Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Joel Malongo akizungumza na vongozi wa Mfuko Kichocheo wa SAGCOT, wawakilishi
wa vyama vya wakulima na wawakilishi wa wabia wa Maendeleo jijini Dar
es Salaam leo wakati wa kusaini mikataba ya makubaliano ya ufadhili wa
Fedha katika mfuko wa Kichocheo wa SAGCOT pamoja na kampuni zilizoibuka
kidedea kwenye kinyang’anyiro cha kuomba ufadhili kutoka kwenye mfuko.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Joel Malongo (Mwenye tai nyekundu waliosimama) akishuhudia wawakilishi wa vyama vya wakulima wakisaini
mikataba ya makubaliano ya ufadhili wa Fedha katika mfuko wa Kichocheo
wa SAGCOT pamoja na kampuni zilizoibuka kidedea kwenye kinyang’anyiro
cha kuomba ufadhili kutoka kwenye mfuko huo jijini Dar es Salaam leo.
wanaosaini hati hizo kutoka kulia ni Mkulima wa miwa Dk George Mlingwa
Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Germao Cane Estate, Mwenyekiti wa
Bodi ya Mfuko Kichocheo wa SAGCOT, Ami Mpungwe, Roy Omulo kutoka kiwanda
cha Maziwa cha Asas Dairies Iringa na Lutengano Peter Mwenyekiti wa
MUWAMARU Tukuyu mkoani Mbeya.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Mfuko Kichocheo wa SAGCOT, Ami Mpungwe akizungumza katika
hafla fupi ya kusaini makubaliano hayo amesema kuwa Mfuko wa SAGCOT
wamesaini mikataba kwaajili ya kibiashara kwanzia mtaji kati ya Dola Za
Kimarekani milioni 50 hadi 100 zitakuwa zikitolewa kwa miradi kupitia
madirisha ya Matching Grant Fund(MGF) ambao utakuwa ukitatua changamoto
za wakulima na masoko yao.
Baadhi ya viongozi hao wakiwa katika mkutano huo leo
Baadhi ya wafadhili wakiwa katika mkutano huo
Washiriki wa mkutano huo kutoka makampuni mbalimbali na serikali
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Mhandisi Joel Malongo akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko Kichocheo wa SAGCOT, Ami Mpungwe wakati wa mkutano huo.
Waziri mwijage azindua siku ya viwango barani Afrika
Arusha
Waziri wa Viwanda Biashara na
uwekezaji Charles Mwijage amelitaka shirika la viwango Tanzania TBS
pamoja na shirika la ushindani wa haki kuhakisha ifikapo July moja
wanamaliza bidhaa zote bandia na zilizo chini ya viwango na wasipo
fanya hivyo ajira zao zitafutwa mara na bidhaa hizo kuteketezwa.
Tamko hilo amelitoa waziri
Charles Mwijage leo hii wakati alipokuwa anatembelea kujionea bidhaa
zinazozalishwa hapa nchini na kusibitishwa ubora wake katika siku ya
viwango afrika ambapo kwa upande wa kampuni ya cement ya Dangote afisa
mkuu masoko Joel Laizer amemhakishi a waziri ubora wa cement
zinazozalishwa na kampuni hiyo.
Wakati huo huo kampuni ya Azania
pamoja na Azam kwa kupitia kwa maofisa wao akiwemo Maofisa masoko afisa
mkuu wa masoko wa AZANIA Naifa Abubakari pamoja Ibrahimu Masome wa
AZAM wamemuhakikishia waziri wa viwanda biashara na uwekezaji kuwa wao
wamejipanga vizuri kuhakisha wanatoa bidhaa zinazokidhi viwango bora na
zenye ushindani na masoko kote duniani
Aidha kwa upande wao kampuni ya
kuzalisha Bodi za magari ya kitalii pamoja na vyuma vya kujengea Maghala
ya viwanda afisa biashara Mohan Krishan amemwambia waziri kuwa wao kama
kampuni ya HANSPAUL wataakikisha wanatengeneza bidhaa bora zenye bei
nafuu.
