Monday, August 30, 2021

Serikali Kuingiza Umeme Wa Jotoardhi Kwenye Gridi Ya Taifa

1.    Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemeni akifungua valvu ya kisima cha nishati ya jotoardhi kinachotoa maji ya moto katika Mradi wa Kiejo Mbaka ulioko Wilaya ya Rungwe Mkoani Mbeya.

  Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemeni ameagiza kuharakishwa kwa utekelezaji wa mradi wa uzalishaji umeme wa jotoardhi ili kuingiza katika gridi ya taifa.

Maagizo hayo ameyatoa mwishoni mwa juma alipotembelea mradi wa nishati ya jotoardhi wa Kiejo Mbaka ulioko Rungwe Mkoani Mbeya akiwa ziarani mkoani humu kukagua miradi ya umeme.

“Tunataka kwenye gridi ya taifa tuingize umeme unaotokana na rasilimali ya jotoardhi, tuanze na megawati 30 za Mbozi (Songwe) na hizi megawati 10 (Kiejo Mbaka) tuwe na megawati 40 mwakani,” alisema Dkt Kalemani.

Ameomba kuongezwa kwa kasi na wataalam ili mradi huo ukamilike mwezi Disemba mwaka 2022.

Ameongeza kuwa katika gridi ya taifa hakuna umeme wa nishati ya jotoardhi ila kwa sasa jitihada zinafanywa na Serikali ili kuwa na umeme huo katika gridi ya taifa.

Dkt. Kalemani amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kutoa shilingi bilioni 1.15 katika utekelezaji wa mradi wa Kiejo Mbaka.

Katika hatua nyingine Dkt. Kalemani ameipongeza Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) kwa kutumia wataalam wa ndani katika utekelezaji wa mradi huo.

“Niwashukuru TGDC kwa mara nyingine kwa kufanya kazi hii na wataalam wa ndani, …ni watanzania wenyewe kwa kupitia uwezo wa ndani na wataalam wa ndani kwa hilo hongereni sana,” amesema Dkt. Kalemani.

Vilevile, ametaka kuimarishwa kwa ulinzi katika eneo la mradi ili kuzua watu wenye nia mbaya kuhujumu miondombinu uliyopo kwenye eneo la mradi huo.

Dkt. Kalemani ameomba kutolewa kwa elimu kwa wananchi wanaozunguka eneo la mradi ili wafahamu umuhimu wa mradi huo na waweze kushiriki kikamilifu katika mradi.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa TGDC, Mha. Kato Kabaka amesema kuwa kwa sasa mradi huu upo katika hatua ya uhakiki wa rasilimali ya jotoardhi kwa kuchoronga visima katika eneo la mradi.

Hatua hii ya uchorongaji wa visima vifupi vitatu (3) vya utafiti, ina lengo la kuongeza taarifa za kisayansi ambazo zitatoa tathimini bora ya kuchoronga visima virefu vya uhakiki wa jotoardhi,” alifafanua Mha. Kabaka.

Aidha, amesema majimoto yaliyopatikana kutokana uchorongaji huo yanatarajiwa kutumika katika miradi ya matumizi mengine kama vile kukausha mazao, kilimo cha nyumba vitalu, ufugaji na uchakataji wa bidhaa za viwanda viwandani.

Mha. Kabaka amesema “hatua hii itaisadia kuharakisha matumizi ya jotoardhi katika shughuli za kiuchumi na kijamii, huku TGDC ikiongeza vyanzo vyake vya ndani vya mapato,”.

 

No comments :

Post a Comment