Monday, May 6, 2024

Mjane aliyekuwa akilala barabarani ajengewa nyumba


Mwonekano wa nyumba hiyo ya kisasa aliyojengewa na wasamaria wema.

Muktasari:

Judith mwenye watoto watano alikuwa akilala kwenye mataa ya Ubungo jijini  Dar es Salaam,  baada ya kufukuzwa na ndugu wa marehemu mumewe kwenye nyumba yake.

Dar es Salaam. Mjane Judith Wambura, aliyekuwa akilala kwa miezi miwili mfululizo katika mataa Ubungo jijini hapa,  amekabidhiwa nyumba mpya iliyojengwa kwa mchango wa  wasamaria wema.

Judithi alijikuta katika hali hiyo akiwa na watoto wake watano,  baada ya mume wake kufariki na baadaye ndugu zake kumfukuza kwenye nyumba waliyokuwa wakiishi.

Hafla ya kukabidhiwa nyumba hiyo ilifanyika jana Mei 5, 2024 Mvuti ambapo nyumba hiyo ya kisasa imejengwa na kuwekwa samani za kisasa ndani.

Akizunguma katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Taasisi ya GF Foundation walioratibu shughuli hiyo, Godilisen Malisa, amesema kupitia mitandao ya kijamii,  wameweza kuchangisha fedha na wengine kujitolea vifaa mbalimbali vya ujenzi hadi nyumba hiyo kukamilika.

"Michango hii tumekuwa tukiichanga ndani ya muda mfupi, hivyo shukrani zote ziende kwa Watanzania hao ambao wamekuwa wakiguswa kwa namna moja au nyingine," amesema Malisa.

Mkurugenzi huyo amesema hii ni nyumba ya nne kujenga kwa wanawake waliokumbana na vitendo vya ukatili wa kijinsia,  na kuahidi kuendelea kuwasaidia wengine kadri watakavyojaliwa.

Ofisa Habari wa taasisi hiyo, James Mbowe, amesema wamekuwa wakifanya kazi hiyo kwa muda mrefu sasa lakini hawana mfadhili yoyote zaidi ya kutegemea michango ya Watanzania.

"Kutokana na kutokuwa na wafadhili wakubwa wenyewe huwa tunajiita Team Jerojero (Sh500), fedha ambazo huchangwa na Watanzania kusaidia watu wenye matatizo mbalimbali," amesema Mbowe.

Mchungaji wa Kanisa la KKKT Mvuti, Goodluck Kalugiro akimkabidhii nyumba,  Judith Wambura aliyojengewa kwa michango ya wananchi kupitia taasisi ya GF Foundation jana. Picha na Nasra Abdallah.

Wito wake kwa Watanzania amewaomba waone umuhimu wa kushiriki katika kusaidia watu kwa kuwa wao kama vijana wameamua kutumia mitandao ya kijamii ili kubadilisha maisha ya watu wanaopitia changamoto mbalimbali.

Kwa upande wake,  Judith amewashukuru Watanzania waliomchangia na kumtoa kwenye ufukara na sasa anajiona kuwa mtu wa thamani.

"Sina la kuwalipa walioshiriki kunisaidia, naomba niseme sadaka hii waliyoinipa nitaitunza kwa nguvu zangu zote," amesema Judith.

Awali akizungumza katika Ibada ya kuzindua nyumba hiyo, Mchungaji wa Kanisa la KKKT Mvuti, Goodluck Kalugiro, amesema kilichofanywa na taasisi hiyo ni kikubwa katika ulimwengu wa roho na kuna kitu jamii inayomzunguka Judith wamejifunza.

No comments :

Post a Comment