Monday, February 1, 2021

Azania Bank wapimwa homa ya ini na Ocean Road kuelekea kilele Siku ya Saratani Duniani

Pichani ni Mkurugenzi Mtendaji wa Azania Bank Co. LTD, Mr. Charles Itembe (kutoka kushoto), akifuatiwa na Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu, Neema Massanja, Mkurugenzi Huduma za kinga ya Saratani wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), Dk. Crispin Kahesa na Dr.Maguhwa Stephano wakiwa pamoja na timu ya watoa huduma kutoka Ocean Road.

…………………………………….

Na Mwandishi Maalum (ORCI) – Dar es Salaam

Benki ya Azania imeamua kuwapa fursa wafanyakazi wake kufanyiwa uchunguzi wa homa ya ini

na wataalamu mabingwa wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), kuelekea kilele cha Siku ya saratani Duniani ambayo huadhimishwa Februari 4, kila mwaka.

Wafanyakazi wasiokutwa na maambukizi ya homa hiyo wanapatiwa chanjo ya Hepatitis B ili kuwakinga dhidi ya maambukizi hayo, imeelezwa.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga wa ORCI, Dk. Crispin kahesa amesema watatoa huduma hiyo kwa wafanyakazi wa benki hiyo iliyosambaa zaidi ya mikoa 11 ikiwa na matawi zaidi ya 25.

“Lengo ni kuwapa chanjo wafanyakazi 550 na zoezi hili limeanza leo,” amebainisha.

Amebainisha mikoa watakayoifikia na kuwapa huduma hiyo wafanyakazi wa benki hiyo ni Dar es salaam, Dodoma, Morogoro, Arusha, Moshi, Mbeya,Tunduma, Geita, Simiyu, Mwanza na Shinyanga.

“Tunazidi kuhamasisha jamii kushiriki na kujitokeza kufanya upimaji na kupokea huduma za kujikinga thidi ya Saratani,” ametoa rai.

Dk. Kahesa amesema Ocean Road imekuwa ikitoa huduma katika jamii kupitia kampeni kwa wananchi, maeneo ya mahali pa kazi na vyuoni.

“Huduma hii inapatikana katika taasisi yetu hapa Dar es Salaam, lakini pia tuna utaratibu maalum na rafiki kuweza kuwafikia wananchi popote walipo mahala pa kazi, vyuoni na kwengineko.

“Hivyo, kwa wale wanaohitaji tuwafikie popote walipo wasisite kuwasiliana nasi kwa utaratibu maalum kwa kuwalisiliana nasi,” amesisitiza.

 

No comments :

Post a Comment