*****************************
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amepokea taarifa ya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali
katika tasnia ya kilimo cha mkonge mkoani Tangana kuagiza mapendekezo
yaliyotolewa na
timu hiyo yakiwemo ya kurejeshwa Serikalini kwa nyumba
na. 176 eneo la Bombo ambayo ilimilikishwa kwa Bw. Salum Shamte
yafanyiwe kazi.
Nyumba
nyingine zilizopendekezwa kurejeshwa Serikalini ni pamoja na nyumba kumi
zilizoko ndani ya Jiji la Tanga katika maeneo ya Raskazone, Bombo,
Nguvumali na Market street ambazo zilinunuliwa na watumishi hao kwa
udanganyifu.
Waziri Mkuu
ametoa maagizo hayo leo (Jumapili, Machi 1, 2020) wakati akizungumza na
watumishi wa halmashauri za mkoa wa Tanga, viongozi wa taasisi
mbalimbali, wadau wa zao la mkonge pamoja na viongozi wa dini kwenye
ukumbi wa hoteli ya Naivera.
Hata hivyo,
Waziri Mkuu ametoa wito kwa wawekezaji ambao wanamiliki mashamba ya
mkonge yenye ukubwa wa zaidi ya ekari 2,000 ambao hawajayaendeleza
wayaendeleze wakishindwa yatachukuliwa na kugawiwa kwa wananchi.
Timu hiyo
maalum ya uchunguzi iliundwa na Waziri Mkuu na ilifanya uchunguzi mkoani
Tanga kuanzia tarehe 29/11/2019 hadi tarehe 07/02/2020. Timu hiyo
iliyokuwa na wajumbe 13 ilihusisha maafisa kutoka ofisi mbalimbali za
Serikali.
Uchunguzi huo
maalum ulihusu masuala mbalimbali katika tasnia ya zao la mkonge mkoani
Tanga ambayo ni pamoja na uzalishaji wa mkonge, bei ya zao la mkonge
katika soko la ndani na nje ya nchi.
Pia,
ilichunguza kuhusu mali za iliyokuwa Mamlaka ya mkonge nchini, ubia kati
ya Kampuni ya Katani Limited na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii
(NSSF), Utendaji kazi wa Kampuni ya Katani Ltd na pia Utendaji kazi wa
Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB).
Awali,Mwenyekiti
wa timu hiyo Bw. Gerald Kusaya alisema timu ilibaini kuwa Kampuni ya
Katani Ltd tokea mwanzo ilikuwa na mgongano wa kimaslahi na kupelekea
kuhujumu uchumi kwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wake Bw. Salum Shamte
alikuwa mtumishi wa umma na alishiriki vikao vyote vya ubinafsishaji wa
Mamlaka ya Mkonge ilhali akijua kuwa ana maslahi kwenye Kampuni
inayonunua.
“Kwa kuwa
uchunguzi umebaini viongozi na wanahisa wa Katani Ltd waliohusika
kuingia mikataba walikuwa watumishi wa Mamlaka ya Mkonge wakati wa
mchakato wote wa ubinafsishaji hivyo walitumia vibaya madaraka yao kwa
kuishawishi Serikali kuingia mkataba huo usiokuwa na tija kwa Serikali
bali kwa manufaa yao binafsi. Hivyo, Timu imeandaa taratibu kwa ajili ya
wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.”
Bw. Kusaya
amesema timu hiyo inapendekeza kuwa Serikali itoe fedha kwa ajili ya
kazi ya kuyapima upya mashamba matano ya Mwelya, Ngombezi, Hale, Magunga
na Magoma ili wananchi wanaoendelea kutumia mashamba hayo kwa
kukodishwa na Bodi ya Mkonge kama ilivyokubalika kwenye Baraza la
Mawaziri mwaka 2005 ili waweze kupewa Hati ndogo (leasehold tittle);
Alisema timu
inapendekeza nyumba 30 zilizopo eneo la Muheza, ambazo baadhi zilitolewa
kwa wananchi waliokuwa watumishi wa Mamlaka ya Mkonge na baadhi kuachwa
kwa ajili ya makazi ziendelee kuwa mali ya wananchi hao kwa kuwa eneo
hilo kwa sasa lipo chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Muheza.
“Nyumba 22
zilizoko ndani ya mashamba ya mkonge na maeneo ya kiwanda cha TANCORD
ziendelee kubaki mali ya Serikali na nyumba iliyoko katika kiwanja Na.
176 eneo la Bombo iliyohamishwa kwenda kwa Ndg. Salum Shamte irejeshwe
Serikalini kwa njia ya urekebishaji wa daftari la Msajili wa Hati.”
Kwa upande
wao, viongozi wa mkoa wa Tanga wakiwemo wabunge wamemshukuru Waziri Mkuu
kwa kuunda timu hiyo ya uchunguzi wa zao la mkonge kwa kuwa mapendekezo
yake yamejibu changamoto zilizokuwa zinalikabili zao hilo.
Wamesema
mapendekezo yaliyotolewa na timu hiyo yanakwenda kufufua kilimo cha zao
la mkonge hivyo kuongeza tija kwa wakulima wa mkonge mkoani Tanga.
No comments :
Post a Comment