Na Masanja Mabula –Pemba ..
ASKOFU
wa Kanisa Katoliki Zanzibar Augostino Shayo amewataka wazazi kuwekeza
katika sekta ya elimu kwa kuwasomesha watoto wao katika skuli ambazo
zinatoa elimu bora ili waweze kumudu ushindani wa soko la ajira.
Amesema
urithi pekee kwa mtoto ni elimu hivyo ni jukumu la kila mzazi
kuhakikisha mtoto wake anapata elimu bora ambayo itamwezesha kukabiliana
na changamoto za utandawazi zinazojitokeza siku hadi siku.
Askofu Shayo
ameyasema hayo kwenye Ibada ya kumpandisha daraja la ushemasi Fratel
Abeil Ignus Ndomba iliyo fanyika katika kanisa kuu Parokia ya Wete Pemba na kuhudhuriwa na waumini wa kanisa hilo Kisiwani hapa.
Amesema kutokana na kutambua umuhimu wa elimu katika maendeleo ya nchi na wananchi wake , kanisa
litaendelea kuiimarisha skuli yake iliyoko Tomondo Unguja ili iweze
kutoa elimu bora kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari .
Amesema
skuli hiyo imekuwa ikitoa wanafunzi bora kwani ina Vifaa vya kutosha ,
mazingira bora ya kufundishia , walimu bora na wanaoingia kazini kwa
wakati .
“Ni lazima kila mzazi kupima ubora wa elimu wanayopewa watoto wao na kuacha kuridhika na elimu inayotolewa bure kwani inakabiliwa na changamoto mbali mbali ”alisema .
Aidha
amezidi kueleza kuwa skuli inayomilikiwa na kanisa hilo ya Tomondo
imejipatia umaarufu kwani imezingatia viwango na idadi ya wanafunzi
katika darasa moja , tofauti na skuli zinazotoa elimu bure ambazo
zinakuwa na msongamano mkubwa wa wanafunzi katika darasa moja.
Naye mkurugenzi wa wito kanisa katoliki jimbo la Zanzibar padri John Pita
Mfoi aliwataka wazazi kusimamia pamoja na kufuatilia maendeleo ya
watoto wao skuli ili kujua mwenendo wao na kusaidia kutatua changamoto za kielimu zinazowakabili.
Amesema
elimu ndiyo njia pekee inayoweza kumkomboa mwananchi kutoka katika
wimbi la umaskini wa kipato , hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanajenga
utamaduni wa kuwa karibu na walimu , kamati ya skuli na wadau wengine wa
elimu .
“Ni
vyema wazazi na walezi kujenga utamaduni wa kufuatilia maendeleo ya
watoto wao skuli kwani elimu ndiyo ambayo inaweza kumkomboa mwananchi
kutoka katika wimbi la umaskini ”alieleza.
Katika
nasaha zake , paroko wa Parokia ya Wete , Padri Beatusi Babu amemtaka
Shemasi Abeil kufanya kazi kwa uhuru na kuyakemea matendo maovu bila ya
woga ili aweze kuitumikia vyema jamii .
No comments :
Post a Comment