Tuesday, May 3, 2022

Makaratasi zinapotumika mbadala wa maji chooni

karatasi pic

Mmoja wa wanafunzi akionyesha majani wanayoyatumia vyooni

By Elizabeth Edward

Igunga. Ni bomu kubwa linalotengenezwa linasubiri kulipuka na siku likilipuka litaacha madhara makubwa. Hivi ndivyo inavyoweza kuelezwa kwa kinachoendelea katika shule ya msingi Mwanzugi iliyopo wilayani hapa mkoani Tabora.

Shule hii iliyo umbali wa kilomita 10 kutoka makao makuu ya halmashauri ya wilaya ya Igunga ina wanafunzi 1,848 wa darasa la awali hadi la saba ina matundu manane ya vyoo. Kulingana na mwongozo wa Serikali tundu moja la choo linatakiwa kutumiwa na wavulana 25 na tundu kama hilo linatakiwa kutumiwa na wasichana 20, hivyo kwa idadi ya matundu nane yaliyopo Mwanzugi inahitaji matundu 84.

Uchache huu wa matundu ya vyoo unasababisha muda wa mapumziko kuwa na foleni kubwa wakisubiri kutumia choo, kukwepa hilo wengi wanalazimika kujisaidia porini.

Shule hiyo inayozungukwa na vichaka vilivyosheni miti vimekuwa msaada kwa watoto hao kwani majani hayo ndiyo yamekuwa yakitumika kama mbadala wa maji katika kujisafishia baada ya kujisaidia.

Pamoja na uwepo wa vyoo hivyo nane, vinne vikiwa vya wavulana na vinne vya wasichana hakuna hata kimoja chenye maji wala ndoo ya maji ambayo yangeweza kutumiwa na wanafunzi hao. Si kwamba shule hiyo haina maji la hasha, bomba lipo umbali wa kati ya mita 70 hadi 100 kutoka kilipo choo na hakuna namna ya kumuwezesha mwanafunzi kukinga maji na kuyapeleka chooni ili yatumike pale anapohitaji.

Kuepusha usumbufu huo watoto wanaamua kuchana madaftari kwa ajili ya kupata karatasi za kujifutia, wengine wanachuma majani huku baadhi wakiamua kutonawa kabisa bila kujua ni hatari kiafya.

ADVERTISEMENT

Naomi Amos ni mwanafunzi wa darasa la sita shuleni hapo, anathibitisha hilo akieleza kuwa mazingira yanawalazimisha kufanya hivyo ili kwenda sawa na muda wa darasani.

“Muda wa mapumziko kunakuwa na foleni kubwa, inaweza kutokea mnaingia wawili kwa pamoja ili kupunguza msongamano, sasa kama hutaki kupoteza muda tunakwenda porini huko tunajisaidia bila shida na kurudi darasani.”

Mwananchi iliingia hadi kwenye vyoo hivyo na kuona hali halisi na havikuwa katika hali ya usafi inayoruhusu kutumiwa na watoto wadogo.

Kuhusu namna wanavyovitumia vyoo hivyo bila kuwepo maji Naomi anasema: “Huwa tunatumia makaratasi, tunachana daftari yaliyoisha na kujisafishia au tunachukua yale majani kwenye miti tunajifutia na kuyatupa shimoni.”


Bomba la maji na wanafunzi

Mbali na bomba hilo kutokuwa msaada kwa wanafunzi wanapohitaji maji baada ya kujisaidia, halikidhi hata mahitaji ya kunywa kutokana na idadi ya kubwa ya wanafunzi hivyo kusongamana katika bomba moja. Hali hii inawafanya wanafunzi kuomba maji nyumba za jirani na shule na wengine wanatumia maji ya bwawa la Mwanzugi kukata kiu zao licha ya kutokuwa salama.

Bomba hilo liko mbali na katika mazingira ambayo si rahisi kutumiwa na watu wengi kwa mara moja kwa kuwa liko chini na fupi hivyo, kuwalazimu wanafunzi kuinama ili kukinga maji.

