Mkurugenzi wa huduma za kinga
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard
Subi akiwa na timu ya uhamasishaji kutoka Wizara ya Afya na taasisi
isiyo yakiserikali ya Project CLEAR juu ya elimu ya kujikinga dhidi ya
maambukizi ya virusi vya Corona.
Mkurugenzi wa huduma za kinga
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard
Subi akinawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka ikiwa ni
sehemu ya kuunga mkono kampeni ya “Mikono safi, Tanzania salama”
inayolenga kuelimisha wananchi juu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya
virusi vya Corona.
Mkurugenzi wa huduma za kinga
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard
Subi akieleza jambo wakati akiongea na Waandishi wa habari katika juu
ya mwenendo wa kampeni ya “Mikono safi, Tanzania salama” inayolenga
kuelimisha wananchi juu ya kujikinga dhidi ya maambukizi ya virusi vya
Corona.
********************************
Na WAMJW- DSM
Mkurugenzi wa huduma za kinga
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Leonard
Subi ametoa wito kwa wananchi kutosafiri kwenda vijijini kwa lengo la
kuwasalimia ndugu katika kipindi hiki ili kuzuia maambukizi ya virusi
vya Corona kusambaa zaidi nchini.
Wito huo ameutoa leo, wakati
akiongea na Waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya
Jijini Dar es Salaam juu ya mwenendo wa kampeni ya “Mikono safi,
Tanzania salama” inayolenga kuelimisha wananchi juu ya kujikinga dhidi
ya maambukizi ya virusi vya Corona.
“Kwa wanaotaka kwenda kuwatembelea
Wazee kijijini, wasubiri Corona iishe, kwasababu tunaona watu watatoka
kwenye miji ambayo inamaambukizi wanaenda vijijini kuwatembelea wazazi
ambao umri wao umeenda, inawezekana wana magonjwa ya uzeeni,
kunauwezekano mkubwa wakuwaambukiza huko” alisema.
Aliendelea kusisitiza kuwa, katika
maeneo yote yenye msongamano hususan maeneo ya biashara na huduma za
Afya, waweke utaratibu mzuri, utaosaidia wateja kukaa umbali wa mita
moja au zaidi pindi wanaposubiri kupata huduma, hali itayosaidia kukata
mnyororo wa maambukizi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.
“Maeneo ya kutoa huduma mbali
mbali, ikiwemo Hospitali na vituo vya Afya, waweke utaratibu mzuri, watu
wanaokuja kupata huduma wakae katika utaratibu wa mita moja au zaidi
ili watu hawa wasiweze kuambukizana maradhi, lengo likiwa kukata
mnyororo wa maambukizi kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine ”
alisema
Aliendelea kusema, ni muhimu
uvaaji wa Barakoa uzingatiwe katika ngazi zote, hasa katika maeneo yenye
mkusanyiko wa watu, huku akisisitiza kuwa, ni muhimu kuzichoma moto
Barakoa zilizotumika ili kuepusha usambaaji wa magonjwa ya mlipuko
yanayoweza kujitokeza.
“Tunasisitiza uvaaji wa Barakoa,
hasa unapokuwa kwenye mkusanyiko wa watu, lakini barakoa sio kitu salama
baada ya kumaliza kukitumia, kinakuwa kichafu na maambukizi, kwa
mantiki hiyo, hakikisha unaitupa sehemu salama na unachoma moto ili mtu
mwingine asiweze kuikokota na kuitumia tena ” alisema
Aidha, Dkt. Subi amesema kuwa,
bado elimu ya kunawa mikono kwa sabuni na maji safi yanayotiririka
haijaeleleweka vizuri, hivyo kuitaka timu ya hamasa kuongeza nguvu
katika hatua zote tano za unawaji mikono ili elimu hiyo isaidie katika
mapambano dhidi ya maambukizi ya virusi vya Corona.
“Tunaposema kunawa mikono kwa maji
safi yanayotiririka na sabuni tunamaana kwamba, unapokwenda kunawa
hakikisha sabuni imekolea vizuri kwenye kiganja cha mikono, hakikisha
umesugua vizuri, povu la sabuni limeshika vizuri, na hakikisha umenawa
vizuri mbele, nyuma, kwenye vidole na kila eneo la mikono vizuri kwa
sekunde zisizopungua 20″alisema
Akiwasilisha ripoti ya utendaji
kazi wa kampeni ya “mikono safi, Tanzania salama,” Mkuu wa Kitengo cha
maji na usafi wa mazingira, Wizara ya Afya, Ndg. Anyitike Mwakitalima
ameweka wazi kuwa, mpaka sasa timu hiyo ya uhamasishaji imeshatembelea
jumla ya maeneo 145 kati ya 213 yaliopangwa yametembelewa ikiwa ni sawa
na asilimia 68.
Mbali na hayo amesema kuwa, licha
ya kutoa elimu ya tahadhari, kikosi cha uhamasishaji kimekuwa kikitoa
zawadi kwa taasisi na watu ambao wanazingatia maelekezo yanayotolewa na
Wizara, vikiwemo vitakasa mikono (Sanitizer), viang’azi (Reflectors) na
khanga za Kampeni.
No comments :
Post a Comment