Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi (Taifa) wa Chama cha Wananchi (CUF), Thomas
D.C Malima (katikati), akizungumza katika mkutano na waandishi wa
habari Makao Makuu ya Chama hicho jijini Dar es Salaam leo kuhusu ruzuku
ya chama hicho iliyopokelewa kupitia akaunti namba 2072300456 ya Benki
ya NMB Tawi la Temeke. Kulia ni Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Mneke
Jafar na Katibu Jumuiya ya Wanawake (JUKE), Salama Masoud.
Meza Kuu. Kutoka kulia ni Kamanda Mkuu, Athumani Hamadi,Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi, Mneke Jafar, Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi (Taifa) wa Chama cha Wananchi (CUF), Thomas D.C Malima, Katibu Jumuiya ya Wanawake (JUKE), Salama Masoud na Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa, Masha Amour.
Wanahabari wakichukua taarifa hiyo.
Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakichukua taarifa hiyo.
Mkutano ukiendelea. |
TAARIFA KWA UMMA
The
Civic United Front (CUF – Chama Cha Wananchi) chini ya Uongozi thabiti
wa Mwenyekiti wake Mhe Profesa Ibrahim Haruna Lipumba kinaishukuru na
kuipongeza Ofisi ya Msajili wa Vyama Vya Siasa kwa kukipatia Chama chetu
Ruzuku yake inayopatikana kwa Mujibu wa Sheria ya vyama vya Siasa Namba
5 ya mwaka 1992.
Pamoja
na Ruzuku ya CUF kuzuiwa kwa Muda wa miezi mine (4) kuanzia mwezi
Septemba, 2016 hadi Desemba 2016 kutokana na sintofahamu ya uongozi wa
Kitaifa wa CUF, Msajili hakuona haja ya kuendelea kuizuia wakati
shughuli za chama zinafanyika kila siku. Kuendelea kuizuia Ruzuku halali
ya chama ni kukizuia kufanya kazi zake halali za kisiasa ikiwa ni
pamoja na kushiriki katika chaguzi mbali mbali za kiserikali
zinazoendelea nchini.
Waheshimiwa
wanahabari, Baada ya Msajili wa Vyama vya Siasa kupitia katiba ya CUF
ya mwaka 1992, Toleo la 2014 alijiridhisha kuwa Mhe Profesa Ibrahim
Haruna Lipumba ndiye Mwenyekiti halali wa CUF kwa kuwa mchakato wa
kukamilisha kujiuzulu kwake haukukamilika kabla yeye kutengua barua yake
ya kujiuzulu.
Mnamo
Tarehe 23 Septemba 2016 , Msajili aliandika barua kwa Katibu Mkuu wa
CUF kumjulisha msimamo na mwongozo wa wake kuwa “Mwenyekiti wa Taifa
wa CUF ni Mhe Profesa Ibrahim Haruna Lipumba”
Baada
ya Katibu Mkuu kupokea barua hiyo aliamua kupinga Uamuzi huo wa Msajili
wa Vyama vya Siasa uliotokana na Malalamiko ya wajumbe wa Mkutano Mkuu
wa Taifa wapatao 324 kati ya 343 ambao walilalamikia uvunjifu wa Katiba
ya CUF unaofanywa na Katibu Mkuu Maalim Seif Sharif Hamad kwa Msajili wa
Vyama vya Siasa.
Maaalim
Seif na timu yake walienda mbali kwa “kuikimbia ofisi yake” iliyoko
hapa Ofisi Kuu ya CUF Buguruni na kukimbilia Mafichoni kusikojulikana na
kusababisha kushindwa kutekeleza majukumu yake ya kiutendaji. Hivyo,
Mwenyekiti wa Taifa aliamua kufanya mabadiliko ya Kurugenzi za Chama kwa
kumujibu wa ibara ya 91(1)(f) ya katiba ya CUF, nainukuu:
“Mwenyekiti
wa Taifa atateua kutoka miongoni mwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa,
wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa au wanachama wajasiri kuwa
wakurugenzi na manaibu wakurugenzi wa Chama pamoja Katibu wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama baada ya kushauriana na Makamu Mwenyekiti na kufikisha
uteuzi huo mbele ya Baraza Kuu la Uongozi la Taifa kwa kuthibitishwa”.
