiyo, Tumeamua kuzipelekea ruzuku Wilaya zote za Tanzania Bara alau ruzuku ya miezi mitatu mitatu kwa kila wilaya. Mpaka sasa tumeshatuma ruzuku katika wilaya 82 ambapo Tsh. 66,300,000/= zimetumika. 
 
Ikumbukwe kuwa Wilaya zinazotakiwa kupokea ruzuku ni wilaya zote zilizofanya uchaguzi wa ndani ya Chama ambapo Jumla ya wilaya 104 zina uongozi halali wa chama. Kwa mantiki hiyo, wilaya 22 bado hazijapewa Ruzuku kutokana na matatizo mbalimbali ikiwemo Akaunti zao kuwa dormat kwa muda mrefu, na nyingine kutowasilisha akaunti namba zao ofisini. 
 
Hivyo, tunatoa wito kwa viongozi wa Wilaya zote wa CUF kwenda benki kuangalia taarifa ya fedha ya akaunti zao kisha kutupa taarifa. Lakini pia ni wajibu wao kufanya matumizi ya fedha hizo kwa mujibu wa sheria za nchi na kanuni ya Fedha za CUF kwa kuwa hizo ni fedha za umma.
 
Waheshimiwa wandishi, tumesikitishwa na tamko la inayojiita Bodi ya wadhamini ya CUF eti fedha zimeibwa na wanazuia viongozi wa wilaya wasichukue fedha zilizoko kwenye akaunti zao. Kwa mujibu wa ibara ya 98(1) nainukuu:- 
 
“ Kutakuwa na Bodi ya wadhamini itakayoteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa mujibu wa sheria za nchi kwa kipindi cha miaka mitano (5) na mjumbe anaweza kuteuliwa tena baada ya muda kumalizika”. 
 
Ndugu wandishi, Bodi ya CUF iliteuliwa kwa mara ya mwisho Januari 2010, hivyo ilimaliza muda wake Januari 2015.  Haijawahi kuteuliwa tena na haijawahi kulipiwa Mchango wa kila mwaka RITA tangu 2013. Kutokana, sheria za nchi na katiba ya CUF, Bodi hiyo ni mfu kwa hiyo haina uwezo wa kushughulikia na kusimamia masuala yoyote ya fedha za CUF. How can a dead body talk about financial matters?. 
 
Wakiwa wanajua ukweli huo, bado wanakubali kutumika kwa maslahi ya Maalim Seif. Hii ni kuthibitisha kuwa “Mbwa mzee hafundishwi mbinu mpya za kuwinda”. Ni kweli Maalim Seif, Bashange na Katau wamezeeka, ni sawa mbwa wazee wasioweza kutumia mbinu mpya za kujijenga kwa wanachama wa CUF bali wanazidi kujifedhehesha. 
 
Ndevu zao ni ishara ya kupitwa na wakati. Ni bora watuachie vijana tujitanabahishe kwa mbinu za kisasa za kuiweka kweli ndani ya CUF na Watanzania kwa ujumla. Kama Maalim Seif alikuwa simba wa vita vya miaka 1980, kamwe hawezi kuwa simba wa vita ya 2016/2017. Huwezi kuwa Katibu Mkuu ambaye unapeleka Ruzuku Zanzibar kupitia Michango ya Wabunge lakini ukawa hutaki Wilaya za Tanzania Bara zipate Ruzuku. Huu ni ubaguzi uliokithiri na sisi hatutaukubali.
 
Tunaiomba ofisi ya Gavana wa Benki kuu kutupilia mbali ombi la Bodi ya wadhamini ya CUF isiyo halali kwa kuwa imepitwa na wakati na inakiuka hata katiba ya CUF ibara ya 98(1) na (2) inayotaka bodi iundwe na jumla ya wajumbe 9 ambapo 3 kati yao lazima wawe wanawake lakini bodi feki ya Mwalimu Seif ina wanaume watupu ndiyo maana wanailalamikia RITA eti wametoa siri za ufeki wao. 
 
Na kama wanahisi RITA wameghushi nyaraka, waende Polisi wakafungue mashitaka dhidi ya RITA, japokuwa nalo ni jambo gumu kwao maana wao ni Bodi mfu, hawana uwezo wa kushitaki wala kushitakiwa.
 
Waheshimiwa wanahabari, kwa sasa Maalim Seif anamlaumu kila mtu. Anamlaumu Jaji Mutungi kwa kusema ukweli, anawalaumu Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa kwa kuupinga udikiteta wake Mkutanoni, anamlaumu Gavana wa Benki, anailaumu RITA, anamlaumu Jaji Kihiyo, anamlaumu Rais Shein, anamlaumu Jecha, anamlaumu Profesa Lipumba eti anakuja kuzuia asipewe urais wa Zanzibar lakini cha ajabu hajilaumu mwenyewe kwa udikiteta wake ndani ya CUF na tamaa yake ya kupenda fedha za Lowasa kuliko utu na thamani yake kwa jamii.
 
Mwisho, tunamtaka Mwalimu Seif na Genge lake waende kwa amani watuachie CUF yetu. Hata Mapalala ailianzisha CUF lakini alipoonekana anaisaliti aliamua kuiacha CUF kwenye mikono salama. “Yeye sasa ni Simba mzee hawezi mawindo ya wakati huu”.
 
Imeandaliwa na;-
Thomas D.C Malima
Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi (Taifa)

No comments :

Post a Comment