Pombe za asili zatamba soko la vinywaji nchini
Wafanyakazi wa DarBrew wakionyesha kinywaji cha Chibuku kwenye chupa ndogo wakati wa kuizindua hivi karibuni
Kikosi
kazi cha menejimenti na wafanyakazi wa DarBrew wakiwa katika picha ya
pamoja wakati wa kusherehekea kupata tuzo ya SABMiller ya kuendeleza
vinywaji vya asili nchini hivi karibuni.
…………………………………………………………………………………………………………..
-TBL Group yajipanga kuziboresha kulinda afya za watumiaji na kuchangia pato la Taifa
Licha ya
kuwepo na viwanda mbalimbali vya kutengeneza bia na vinywaji vingine vya
kisasa ikiwemo uingizwaji wa vinywaji hivyo kutoka nje ya nchi bado
idadi kubwa ya watanzania wanatumia pombe za asili na sababu kubwa
inabainishwa kuwa hali hiyo inatokana na vinywaji vya kisasa kuuzwa kwa
bei ya juu.
Utafiti
uliofanywa na taasisi ya CanBack kuhusiana na matumizi ya pombe za
asili nchini umebainisha kuwa matumizi ya pombe za asili nchini ni
asilimia 50% ambapo kati ya asilimia hizo vinywaji vya asili
vinavyototengenezwa kisasa viwandani vinatawala kwa asilimia 8% .
Sababu kubwa
ya watumiaji wa vinywaji vya asili ambavyo vingi vinatengenezwa kwenye
mazingira yasiyo salama na vinaendelea kuleta athari kwenye jamii ni
kutokana na bei kubwa ya bia ,wine na vinywaji vinginevyo vya kisasa
ambapo idadi kubwa ya wananchi hawana uwezo wa kumudu kuvinunua na
kuvitumia.
Akitoa
ripoti ya utendaji wa kampuni katika kipindi cha mwaka 2015 na mikakati
yake ya mbele katika kipindi cha mwaka 2016/17 kwa waandishi wa habari
hivi karibuni,Mkurugenzi Mkuu wa TBL Group,Roberto Jarrin alisema kuwa
kampuni yake tayari imeanza kutekeleza mkakati wa kuboresha vinywaji
vya asili na kuhakikisha vinaingia katika mfumo rasmi unaotambulika kwa
kuviwezesha kuchangia pato la taifa kwa njia ya kodi ikiwemo kulinda
afya za wananchi.
Jarrin
alibainisha kuwa kampuni ya DarBrew imeweza kuleta mapinduzi ya uuzaji
wa pombe za asili nchini kwa kuwawezesha watumiaji kupata kinywaji cha
Chibuku na Nzagamba kikiwa kimefungwa kwa viwango mbalimbali na katika
mazingira ya usafi yanayolinda afya za watumiaji na hivi sasa imekuja na
mkakati wa kuwainua akina mama kimapato kupitia kuuza bidhaa zake
unaojulikana kama Chibuku Mamas ambao hadi kufikia sasa wanawake wapatao
130 wameishajiunga na mpango huu.
Alisema kuwa
akina mama wakiendelea kujiunga na mpango huu wataweza kujikwamua
kimapato na kulinda afya zao na wanywaji pia kupunguza uharibifu wa
mazingira kwa kutumia kuni kwa ajili ya kupikia pombe za asili ambazo
zimekuwa zikiuzwa katika vilabu mbalimbali.”Tunawasihi watumiaji wa
vinywaji vya asili kujenga mazoea ya kutumia vinywaji vyenye ubora na
vilivyotengenezwa kwenye mazingira mazuri kwa ajili ya kulinda afya zao”.Alisema
Katika
kuhakikisha watumiaji wanamudu vinywaji vya asili vya Chibuku na
Nzagamba alisema kampuni imeanza kusambaza vinywaji hivi vikiwa kwenye
ujazo wa chupa za ukubwa wa aina mbalimbali ili wanywaji wote waweze
kuvipata kulingana na vipato vyao.
Kuhusu
mtazamo wake wa hali ya biashara ya kampuni kwa sasa Jarrin alisema
sekta ya uuzaji wa vinywaji inakabiliwa na changamoto mbalimbali
mojawapo ni bei kubwa ya bia ambayo watumiaji wake wengi wanashindwa
kuimudu,kuwepo na vinywaji visivyo katika mfumo rasmi wa ushindani
katika soko,kukosekana kwa motisha katika uzalishaji wa malighafi za
kutengeneza vinywaji nchini kwa kuwa zinatozwa kodi kubwa ya zuio kuliko
malighafi zinazotolewa nje ya nchi.