Kwa mujibu wa Ibara ya 95(3) ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992, Toleo la 2014, Nainukuu:-
“Naibu Katibu Mkuuatakayemfuatia Katibu Mkuu kwa madaraka ni Yule
anayetoka upande tofauti wa Jamhuri ya Muungano na upande anotoka Katibu
Mkuu”. Kwa kifungu hicho, Katibu Mkuu anaposhindwa kutekeleza majukumu
yake kwa sababu yoyote ile, Naibu Katibu Mkuu Bara ndiye anakaimu
Ukatibu Mkuu mpaka atakaporejea ofisini kuendelea na majukumu yake.
Hii inatokana ukweli wa kikatiba uliowekwa kwenye ibara ya 105 (1) ya Katiba ya CUF ya mwaka 1992, Toleo la 2014, Nainukuu:-
“Pale
ambapo mwanachama yeyote wa Chama mwenye madaraka kwa mujibu wa
masharti ya katiba hii, kwa sababu yeyote ile, hawezi kutekeleza kazi
zake kwa muda, mwanachama anayemfuata kwa madaraka kwa mujibu wa katiba
atakaimu nafasi yake”.
Hivyo,
kwa mujibu wa ibara hii na ile ya 95(3) Ni suala la kikatiba lisilo na
shaka kwa Mheshimiwa Magdalena Sakaya (Mb) ambaye ndiye anayemfuata
Katibu Mkuu kwa Madaraka kukaimu ofisi ya Katibu Mkuu mpaka atakaporejea
ofisini kwake Buguruni. Kwa hiyo, Mhe Sakaya ataendelea kufanya
majukumu yote ya Katibu Mkuu kwa mujibu wa Katiba ya CUF. Na Katibu Mkuu
hapaswi kulalamika.
Kuhusu
masuala ya fedha, Kwa mujibu wa kanuni ya jfedha ya mwaka 2014, ibara
ya 22(2)(a) (B):-“Masuala yote ya fedha yanasimamiwa na Mkurugenzi wa
Fedha na Uchumi na ndiye Mshauri Mkuu wa Katibu Mkuu kuhusu Masuala ya
Fedha”.
Na
kwa kuwa Katibu Mkuu ni Ofisi siyo mtu, anapokuwa hayupo ofisini Naibu
Katibu Mkuu Bara atatekeleza majukumu yote ya ofisi ya Katibu Mkuu kama
Kaimu Katibu Mkuu. Ni aibu kwa Mwalimu Seif kulalamika wakati anaijua
katiba ya CUF na anajua kuwa amekimbia ofisi mwenyewe ndiyo maana Mhe
Sakaya anafanya kazi alizozikimbia kwa kushirikiana na wakurugenzi
walioteuliwa na Mwenyekiti wa Taifa kwa mujibu wa Katiba.
Waheshimiwa
wanahabari, Chama Chetu kimepokea sehemu ya malimbikizo ya ruzuku ya
CUF Kiasi cha Tsh. 369,366,671/=. Tumepokea Ruzuku hiyo kupitia Akaunti
namba 2072300456 ya The Civic United Front (CUF-Chama cha Wananchi) NMB
Tawi la Temeke. Hii siyo akaunti Mpya ya Chama kama inavyodaiwa Maalimu
Seif na genge lake.
Akaunti
hii ilifunguliwa zaidi ya miaka Kumi iliyopita na Katibu Mkuu kwa ajili
ya kupokea na kutoa fedha za CUF kwa wilaya ya Temeke. Na kwa mujibu wa
Kanuni ya Fedha ya CUF ya mwaka 2014, ibara ya 23(1)(f) Nainukuu: –
“Chama
ngazi ya Taifa kinaweza kufungua akaunti tofauti au kubadili matumizi
ya akaunti iliyopo kwa ajili ya kazi au shughuli maalum kadri
itakavyoona inafaa. Akaunti hizo zilizofunguliwa utawekwa utaratibu
maalum wa kuzihudumia”.
