Wednesday, September 7, 2022

TIBA NA DAWA YA UKIMWI, MALARIA NA KIFUA KIKUU NI BURE; WAZIRI UMMY MWALIMU












 Englibert Kayombo WAF - Kibaha, Pwani.

Serikali kwa kushirikiana na Global Fund bado zinaendela kukabiliana na magonjwa ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria kwa kuhakikisha matibabu ya magonjwa hayo yanapatikana bure na kwa urahisi katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu akiwa na mgeni wake Bw. Peter Sands Mtendaji Mkuu wa Global Fund walipotembelea Zahanati ya Disunyara iliyopo Wilaya ya Kibaha kuona hali ya utoaji huduma na utekelezaji wa afua za mapambano dhidi ya magonjwa hayo

“Bado tunapambana na mgonjwa makubwa matatu Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria, tunawashukuru sana Global Fund kwa kufadhili mwitikio wa nchi katika mapambano dhidi ya magonjwa hayo” amesema Waziri Ummy Mwalimu

Waziri Ummy ameishukuru  Global fund kwa kuendelea kufadhili upatikaji bure wa dawa za kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARV), vipimo vya haraka vya utambuzi wa ugonjwa wa Malaria, Sindano za Malaria kali, Dawa za Malaria (ARU) pamoja na tiba ya ugonjwa wa Kifua Kikuu.

Hata hivyo Waziri Ummy amewatahadharisha wachanchi kuepuka kununua dawa, vipimo, sindano za Malaria kali kwa kuwa zinatolewa bure ikiwemo pamoja na tiba ya Kifua Kikuu na Ukimwi.

Waziri Ummy ameshukuru Global Fund kwa kuipatia Tanzania zaidi ya Shiligi. Trilioni 1.5 ndani ya kipindi cha miaka mitatu toka 2020 kwa ajili ya utekelezaji wa afua za mapambano dhidi ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria huku pia wakitoa mchango kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa UVIKO-19 pamoja na kuimarisha mifumo ya afya.

Kwa upande wake Bw. Peter  Sands ameshukuru kwa kupata Mwaliko kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuja nchini na kuona namna Tanzania inavyopambana kukabiliana na Ugonjwa wa Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria.

“Sikutaka ziara yangu hapa Tanzania iishie kufanya vikao tuu bali nitembelee na kujionea jinsi gani huduma zinatolewa katika ngazi ya msingi pamoja na mapambano dhidi ya magonjwa kwa kushirikiana na Global Fund” amesema Bw. Sands

Bw. Sands amesema amefurahishwa na hali ya utoaji huduma za afya katika vituo vya kutolea huduma hizo na kuipongeza Serikali kwa juhudi kubwa inazozifanya katika kuboresha ubora wa huduma za afya.

“Kwa pamoja tumeweza kupata mafanikio makubwa katika mapambano dhidi ya magonjwa haya matatu na kuweza kuokoa maisha ya watu na kupunguza kiwango cha maambuki katika magonjwa ya Ukimwi, Kifua Kikuu na Malaria, bado tuna kazi kubwa sana lakini tumepiga hatua kubwa” amesema Bw. Sands

Bw. Sands amesema kuwa baada ya wiki mbili zijazo Rais wa Marekani Mhe. Joe Biden anatarajia kuitisha Mkutano mkubwa kwa ajili ya kuhamasisha upatikanaji wa Shilingi Bilioni 18 (USD) Dola za Marekani kwa ajili ya kutunisha mfuko wa Global Fund kuwezesha utekezaji wa mapambano zaidi ya magonjwa hayo.

No comments :

Post a Comment