Rais wa Jamhuri ya Burundi, Evariste Ndayishimiye akiwa kwenye mazungumzo na ujumbe wa Benki ya CRDB, ulioongozwa na Mwenyekiti wake, Dkt. Ally Laay na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela wakati walipomtembelea kwenye makazi rasmi yaliyopo eneo la Kiriri, Bujumbura, Novemba 25, 2022. Mkutano huo ilikuwa ni sehemu ya muendelezo wa maadhimisho ya miaka 10 ya kampuni tanzu ya Benki ya CRDB Burundi, ambayo kilele chake kilifanyika mwishoni mwa wiki. Picha zote na Othman Michuzi.
---
Bujumbura, Burundi. Ikitarajia kufungua tawi la tano mapema mwakani itakapofikisha miaka 11 ya kutoa huduma za fedha nchini Burundi, Rais wa Jamhuri ya Burundi, Evariste Ndayishimiye ameipongeza Benki ya CRDB kwa huduma bora ilizozitoa kwa muongo mmoja sasa.
Benki hiyo iliyoingia nchini Burundi mwaka 2012 ina matawi manne kwa sasa yanayotoa huduma pamoja na mawakala zaidi ya 600 wanaohakikisha wananchi na wafanyabiashara wanahudumiwa kwa wakati na mapato ya Serikali kukusanywa kwa utaratibu rahisi nchini humo.
Rais Ndayishimiye ametoa pongeza hizo alipozungumza na menejimenti ya Benki ya CRDB iliyoongozwa na Afisa Mtendaji Mkuu wake, Abdulmajid Nsekela aliyeambatana na wajumbe wa bodi ya wakurugenzi kusherehekea miaka 10 ya kutoa huduma nchini humo.
“Burundi tumeipokea Benki ya CRDB kwa mikono miwili na tunajivunia uwepo wake. Tanzania na Burundi ni ndugu wa karibu, hata mipaka iliyopo ni matokeo ya ukoloni lakini haiwezi kuwa kikwazo cha mahusiano mazuri yenye historia kubwa ya ushirikiano. Tunashukuru kuwa Tanzania ilishiriki kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa amani Burundi na sasa mnakuja tufanye maendeleo kwa pamoja kwa manufaa ya nchi zetu,” alisema Rais Ndayishimiye.
Katika kipindi hicho cha kutoa huduma nchini Burundi, Benki ya CRDB imefanya vyema sokoni hadi kushika nafasi ya tatu kwa kupata faida kubwa kati ya benki 13 zilizopo. Mpaka Septemba mwaka huu, benki hiyo ilikuwa imetoa mikopo kiasi cha faranga 300 bilioni (Sh338 bilioni).
Mwaka 2019 Serikali ya Burundi iliyahamisha makao makuu yake kutoka Bujumbura kwenda jiji la Gitega hivyo Benki ya CRDB inatarajia kufungua tawi jipya huko ili kuihudumia pamoja na wafanyakazi wake, wafanyabiashara na wananchi wa kawaida. Tawi hilo litafunguliwa mapema mwakani.
“Tunawashuru sana kwa jitihada zenu ya kutoa elimu ya fedha kwa Warundi ili wajifunze namna nzuri ya usimamizi wa fedha na kuwekeza. Tungependa kushirikiana nanyi zaidi katika programu za vijana na wanawake ambao ni kipaumbele chetu kikubwa kwa sasa,” alisema Rais Ndayishimiye.
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa CRDB, Nsekela alisema Serikali ya Burundi inawapa ushirikiano mkubwa unaowasaidia kupata mafanikio ndani ya miaka 10. Serikali imeipa benki9 hiyo eneo la kujenga ofisi katika Jiji la Gitega.
“Benki ya CRDB itaendelea kuunga mkono jitihada za kukuza uchumi wa Burundi kwa manufaa ya Warundi, Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla. Tunatarajia kuingia DRC (Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo) hivi karibuni na tutafungua matawi katika mikoa iliyo karibu na mpaka wa Burundi na DRC ili kuchochea biashara kati ya nchi hizo mbili,” alisema Nsekela.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa CRDB, Dk Ally Laay alisema haikuwa rahisi kuridhia uamuzi wa kufungua biashara nchini Burundi kwa kuwa ilikuwa ni mara ya kwanza kutoa huduma nje ya nchi.
“Maswali yalikuwa mengi juu ya kuichagua Burundi lakini leo hii sote tunajivunia na kuona nchi zote mbili zinanufaika. Hapa Burundi tunalipa kodi na kutoa ajira huku faida inayopatikana ikiwanufaisha wanahisa wetu hadi Tanzania,” alisema Dk Laay.
Rais wa Jamhuri ya Burundi, Evariste Ndayishimiye (katikati) akimpongeza Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa (kulia) wakati walipomtembelea kwenye makazi rasmi yaliyopo eneo la Kiriri, Bujumbura, Novemba 25, 2022. Kushoto ni Mjumbe wa Bodi ya Benki ya CRDB Burundi, Kahumbya Bashige
Rais wa Jamhuri ya Burundi, Évariste Ndayishimiye akiagana na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, baada ya kumaliza mazungumzo yao walipomtembelea kwenye makazi yake rasmi yaliyopo eneo la Kiriri, Bujumbura, Novemba 25, 2022. Wengine pichani ni Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay (watatu kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya CRDB Burundi, Hosea Kashimba (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Burundi, Fredrick Siwale (wapili kushoto), Afisa Mkuu wa Uwendeshaji wa Benki ya CRDB, Bruce Mwille (kulia), Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa, Mjumbe wa Bodi ya Benki ya CRDB Burundi, Kahumbya Bashige pamoja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Burundi, Menard Bucumi. Mkutano huo ilikuwa ni sehemu ya muendelezo wa maadhimisho ya miaka 10 ya kampuni tanzu ya Benki ya CRDB Burundi, ambayo kilele chake kilifanyika mwishoni mwa wiki.
--
No comments :
Post a Comment