Kwa
kuzingatia hali iliyopo, Tuliona kubadilisha matumizi ya Akaunti ya The
Civic United Front (CUF-Chama cha Wananchi), Tawi la Temeke itumike
kupokelea Ruzuku ya Chama toka serikalini ili iweze kufikia katika
mikono salama kwa ajili ya uendeshaji wa Shughuli za Chama.
Waheshimiwa
wandishi, Baada ya kuipokea Ruzuku hiyo, tayari tumeshaitumia katika
harakati za Kiuchaguzi katika Chaguzi za marudio ya Udiwani katika kata
14 ambapo CUF imefanya vizuri sana katika kata tatu (3) ambazo ni Nkome
(Geita), Malya (Kwimba) na Kijichi (Temeke).
Waheshimiwa
wandishi, Ikumbukwe kuwa Tangu Mwalimu Seif na Genge lake wakimbie
Ofisi Kuu Buguruni Tarehe 23 Septemba 2016, shughuli za chama zilikuwa
zikiendelea kufanyika japokuwa hatukuwa tunapata ruzuku toka Serikalini.
Wanachama wetu walikuwa na ari zaidi ya kukichangia chama ili
kuendeleza harakati za ukobozi wa Haki sawa kwa Wote. Kwa mapenzi
makubwa ya Chama chake Mheshimiwa Mwenyekiti wetu Profesa Ibrahim Haruna
Lipumba alikuwa Msitari wa mbele kukisaidia chama kwa kujitolea na hata
kukikopesha chama ili tutekeleze Majukumu ya ujenzi wa chama.
Waheshimiwa
wanahabari, Hii si mara ya kwanza Mhe Profesa kukisaidia chama Chetu.
Ipo mikataba kadhaa ambayo Mwenyekiti wetu amewahi kukikopesha chama
fedha zake mwenyewe.
Waheshimiwa
wandishi, Ni jambo la kusikitisha kuwa kwa takribani mwaka mmoja hasa
baada ya Mhe Profesa Lipumba kuwa nje ya uenyekiti wa Taifa wa CUF,
Wilaya zote za Tanzania Bara zilisitishiwa Ruzuku toka Ofisi kuu wakati
wilaya zote za Zanzibar zikiwa zinaendelea kupokea ruzuku. Kwa kweli huu
ni uonevu mkubwa kwa wanaCUF wa Tanzania Bara na huu ni mpango wa
Makusudi wa Maalim Seif na genge lake.
Baada
ya kupokea Ruzuku hiyo, Tumeamua kuzipelekea ruzuku Wilaya zote za
Tanzania Bara alau ruzuku ya miezi mitatu mitatu kwa kila wilaya. Mpaka
sasa tumeshatuma ruzuku katika wilaya 82 ambapo Tsh. 66,300,000/=
zimetumika.
Ikumbukwe
kuwa Wilaya zinazotakiwa kupokea ruzuku ni wilaya zote zilizofanya
uchaguzi wa ndani ya Chama ambapo Jumla ya wilaya 104 zina uongozi
halali wa chama. Kwa mantiki hiyo, wilaya 22 bado hazijapewa Ruzuku
kutokana na matatizo mbalimbali ikiwemo Akaunti zao kuwa dormat kwa muda
mrefu, na nyingine kutowasilisha akaunti namba zao ofisini.
Hivyo,
tunatoa wito kwa viongozi wa Wilaya zote wa CUF kwenda benki kuangalia
taarifa ya fedha ya akaunti zao kisha kutupa taarifa. Lakini pia ni
wajibu wao kufanya matumizi ya fedha hizo kwa mujibu wa sheria za nchi
na kanuni ya Fedha za CUF kwa kuwa hizo ni fedha za umma.