Alisema
baadhi ya mambo yanayostahili kufanyika katika uboreshaji wa sekta ili
iendelee kuchangia pato la taifa ni kupunguza kodi za malighafi
zinazozalishwa nchini kama kimea kinachotumika kutengeneza bia pia
kulasimisha pombe za asili ziende sambamba na vinywaji vya sili
vinavyolipiwa kodi na kuhakikisha vinywaji vya asili vinapatikana
katika mazingira ya usafi “Pamoja na changamoto nyingi zilizopo
katika sekta hii tunaendelea kukabiliana nazo na tumedhihirisha uwezo
wetu kwa kuwa na viwanda vyenye ubora wa hali ya juu nchini
Tanzania”Alisema Jarrin
Wakala ya serikali mtandao kufanya ziara ya kutembelea taasisi za serikali.
Meneja
wa Habari, Elimu na Mawasiliano toka Wakala wa Serikali Mtandao Bi
Suzan Mshakangoto akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo
pichani) kuhusu mpango wa taasisi yake kutembelea wateja wake ambao ni
taasisi za Umma ikiwa ni sehemu ya maadhimishi ya wiki ya Utumishi wa
Umma.
Picha na Eliphace Marwa – Maelezo
……………………………………………………………………………………
Na Eliphace Marwa – Maelezo
Wakala wa Serikali Mtandao (eGA)
imeandaa utaratibu wa kutembelea wateja wake ambao ni taasisi za umma
ili kusikiliza na kutatua changamoto zinazo tokana na huduma
wanazotoa,huduma hizo ni pamoja na mfumo wa barua pepe unaorahisisha
mawasiliano serikalini.
Hayo yamesemwa na Meneja wa
Habari, Elimu na Mawasiliano wataasisi hiyo Bi Suzan Mshakangoto,
alipokuwa akiongea na waandishi wa habari ofisini kwake mapema hii leo
jijini Dar es Salam na kutaja baadhi ya taasisi 34 zitakazoanza
kutembelewa kuanzia tarehe 22 Juni hadi Juni 23.
Alizitaja baadhi ya taasisi hizo
kuwa ni pamoja na Ofisi ya Raisi Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge,Kazi, vijana, Ajira na
Walemavu, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo na Makazi, Wizara ya
Elimu,Sayansi Teknolojia na Ufundi, Wizara ya Habari,utamaduni Sanaa na
Michezo, Wizara ya kilimo, Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Mambo ya Nje
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa.
Aidha aliongeza kuwa huduma
nyingine zinazotolewa na wakala wa serikali ni pamoja na uhifadhi wa
mifumo ya tovuti za serikalini, utoaji huduma za simu za mikononi,
Uratibu wa mitandao serikalini, Ugawaji wa masafa ya internet, huduma
za ujumbe mfupi wa maandishi (sms) pamoja na utengenezaji wa mifumo ya
tovuti na usajili anuani za tovuti.
Hiyo ni kutimiza Agizo la Waziri
wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mh.Angela Kairuki
la kutaka kila Wizara, wakala na Taasisi za Serikali katika kipindi cha
Wiki ya Utumishi wa Umma kukutana na wateja wao na kusikiliza kero
walizonazo ili kuweza kuzipatia ufumbuzi, aidha kauli mbiu ya mwaka huu
ni, “Uongozi wa Umma kwa Ukuaji jumuishi kuelekea katika Afrika
tunayoitaka”.
Kila taasisi itatembelewa na
wataalam wawili wa wakala wa serikali watakao sikiliza maoni na kutoa
msaada wa kiufundi na ushauri wa kitaalamu katika kutatua changamoto
mbali mbali zinazojitokeza juu ya huduma mbali mbali zinazotolewa na
wakala.
Mkurugenzi Muhimbili Akutana na Madaktari, Aongeza Posho
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru LEO
amekutana na madaktari bingwa wa hospitali hiyo kwa ajili ya
kuwasikiliza na kujibu kero mbalimbali.
Baadhi ya madaktari bingwa wakimsikiliza Profesa Museru baada ya kukutana nao LEO kwenye ukumbi wa CPL katika hospitali hiyo.
