Na Eleuteri Mangi-MAELEZO, Dodoma.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli
ametimiza siku ya 365 Watanzania wameona, kushuhudia utendaji na
mwelekeo wake wa kuiongoza Serikali ya Awamu ya Tano kwa mafanikio.
Kauli hiyo imetolewa na leo
Bungeni mjini Dodoma na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Kassim Majaliwa Majaliwa kabla ya kuanza kujibu maswali ya papo kwa papo
ambayo huulizwa na Wabunge kwa Waziri Mkuu kwa kumwomba Naibu Spika
Dkt. Tulia Akson kuridhia kuwakumbusha Watanzania kuhusu muda wa uongozi
tangu Rais Dkt. Magufuli aingie madarakani.
“Jukumu letu, ni kumwombea Mhe.
Rais aweze kuendelea vizuri na kazi ya kuiongoza nchi yetu na wananchi
wote tuungane pamoja kila moja kwa dhehebu lake kuweza kuiombea Serikali
hii ili iweze kupata mafanikio makubwa” amesema Waziri Mkuu.
Akijibu swali lililoulizwa na
Munde Tambwe Abdallah (Mb) juu ya mifumo ya Serikali ya kupeleka fedha
za maendeleo katika halmashauri kwa kuzingatia mifumo, sheria, taratibu
na miongozo ambayo husababisha halmashauri kuchelewa kupelekewa fedha
mara baada ya bajeti kukamilika, Waziri Mkuu amesema kuwa baada ya Bunge
la Bajeti kukamilisha kazi yake, Serikali inawajibika kutekeleza
maamuzi ya Bunge kwa kupeleka fedha zilizopangwa kulingana na bajeti
hiyo.
Akifafanua suala hilo, Waziri
Mkuu amesema kuwa baada ya Bunge kuridhia na kutoa mamlaka ya matumizi
ya fedha, Serikali ya Awamu ta Tano ilianza na majukumu muhimu ya
kujiridhisha na uwepo wa mifumo sahihi ya makusanyo ya mapato na
matumizi yake, kupeleka watumishi watakaosimamia shughuli za usimamizi
wa ukusanyaji wa mapato na matumizi yake kwenye halmashauri zote nchini
na kuratibu na kutathmini miradi yote iliyokuwa imeanza halafu
kutokuendelezwa pamoja na miradi mipya ili kutambua pamoja na thamani
zake.
Baada ya kujiridhisha juu ya
mambo hayo, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali imeanza kupeleka kwenye
halmashauri zote nchini ambapo kufikia mwezi Oktoba kwa mujibu wa
Hazina, jumla ya zaidi ya shilingi Bilioni 177 za miradi ya maendeleo
zimepelekwa kwenye halmashauri.
Kwa kudhihirisha masuala hayo,
Waziri Mkuu amesema kuwa hivi karibuni vyombo vya habari ikiwemo
magazeti kwa wiki tatu yameanza kutoa matangazo ya zabuni kutoka kwenye
halmashauri mbalimbali juu ya miradi iliyokuwepo na ile inayoendelea na
miradi mipya imeanza kutengewa fedha na ambayo imeanza kutangaza kwa
ajili ya kuetekeleza miradi hiyo.
Aidha, Waziri Mkuu
amewahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kupeleka fedha kwenye
halmashauri kwa ajili ya shughuli za maendeleo na kuzisisitiza
halmashauri ziendelee kukusanya mapato ya ndani ili kuongezea bajeti
fedha za Serikali zinazopelekwa na kuongeza kuwa ukusanyaji wa mapato
hayo uwe wa mfumo wa kielekroniki ili kudhibiti mapato yanayopatikana.
Akijibu swali la nyongeza juu
halmashauri zote kutumia mashine za kielekroniki, Waziri Mkuu amewaagiza
Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Watendaji wote wa Halmashauri
wakiwemo Wakurugenzi kuhakikisha kila eneo la makusanyo vifaa vya
kielekriniki vinatumika na matumizi ya vifaa hivyo yaendelee ili
kuboresha ukusanyaji wa mapato nchini.
Zaidi ya hayo Waziri Mkuu
ameendelea kusisitiza kuwa matumizi sahihi ya fedha ambazo zinapelekwa
kwenye halmashauri ni lazima zitumike kulingana na malengo
yaliyokusidiwa katika kutekeleza miradi iliyoandaliwa kwenye halmashauri
na kuwasihi Wabunge wakiwa wajumbe wa baraza la madiwani katika
halmashauri zao waendelee kusimamia na kufuatilia matumizi ya fedha
zinazopelekwa ili zitekeleze miradi hiyo kikamilifu.
Kuhusu swali la Mbunge wa Ukonga
Mwita Witara juu ya Mfuko wa Jimbo, Waziri Mkuu Majaliwa amemhakikishia
Mbunge huyo kuwa Serikali haijafilisika, na kusisitiza kuwa suala la
Mfuko wa Jimbo bado unatambulika na fedha zitapelekwa kwenye majimbo na
wabunge wote watajulishwa ni kiasi gani cha fedha kimepelekwa kwenye
majimbo yao ili sheria ziendelee kutumika na kutekelezwa na Mbunge akiwa
mwenyekiti wa Mfuko huo anatakiwa kuendelee kuratibu fedha hizo.