Hakuna vikombe au ndoo ambazo zingewazesha wanafunzi kupata maji safi na salama na badala yake wanatumia kwa kukinga mikono au madumu tena kwa kupokezana.

James Mashimba si jina halisi ni mwanafunzi wa darasa la tano shuleni hapo na ambaye alithibitisha wanafunzi kutumia maji ya bwawa hilo huku akikiri mara kadhaa wanaugua matumbo na maradhi mengine kutokana na maji hayo.

“Pale kuna bomba kama unavyoona watumiaji ni wengi, wanafunzi na walimu wote tunategemea bomba lile, kuna muda inatokea mnakuwa wengi, wengine wanaona kusimama pale kwa muda mrefu ni shida hivyo wanakwenda kunywa maji ya bwawani.

Yale maji ya bwawani tunaambiwa sio mazuri ni machafu lakini tumekuwa tukinywa hayo kwa muda mrefu na kweli kuna wakati inatokea tunapata madhara, mimi binafsi sinywi tena maji yale niliwashi kuumwa sana tumbo. Tangu wakati huo ni bora nisuburi watu wapungue ili ninywe maji masafi ya bombani,” anasema Mashimba.

Mmoja wa walimu shuleni hapo ambaye hakutaka kuweka wazi jina lake, anasema pamoja na uhaba wa matundu ya vyoo, jamii hiyo ina changamoto ya matumizi sahihi ya vyoo.

“Ni kweli hapa kuna changamoto ya vyoo hata maji hayapo kwenye vyoo lakini jamii ina shida kwenye suala zima la afya na usafi, watoto wamezoea kujisaidia porini na hata ikitokea ametumia choo ni nadra kujisafisha kwa maji.

“Maji yapo lakini mtu anaona ni heri atumie majani au avae nguo hivyo hivyo kuliko kwenda bombani kutafuta chombo akinge maji ajisafishe mwili wake vizuri na kunawa mikono kabla ya kurejea darasani, kiukweli hii ni changamoto kubwa,” anasema mwalimu huyo.

Deokalia Shija ni mzazi wa mwanafunzi anayesoma shuleni hapo, anasema kuna tatizo kubwa la watoto kuugua sababu ya uchache wa vyoo na unywaji wa maji ya kwenye bwawa.

“Vyoo viko nane, unafikiri wakiachiwa mapumziko kuna nini pale kama sio mbanano ndiyo maana wengine wanakwenda porini kujisaidia, sasa kwa mtindo huu kila siku tuna kazi ya kupeleka hospitali watoto wanaumwa mara tumbo, mara UTI sijui wengine wanaharisha.

Hilo bomba liko moja wanatumia walimu na wanafunzi 1,848 hapo lazima kuwepo foleni na wakati mwingine watoto wanakwenda nyumba za jirani kuomba maji, sasa afadhali wafanye hivyo, wengine wanakunywa maji ya bwawani.”


Maoni ya wadau wa elimu

Wadau wa elimu akiwemo Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet), Wayoga Ochola anasema “Nimeshtushwa na hili, haiingii akilini watoto zaidi ya 1,800 kutumia matundu nane ya vyoo, hii ina maana ikitokea ule muda wa mapumziko wote wanahitaji kwenda chooni basi maafa yanayeweza kutokea.

“Hii ni hatari, hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa tena kwa uzito maana hatuwezi kuwa tunafurahia watoto wanapata elimu wakati wapo katika mazingira hatarishi. Mtu ni afya na elimu inapaswa kwenda sambamba na afya,”.

Naye Meneja shirika la Uwezo Tanzania Greyson Mgoi anatupa lawama kwa wanajamii kwa kuweka hatarini afya na maisha ya watoto.

“Hali imeshakuwa hivyo watoto 1,800 wanatumia vyoo nane, huwezi kukaa kusubiri Serikali ije kujenga vyoo,” anasema.

No comments :

Post a Comment