Waheshimiwa
wandishi, tumesikitishwa na tamko la inayojiita Bodi ya wadhamini ya
CUF eti fedha zimeibwa na wanazuia viongozi wa wilaya wasichukue fedha
zilizoko kwenye akaunti zao. Kwa mujibu wa ibara ya 98(1) nainukuu:-
“
Kutakuwa na Bodi ya wadhamini itakayoteuliwa na Baraza Kuu la Uongozi
la Taifa kwa mujibu wa sheria za nchi kwa kipindi cha miaka mitano (5)
na mjumbe anaweza kuteuliwa tena baada ya muda kumalizika”.
Ndugu
wandishi, Bodi ya CUF iliteuliwa kwa mara ya mwisho Januari 2010, hivyo
ilimaliza muda wake Januari 2015. Haijawahi kuteuliwa tena na
haijawahi kulipiwa Mchango wa kila mwaka RITA tangu 2013. Kutokana,
sheria za nchi na katiba ya CUF, Bodi hiyo ni mfu kwa hiyo haina uwezo
wa kushughulikia na kusimamia masuala yoyote ya fedha za CUF. How can a
dead body talk about financial matters?.
Wakiwa
wanajua ukweli huo, bado wanakubali kutumika kwa maslahi ya Maalim
Seif. Hii ni kuthibitisha kuwa “Mbwa mzee hafundishwi mbinu mpya za
kuwinda”. Ni kweli Maalim Seif, Bashange na Katau wamezeeka, ni sawa
mbwa wazee wasioweza kutumia mbinu mpya za kujijenga kwa wanachama wa
CUF bali wanazidi kujifedhehesha.
Ndevu
zao ni ishara ya kupitwa na wakati. Ni bora watuachie vijana
tujitanabahishe kwa mbinu za kisasa za kuiweka kweli ndani ya CUF na
Watanzania kwa ujumla. Kama Maalim Seif alikuwa simba wa vita vya miaka
1980, kamwe hawezi kuwa simba wa vita ya 2016/2017. Huwezi kuwa Katibu
Mkuu ambaye unapeleka Ruzuku Zanzibar kupitia Michango ya Wabunge lakini
ukawa hutaki Wilaya za Tanzania Bara zipate Ruzuku. Huu ni ubaguzi
uliokithiri na sisi hatutaukubali.
Tunaiomba
ofisi ya Gavana wa Benki kuu kutupilia mbali ombi la Bodi ya wadhamini
ya CUF isiyo halali kwa kuwa imepitwa na wakati na inakiuka hata katiba
ya CUF ibara ya 98(1) na (2) inayotaka bodi iundwe na jumla ya wajumbe 9
ambapo 3 kati yao lazima wawe wanawake lakini bodi feki ya Mwalimu Seif
ina wanaume watupu ndiyo maana wanailalamikia RITA eti wametoa siri za
ufeki wao.
Na
kama wanahisi RITA wameghushi nyaraka, waende Polisi wakafungue
mashitaka dhidi ya RITA, japokuwa nalo ni jambo gumu kwao maana wao ni
Bodi mfu, hawana uwezo wa kushitaki wala kushitakiwa.
Waheshimiwa
wanahabari, kwa sasa Maalim Seif anamlaumu kila mtu. Anamlaumu Jaji
Mutungi kwa kusema ukweli, anawalaumu Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa
kwa kuupinga udikiteta wake Mkutanoni, anamlaumu Gavana wa Benki,
anailaumu RITA, anamlaumu Jaji Kihiyo, anamlaumu Rais Shein, anamlaumu
Jecha, anamlaumu Profesa Lipumba eti anakuja kuzuia asipewe urais wa
Zanzibar lakini cha ajabu hajilaumu mwenyewe kwa udikiteta wake ndani ya
CUF na tamaa yake ya kupenda fedha za Lowasa kuliko utu na thamani yake
kwa jamii.
Mwisho,
tunamtaka Mwalimu Seif na Genge lake waende kwa amani watuachie CUF
yetu. Hata Mapalala ailianzisha CUF lakini alipoonekana anaisaliti
aliamua kuiacha CUF kwenye mikono salama. “Yeye sasa ni Simba mzee
hawezi mawindo ya wakati huu”.
Imeandaliwa na;-
Thomas D.C Malima
Mkurugenzi wa Fedha na Uchumi (Taifa)
No comments:
Post a Comment