********************************************
Na. Angela Msimbira CHEMBA
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo amechefuliwa na kitendo cha ucheleweshwaji wa miradi katika Wilaya ya Chemba huku akimwagiza Mkurugenzi kuhakikisha leo saa nne asubuhi anampelekea maelezo ni kwanini
wasichukuliwe hatua kwa uzembe huo.Hali hiyo ilijitokeza leo wakati alipotembelea Miradi inayotekelezwa kwenye Wilaya hiyo ambapo kwa kiasi kikubwa hakufurahishwa na kasi ya ujenzi wakati maeneo mengine nchini imekamilika licha ya fedha kutolewa kwa wakati.
Waziri Jafo ameitaja miradi hiyo kuwa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na bweni moja katika Shule ya Sekondari ya Chemba na Jengo la Utawala la Halmshauri ya wilaya hiyo ambayo hadi sasa haina maendeleo yoyote licha ya kutakiwa iwe imekamilika mwaka huu.
Aidha, alikataa kupokea taarifa kuhusu mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Wilaya hiyo ambayo inaeleza uwepo wa mapungufu ya fedha wakati Serikali imetoa Fedha yote bilioni 1.8 lakini wao wanasema bilioni 1.5.
“Nimezunguka nchi nzima lakini hapa Chemba mna hali mbaya na hiyo inasababishwa na baadhi ya viongozi kutojua changamoto za wananchi maana hapa kuna watoto wanahitaji huduma lakini ninyi hamfanyi kazi na ni dhambi kubwa mnafanya” amesema Mhe. Jafo.
Amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba Dkt. Semistatus Mashimba na wakuu wa idara kuwasilisha kesho maelezo kuhusu kwa nini wasichukuliwe hatua kwa uzembe wakutokukamilisha miradi ya maendeleo kwa wakati na uzembe uliokidhiri.
“Chemba ni wazembe na mmecheza na fedha licha ya kwamba Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Mhe Dkt. John Pombe magufuli ndio ametoa na hii inatokana na wengi wenu mmekulia kwenye mboga nane na hamjui changamoto za wananchi wa chini,”amesisitiza Waziri Jafo.
Waziri Jafo ameongeza kuwa hawezi kuhangaika kwa watu ambao hawana uchungu na wananchi na kwamba kuna viongozi wamepewa dhamana lakini hawajui matatizo.
Kuhusu ujenzi wa Bweni na shule alisema viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba hawapo makini na kazi kwani miradi mingi imedorora, hali ambayo inarudisha nyuma maendeleoya halmashauri hiyo.
“kwa sababu haiwezekani hadi leo hamjakamilisha ujenzi wa shule na bweni ndio mmeanza msingi kwahiyo nataka maelezo kwanini serikali isifanye jambo kwa uzembe huo, ujenzi hospitali za wilaya wenzenu wamefanya mambo makubwa zaidi ya mliyofanya na sijaridhishwa na mmenipa taarifa ya uongo kwamba mmepokea Bilioni 1.5 badala ya bilioni 1.8 ni kosa kubwa.amesisitiza” Waziri Jafo
Kutokana na changamoto hizo, Waziri Jafo amemwagiza Katibu Mkuu TAMISEMI, Mhandisi Joseph Nyamhanga kuunda timu maalum ili kuchunguza matumizi ya fedha za miradi katika Wilaya hiyo na kazi hiyo ianze Januari mosi hadi 19 mwakani iwe imekamilika.
“Pia wachunguze nani alifanya uzembe na kwanini ziliingia kule na kurudi serikalini pia wachunguze mahusiano yaliyopo baina ya watendaji na wafanyakazi maana hakuna mahusiano mazuri Chemba ili itafutwe dawa ya kuondoa changamoto hiyo,”Amesisitiza Waziri Jafo
No comments :
Post a Comment