Friday, July 8, 2022

Prof: Kahyarara: Watanzania Mnaweza Kumiliki Viwanda Vijijini Na Mijini


 Na Mwandishi Wetu

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Prof. Godius Kahyarara amesema  Wizara imeandaa programu maalumu ya  Suluhisho la Pamoja la Uwekezaji katika Viwanda inayojulikana kama "Total Industrial Solution" inayolenga kuwawezesha wananchi kumiliki  viwanda kuanzia vijijini hadi mijini ndani ya miezi sita (6)  kwa milioni 6 - 600.



Prof. Kahyarara ameyasema hayo Julai 7, 2022 wakati wa kipindi cha Supa Brekfast  kinachoendeshwa na Kituo cha Radio cha East  Africa,  jijini Dar es salaam kwa lengo la  kuelimisha umma kuhusu programu maalumu ya Total Indusrtial Solution inayowawezesha wawekezaji wa ndani kumiliki viwanda vidogo na vya kati maeneo mbalimbali nchini.

Amesema  matokeo makubwa ya programu hiyo ni kuondoa changamoto ya upungufu wa sukari na mafuta ya kula  na kupunguza uagizaji wa bidhaa hizo ndani ya miaka miwili (2) kwa  kuwawezesha wananchi  kuwa na mitaji, maeneo  na mashine au mitambo midogo ya kuchakata mazao hayo  kwa gharama nafuu na kwa muda mfupi ili kutatua changamoto mbalimbali za uhaba wa bidhaa muhimu pamoja na kuongeza ajira.

Akiongea kuhusu matokeo ya diplomasia ya uchumi,  Prof. Kahyarara amesema baada ya  EXPODUBAI 2020, Filamu ya Royal Tour na ziara katika nchi mbalimbali  za nje, uchumi umepanda,  makusanyo ya kodi kwa kila mwezi yameongezeka kutoka Tirioni 1.3 hadi Tirioni 1.9 na mauzo ya nje yameongezeka kwa asilimia 30.

Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita  imepanga kutumia viwanja vya ndege vya  kama lango la uchumi  na kuboresha masoko ya mipakani kwa kujenga maeneo maalumu yatakayokuwa na  viwanda vya uchakataji na uhifadhi wa mazao kwa ajili ya mauzo ya nje ili kurahisisha usafirishaji wa mazao hayo pamoja na kusaidia wakulima kupata soko la mazao yao kwa bei inayostahili.

Akifafanua zaidi kuhusu Maonesho ya 46  ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yalianza tarehe 28 Juni hadi 13 Julai 2022, Prof. Kahyarara amesema mwaka huu maonyesho hayo yamejumuisha  makampuni yaliyoshiriki 3200 ya ndani na 180  ya nje pamoja na  kongamano lilowakutanisha  wawekezaji, wanunuzi na wauzaji 75 wa ndani na 21 wa nje ya nchi  waliojadiliana na  kuonesha uhitaji mkubwa wa mazao mbalimbali ikiwemo Mahindi na mchele kuuzwa nje ya nchi. Pia yatatambua wawekezaji walipaji kodi  wakubwa watatu (3) na wanaoongoza kwa mauzo ya nje watatu (3.) 

No comments :

Post a Comment