Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Nijeria, umeanza kufundisha rasmi Lugha ya Kiswahili nchini humo. Darasa la kwanza limejumuisha wafanyakazi takribani hamsini (50) wa Nigerian Export Promotion Council (NEPC). Program hiyo inatarajiwa kuendeshwa kwa kipindi cha miezi mitatu.
NEPC imeamua kuwapatia mafunzo hayo Wafanya kazi wake ili kuwawezesha kufanya maonesho ya Biashara na kutangaza bidhaa zinazozalishwa nchini Nigeria katika nchi zinazozungumaza Kiswahili hususan ukanda wa Afrika Mashariki.
Ubalozi umeanzisha program hiyo kwa kushirikiana na BAKITA na Diaspora wa Tanzania nchini Nigeria ambao wamejitolea kuendesha program hiyo kwa uzalendo. Wenza wa Maafisa wa Ubalozi pia wamejitolea kuunga mkono juhudi hizo.
Akifungua mafunzo hayo, Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Nigeria alieleza kuwa “mafunzo hayo yatazidi kuimarisha ushirikiano kati ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirikisho la Nigeria mbali na kukuza lugha hii adhimu”.
Kuanzishwa kwa mafunzo hayo, ni utekelezaji wa sera na maelekezo ya Serikali kukikuza Kiswahili na kufanya lugha hiyo kuwa miongoni mwa lugha inayozungumzwa na idadi kubwa ya watu ulimwenguni. Aidha, Mafunzo haya yataendeleza na kukuza utamaduni wa Watazania katika nchi mbalimbali.
No comments :
Post a Comment