Benki ya CRDB leo imehitimisha awamu ya kwanza ya kampeni yake ya “Tisha na TemboCard” kwa kuwakabidhi tiketi za kushuhudia mashindano ya Kombe la Dunia wateja wake wanne walioibuka washindi wa jumla wa kampeni hiyo.
Akizungumza katika hafla ya kubadhi tiketi hizo iliyofayika kwenye makao makuu ya Benki hiyo yaliyopo barabara ya Ali Hassan Mwinyi, jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Manunuzi wa Benki ya CRDB, Pendason Philemon aliwapongeza washindi hao ambao walipatikana kutokana na kufanya miamala mingi zaidi kupitia kadi zao za TemboCard wakati kampeni hiyo ikiendelea.
“Kwa niaba ya benki niwapongeze kwa kuibuka washindi katika kampeni hii ambayo lengo na madhumuni yake ilikuwa ni kuwajengea watanzania utamaduni wa kutumia kadi zao kufanya malipo mbalimbali” alisema Pendason.
Pendason alisema Benki hiyo inafahamu namna ambavyo Watanzania wanapenda michezo na katika msimu huu wa kuelekea mashindano makubwa ya Kombe la Dunia, imeona ni vyema ikawa sehemu ya kutimiza shauku yao ya kushiriki katika mashindano hayo.
Akielezea kuhusiana na zawadi hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati wa Benki ya CRDB, Bonaventure Paul alisema pamoja na tiketi hizo za kushuhudia mechi za Kombe la Dunia, safari nzima ya washindi hao itagharamiwa kuanzia tiketi za ndege kuelekea Doha Qatar, malazi, pamoja na fedha za matumizi wakifika huko.
Washindi walioibuka kidedea kwenye safari ya kushuhudia Kombe la Dunia mwaka huu wa 2022 ni:, Haji Athumani Msangi, Erick Boniface Kashangaki, Kelvin Jackson Twissa na Rajabu Dossa Mfinanga wote ni wakazi wa jijini Dar es Salaam.
Katika hafla hiyo Benki ya CRDB pia ilikabidhi zawadi za fedha taslimu kwa washindi wengine watatu wa kampeni hiyo ambao ni, Janeth Nyingi amejishindia shilingi Milioni Moja, Benedict Tilisho na Marsh Bakari wamejishindia shilingi laki tano kila mmoja.
Akitoa shukrani kwa wateja na wadau wote walioshirki katika kampeni hiyo, Meneja Masoko wa Bidhaa na Huduma Benki ya CRDB, Julius Ritte alisema kampeni hiyo ya “Tisha na Tembocard” sasa inakwenda kuingia katika awamu ya pili huku akiwataka wateja kuendelea kutumia kadi zao za TemboCard.
Mkurugenzi wa Manunuzi wa Benki ya CRDB, Pendason Philemon (wa pili kulia) akimkabidhi mfano wa hundi ya safari iliyolipiwa kwenda Doha – Qatar kushuhudia mashindano ya kombe la Dunia mmmoja wa washidi Haji A. Msangi (katikati) katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa jumla katika hitimisho la awamu ya kwanza ya kampeni “Tisha na TemboCard”, iliyofanyika Makuu ya Benki, Palm Beach, jijini Dar es salaam leo Novemba 03, 2022. Wengine pichani kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Wateja Wadogo na Wakati Bonaventure Paul, Mkuu wa Kitengo cha Masoko Joseline Kamhanda, na Mkuu wa Biashara ya Kadi Benki ya CRDB, Farid Seif.
No comments :
Post a Comment