Waziri Mkuu amesema kuwa fedha za
Mfuko wa Jimbo ni miongoni mwa fedha inayotengwa kwenye Bajeti na
kukumbusha kuwa tangu Bunge la bajeti limalize kazi yake miezi mitatu,
bado kuna miezi saba ya kutekeleza bajeti hiyo ambapo fedha hizo
zitapelekwa kwenye miradi iliyokusudiwa kwenye majimbo mbalimbali
nchini.
Kwa upande wa Wafanyabishara
kunyanyaswa na Maafisa wa Kodi nchini swali lililoulizwa na Ritha Kabati
Mbunge wa Iringoa, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali inaheshimu na
kuwathamini wafanyabiashara wote nchini, wawekezaji, wadau na walipa
kodi wote wa ndani ya nchi kwa kuzingatia kuwa maendeleo katika nchi
yataletwa na sekta ya wafanyabiashara na wawekezaji wakiwa ndio walipa
kodi wakubwa nchini.
Kuhusu suala la nidhamu ya
wafanyakazi wa Mamlaka ya Mpato Tanzania (TRA), Waziri Mkuu amewaonya
wafanyakazi hao kuwa watumie lugha nzuri na busara wanapokwenda kutimiza
majukumu yao kwa kutumia sheria na kanuni na taratibu za kufanya kazi
yao.
Kwa upande wa wafanyabiashara,
Wairi Mkuu amewataka wafanyabishara hao kutoa taarifa juu ya jambo
linalowakwaza kwenye vyombo vya usalama ikiwemo kitengo cha nidhamu
kilichopo TRA ili kutafuta dawa sahihi juu ya wafanyakazi ambao
hawaendani na nidhamu ya watumishi wa umma.
Swali lingine lililoelekezwa kwa
Waziri Mkuu liliulizwa na mbunge wa jimbo la Liwale Zuberi Kuchauka
ambalo lilihusu uwepo wa Sera ya wafanyakazi kutoka nje ya nchi (TX)
kupitia makampuni mbalimbali, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Sera
hiyo bado ipo na Serikali inaisimamia kwa kuzingatia msingi wa kuwapa
muda mfupi wataalamu hao wenye ufundi maalumu katika sekta ya kazi ili
kujenga wigo mpana kwa Watanzania kupata ajira na kuweza kusimamia
maeneo yanayohitaji utaalamu.
“Tumetoa nafasi kwa watumishi wa
nchi za nje kuja nchini Tanzania kufanya kazi ambazo hapa ndani sisi
tunakosa utaalamu ndio tunafuata msingi huo, tunawapa miaka miwili ya
mwanzo, tukiamini Watanzania waambata watakuwa wamejifunza utaalamu ule
kwa miaka miwili hadi mitano ambapo baada ya hapo wataalamu wa nje ya
nchi wanaweza kuondoka, tunamini Watanzania watakuwa wamepata taaluma
hiyo na kusimamia sekta ya kazi” amesisitiza Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amewahakikishia
Watanzania kuwa makakati wa Serikali wa kufugua milango ya ajira katika
sekta zote ikiwemo utalamu, utaratibu huo utaendelea kusimamiwa wa
kupokea utaalamu kutoka nje ambao Tanzania haupo ili kutoa nafasi kwa
Wanzania kujifunza.
Kuhusu swali la ruzuku ya
pembejeo kwenye sekta ya kilimo kuwafikia wakulima kwa wakati ambalo
liliulizwa na Mbunge wa Mbeya vijijini Oran Njeza, Waziri Mkuu amesema
kuwa Serikali kupitia Wizara ya Kilimo imeweka utaratibu wa kusambaza
pembejeo nchini kwa kutumia Kampuni ijulikanayo Tanzania Fertilizer
Cooperation ili kupeleka mbolea kwa wakulima wakati taasisi nyingine
zimepewa kazi kusambaza pembejeo nyingine.
Ili kuhakikisha wananchi wanapata
mbolea na pembejeo nyingine kwa wakati, Waziri Mkuu amesema kuwa
Serikali imetoa fedhakwa ajili ya kununua pembejeo kwa kampuni hizo na
zitatumia mawakala waliopo hadi ngazi za vijiji na kuhakikisha pembejeo
hizo zinzwafikia walengwa zinazohitajika katika musimu wa kilimo
unapoanza.
Maswali ya papo kwa papo ya
Wabunge ambayo huelekezwa kwa Waziri Mkuu yapo kwenye utaratibu
kulingana na ratiba ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kila
siku ya Alhamisi ili kutoa majibu ya maswali hayo yanayoelekezwa kwenye
sekta mbalimbali nchini kwa musatakabali wa kuboresha maisha ya
Watanzania na taifa kwa ujumla ili kuwa na maendeleo endelevu ifikapo
mwaka 2025 kulingana na Dira ya Maendeleo ya Taifa.
No comments :
Post a Comment