MWENYEKITI wa Mfuko wa Kuchochea Maendeleo Jimbo la Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo akiwa ameongoza na wajumbe wa Mfuko huo wa Jimbo ambao ni Diwani wa Kata ya Makurumla, Bakari Kimwanga (kulia), Diwani wa Viti Maalumu, Hawa Abdulrahman (hayupo pichani) wakikagua miradi ya jimbo
MWENYEKITI wa Mfuko wa Kuchochea Maendeleo Jimbo la Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo, amewaongoza wajumbe wa mfuko huo kufanya ukaguzi wa
miradi ya maendeleo ambayo inatarajiwa kupatiwa fedha na mfuko huo.
Katika ziara
hiyo Profesa Kitila aliambatana na wajumbe wa Mfuko huo wa Jimbo ambao
ni Diwani wa Kata ya Makurumla, Bakari Kimwanga, Diwani wa Viti Maalumu,
Hawa Abdulrahman.
Wengine ni Isihaka Waziri, Rozina Kimario
pamoja na mchumi, ambapo hatua hiyo imetokana na uamuzi wa kamati hiyo
kutembelea miradi yote kwenye jimbo kabla ya kuanza kutoa fedha.
Kutokana
na changamoto kadhaa zilizopo katika kata nane za Jimbo la Ubungo
ambazo ni Ubungo, Kimara, Makuburi, Sinza, Mburahati, Makurumla, Mabibo
na Manzese wajumbe kwa kauli moja waliamua kwenda kufanya ukaguzi wa
miradi hiyo ili kujiridhisha kama ina vigezo vya kusaidiwa kwa haraka.
Katika
ziara hiyo Mwenyekiti wa Mfuko wa Kuchochea Maendeleo Jimbo la Ubungo,
Profesa Kitila aliwaambia wananchi wa kata za Makurumla, Manzese na
Mabibo kuwa Serikali imetoa kiasi cha Sh milioni 70.6 kwa ajili ya
kuchochea maendeleo kwenye jimbo hilo.
Amesema wajumbe kwa kauli
moja wamekubaliana kutoa kipaumbele cha fedha katika miradi ya elimu,
afya na miundombinu hasa ya babarabara na vivuko ambavyo vimekuwa kero
kubwa kwa wananchi.
“Tumetembea hapa Mto China na tumeona hali
ya takataka zinazosafirishwa na maji namna zilizoziba mto nasi kupitia
Mfuko wa Jimbo tutaingiza kiasi cha fedha ili kisaidie kazi hii ambayo
chini ya diwani ataisimamia.
Pia tutasaidia barabara muhimu ya
kwa Mloka Mtaa wa Kilimahewa ila kubwa tunawaomba watalaamu wa Tarura
watusaidie gharama ili tuweze kukamilisha kazi hii kwa wakati.
“Tunataka
fedha hizi zinazotolewa na Serikali ziende zikaguse maendeleo ya
wananchi moja kwa moja,nasi kupitia Kamati ya Mfuko wa Jimbo kila senti
ambayo tutapokea kutoka serikalini tutaweka wazi na wala si kificho,”
amesema Profesa Kitila
Pamoja na hali hiyo wajumbe hao walitembelea Kata ya Mabibo na kuona athari za Mto Gide pamoja na Mto Mbokomu Kata ya Manzese.
No comments :
Post a Comment