Dk Saidia Primos wa hospitali hiyo akiuliza swali kwenye mkutano huo. Mkurugenzi wa Fedha, Gerald Kimambo (kushoto) akiteta jambo na Mkurugenzi wa Upasuaji, Dk John Kimario kwenye mkutano huo LEO.
………………………………………………………………………………………………………….
Na Neema Mwangomo, Dar es salaam
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Lawrence Museru leo
amekutana na Madaktari wa MNH ikiwa ni mkakati wa kukutana na
watumishi kwa lengo la kuwasikiliza na kujibu kero zao.
Katika mkutano huo uliofanyika
kwenye ukumbi wa CPL uliopo ndani ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH),
Profesa Museru amewapongeza madaktari hao kwa kufanya kazi kwa bidii
na kuimarisha utoaji huduma kwa wagonjwa na kwamba hali hiyo imechangia
MNH kuongeza mapato yake.
Amesema kuongezeka kwa mapato
ya Hospitali na kufikia Shingili Bilioni 4. 5 kwa mwezi kumetokana na
kila mmoja kutimiza wajibu wake.
Amesema kutokana na mafanikio
hayo, MNH imewaongezea madaktari wake posho mbalimbali ili kuongeza
tija katika utendaji, lakini pia hospitali imeamua kutenga Shilingi
Milioni 800 kwa mwaka ili kuwapa mkono wa heri wastaafu wake jambo
ambalo awali halikuwapo.
Hata hivyo amesema mbali na
hatua hiyo, pia MNH imefanikiwa kulipa malimbikizo mbalimbali ya
stahiki za wafanyakazi wake ikiwamo pesa za likizo kwa madaktari
pamoja na watumishi wengine kwa ujumla.
“ Awali changamoto kubwa
ilikuwa ni ucheleweshaji wa stahiki za wafanyakazi kwa Madaktari na
watumishi wengine, lakini katika hilo tumefanikiwa kwani tunaenda nalo
vizuri na tumelipa malimbikizo hayo “ amesema Profesa Museru.
Akielezea mipango ya MNH
Profesa Museru amesema Hospitali ya Taifa Muhimbili ina mipango
mbalimbali ya kuendelea kuboresha huduma zake ikiwemo kuongeza vitanda
vya Chumba ya wagonjwa Mahututi-ICU-, kuongeza ICU ya watoto pamoja na
kina Mama wajawazito.
Kaimu Mkurugenzi huyo Mtendaji wa MNH kesho Juni 23, 2016 atakutana na Wauguzi pamoja na Maafisa Ustawi wa Jamii.
PROF. MAKAME MBARAWA AZINDUA BODI YA TPA
Mwenyekiti
wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Profesa
Ignas Rubaratuka, akitoa ufafanuzi kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (katikati), wakati wa uzinduzi wa
Bodi hiyo jijini Dar es Salaam.Kulia ni Katibu MKuu wa WIzara hiyo,
Sekta ya Uchukuzi, Dr. Leonard Chamuriho.
Wajumbe
wa Bodi mpya ya Bandari Nchini (TPA), wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, wakati wa uzinduzi wa
bodi hiyo.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Profesa
Ignas Rubaratuka (kulia), akimkabidhi Mwenyekiti mpya wa Bodi ya
Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Profesa Ignas
Rubaratuka, vitendea kazi baada ya kuizindua rasmi bodi hiyo.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa akitoa
maelekezo kwa Kaimu Meneja wa Bandari ya Dar es Salaam, Bw. Hebel Mhanga
alipokagua eneo la kupakulia makontena bandarini hapo.
Kaimu
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Nchini (TPA), Eng.
Aloyce Matei (wa kwanza kushoto), akitoa maelezo kwa Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa (wa pili kushoto),
alipokagua miundombinu ya Bandari ya Dar es Salaam.
Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akitoa
maelekezo kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari
Tanzania (TPA), Profesa Ignas Rubaratuka (kushoto), wakati alipokagua
eneo la kuhifadhia magari katika bandari ya Dar es Salaam.
Habari Picha na Benjamini Sawe-Maelezo.
Messi aitanguliza Argentina fainali za Copa America na rekodi juu!
Alfajiri
ya kuamkia Jumatano hii kupitia king’amuzi cha StarTimes watanzania
wapenda soka walishuhudia muendelezo wa burudani ya soka kupitia kwa
nyota wa dunia Lionel Messi akiiongoza Argentina kutinga fainali ya Copa
America kwa kipigo cha magoli 4 – 0 dhidi ya Marekani ambapo alifunga
goli safi kwa mkwaju wa mpira wa adhabu na kutoa pasi za magoli
yaliyosalia kwa Ezequiel Lavezzi (1) na Gonzalo Higuan (2).
Katika mechi hiyo ambayo Messi
ameisaidia kuingia fainali za kombe hilo pia ameweka rekodi ya kuwa
mfungaji bora wa muda wote kuifungia timu ya taifa ya Argentina kwa
kufikisha magoli 55 moja zaidi ya Gabriel Batistuta aliyekuwa
akiishikilia kwa muda wa miaka 14.
Kwa ushindi huo timu ya taifa ya
Argentina ambayo ina kiu kali ya muda wa miaka 23 tangu iuchukue ubingwa
huo sasa inasubiria mshindi wa nusu fainali ya mechi ya pili kati ya
Chile na Colombia itakayochezwa saa 9 alfajiri ya tarehe 23 katika
uwanja wa Soldier Field, Chicago – Illinois nchini Marekani.
Chile ambao ndio mabingwa
watetezi wanatarajia kutetea vema nafasi ya kwenda hatua ya fainali
baada ya kutinga hatua hii kwa kuibamiza timu ya taifa ya Mexico kwa
magoli 7 – 0. Timu hiyo inayoongozwa na nyota wake Alexis Sanchez na
Arturo Vidal mwaka jana ilichukua kombe hilo baada ya kuwafunga timu ya
taifa ya Argentina kwa mikwaju ya penati baada ya kutoshana nguvu ndani
ya dakika 90 za mchezo.
Hivyo basi mashabiki wa soka
ulimwenguni na Tanzania kwa ujumla ambao kwa mara ya kwanza wamepata
fursa ya kujionea michezo yote moja kwa moja kupitia chaneli za Sports
Focus na World Football za StarTimes wanatarajia kushuhudia aidha
fainali ya mwaka jana inajirudia au Colombia kufanikiwa kufikia hatua
hiyo.
Wateja wa StarTimes Tanzania
mbali na kufurahia mechi hizo pia wanazo fursa kabambe za kushiriki
kampeni mbalimbali zinazoendeshwa na kampuni na kushinda zawadi kupitia
kwenye mitandao ya kijamii kama vile facebook na instagram.
Wateja wanaombwa kushiriki
kampeni za ‘tabiri na ushinde’ pamoja na hash tag ya
#CopaAmericaonStarTimes ambazo wanaweza kujishindia fedha taslimu,
tiketi ya ndege kwenda Ujerumani kushuhudia ligi ya Bundesliga msimu
ujao pamoja na simu za mkononi za kisasa.
Wateja wa StarTimes wanashinda
kila siku kutokana kufuatilia kwa makani kampeni hizo kwenye kurasa za
mitandao ya kijamii, lakini ile zawadi kubwa itatangazwa baada ya
mashindano kuisha.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi kukabidhi Ripoti ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 kesho.
Na Daudi Manongi,MAELEZO
Tume ya Taifa ya Uchaguzi
itakabidhi Ripoti ya Uchaguzi mkuu uliofanyika October 2015 kwa Rais wa
Jamhuri Muungano wa Tanzania, Mhe.John Pombe Magufuli kesho tarehe 23
Juni, Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Uchaguzi Bw.Ramadhani Kailima kwa waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam.
Ripoti ya Uchaguzi Mkuu
uliofanyika Mwaka 2015 itafanyika kwa mujibu wa Katiba ya Muungano wa
Tanzania ya Mwaka 1977 ambapo Tume imepewa majukumu ya kuendesha
Uchaguzi wa Rais na wabunge katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Uchaguzi wa Madiwani kwa upande wa Tanzania bara.
Kukamilika kwa Ripoti ya Uchaguzi
Mkuu wa Mwaka 2015 na kukabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kunakamilisha mchakato mzima wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na
kuashiria kuanza kwa maandalizi ya Uchaguzi Mkuu ujao wa mwaka 2020.
No comments :
Post a Comment